TIMU ya Simba imemkaribisha kwenye Ligi Kuu ya NBC kocha mpya wa Namungo Juma Mgunda baada ya kuifunga timu hiyo 3-0 katika mchezo uliochezwa uwanja wa KMC Dar es Salaam.
Ilimchukua dakika 5 tu mlinzi wa kulia wa Simba Shomari Kapombe ambaye pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kufungua ukurasa wa mabao baada ya kufunga kabla ya kiungo wa timu hiyo Jean Ahoua kufunga bao la pili dakika ya 34 hivyo kuifanya Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo kiungo wa timu hiyo Debora Fernandes aliweza kuongeza bao la 3 dakika ya 84 ya mchezo huo hivyo kufanya matokeo kuwa 3-0 ikiwa ni mechi ya kwanza mara baada ya Juma Mgunda kutajwa kurithi mikoba ya Mwinyi Zahera kama kocha mkuu wa timu hiyo.
Michezo mingine iliyopigwa imeshuhudia Singida Black Stars ikiifunga Fountain Gate mabao 2-0 kwenye uwanja wa Liti, Singida huku Azam ikipata ushindi mnono wa mabao 4-1 nyumbani dhidi ya timu ya KenGold ya Mbeya kwenyw uwanja wa Azam Complex, Dar.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho ambapo Coastal Union itawakaribisha Yanga katika Uwanja wa Sheikhe Amri Abeid jijini Arusha,Prisons watawakaribisha KMC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Dodoma Jiji watawakaribisha JKT Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma