SINGIDA, FOUNTAIN, AZAM ZATAMBA LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo iliyochezwa katika mikoa ya Arusha,Singida na Dar es salaam.

Katika dimba la Singida, timu ya Singida Black Stars waliwakaribisha Pamba Jiji katika mchezo uliokuwa na kasi na ushindani mkubwa ulioshuhudia wenyeji wakionyesha ubora wao kwa kupata ushindi wa 3-1.

Mabao mawili yaliwekwa kambani na Ndumumwe Mossi aliyefunga dakika ya 21 na kuongeza lingine dakika ya 53 huku Horso Malanga akijiunga kwenye orodha ya wafungaji kwa bao la dakika ya 70 na kuhakikisha Singida wanakusanya alama zote tatu.
Bao pekee la Pamba Jiji lilifungwa na Henry Lutonja dakika ya 90 ingawa haikutosha kuzuia ushindi wa Singida.

Wakati huo huo, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Fountain Gate walikuwa na kibarua kigumu dhidi ya Coastal Union walioanza mchezo kwa kasi wakiandika bao la mapema dakika ya 2 kupitia kwa Shiza Kichuya.

Hata hivyo, Fountain Gate walirudi na kusawazisha kupitia Chukwunonye Obasi dakika ya 14 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 33 huku Henry David akifunga bao la tatu dakika ya 70 na kufanya matumaini ya ushindi kuwa makubwa kwa wenyeji.

Coastal Union hawakukata tamaa, wakipata bao la pili dakika za nyongeza (90+3) kupitia Meshack Mwamita, lakini juhudi zao hazikutosha kubadili ubao wa matokeo.

Katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam FC walikuwa wenyeji wa Namungo katika mchezo uliokuwa wa ushindani mkubwa huku timu zote zikionesha nidhamu ya hali ya juu.

Azam walifanikiwa kupata bao pekee la mchezo dakika ya 41 kwa njia ya penalti iliyofungwa kwa utulivu na Feisal Salum aliandika bao lake la kumi msimu huu lililodumu hadi mwisho na kuwapatia ushindi muhimu.

Kwa ujumla, michezo hiyo imeendelea kuonyesha ushindani mkubwa ndani ya ligi, huku timu zikionyesha nia ya kupambana hadi dakika ya mwisho kusaka alama tatu muhimu.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *