Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

TAARIFA YA KAMATI YA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Mei 9, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 169: Simba SC 2-2 Young Africans

Klabu ya Young Africans imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Saalam kuelekea mchezo tajwa hapo juu Mei3, 2026. Young Africans iliwasili uwanjani saa 10:35 alasiri badala ya saa 10:30 alasiri jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Young Africans imetozwa faini ya Sh. 30,000,000 (milioni thelathini) kwa kosa la wachezaji na maofisa wake wa ufundi kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam badala yake walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja upande wa pili wa Barabara kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi.

Meneja wa Klabu ya Young Africans Walter Harson amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Simba Clatous Chama kwenye mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 45:2(2.1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa Wengine wa Ufundi.

Shabiki wa klabu ya Young Africans aliyetambulika kwa jina la Mohamed Ally Mposo ambae amekuwa akiambatana na maofisa wa ufundi wa klabu hiyo amefungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi 12 kwa kosa la kuingia kwenye eneo la kuchezea wakati wa mapumziko na kumwaga vimiminika kitendo kilichotafsiriwa kama imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 Mechi Namba 154: Mtibwa Sugar 0-1 Dodoma Jiji FC

Klabu ya Dodoma Jiji ya Dodoma imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) huku wakiwa pungufu bila kuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kikanuni, Dodoma Jiji iliwakilishwa na wawakilishi wawili pekee badala ya watano huku wakiwa hawana vifaa kamili kinyume na matakwa ya kanuni 17:2 (2.2).

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Ligi ya Championship ya NBC

Mechi Namba 172: Geita Gold 6-1 Hausung FC

Klabu ya Hausung ya Mkoani Njombe imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la maofisa wake kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kwa dakika 20, maofisa hao walifika saa 1:35 usiku badala ya saa 1:15 usiku kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2 (2.2) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo

Mechi Namba 182: TMA FC 2-0 Gunners FC

Mchezaji wa TMA Said Kulwa amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuonekana na chupa yenye kimiminika na kumwaga kimiminika hicho kwenye upande wa timu ngeni wakati wa ukaguzi wa uwanja jambo lililotafsiriwa kama imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.5) ya Championship kuhusu Udhibiti kwaWachezaji.

Wachezaji Mohamed Lipangala na Joel Stephano wa TMA FC, wamefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kila mmoja kwa kosa la kuonekana wakichimbia vitu kwenye nguzo ya timu yao jambo lililo tafsiriwa kama imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.5) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi Namba 190: Mbeya Kwanza vs Hausung FC

Klabu ya Hausung FC ya mkoani Njombe imepoteza mchezo tajwa hapo juu na Timu ya Mbeya Kwanza ya mkoani Tabora imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama (3) kwa kosa la Hausung FC kushindwa kufika kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora bila sababu za msingi na zinazokubalika hivyo kusababisha mchezo huo kushindwa kufanyika.

Sambamba na adhabu hiyo, Hausung FC imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi)na kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo Pamoja na kupokwa alama tatu (3) katika msimamo wa Ligi ya Championship.Pia Mwenyekiti wa klabu ya Hausung FC, Erasto Haule amefungiwa kwa kipindi cha mwakammoja (1) kwa kosa la klabu yake kushindwa kufika uwanjani.

Adhabu hizi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 31:1(1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship kuhusu Kutofika Uwanjani.

First League

Mechi Namba 37B: Alliance FC 0-3 IAA FC

Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la maofisa wake kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwakosa la shabiki wake kumvamia mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Julius Ottu na kumpiga ngumi usoni.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 41A: Nyumbu FC 1-1 Moro Kids

Timu ya Moro Kids ya Mkoani Morogoro imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye uwanja wa mchezo Filbert Bayi Mkoani Pwani. Moro Kids ilifika saa 8:35 badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 43A: Magnet FC 0-2 Bandari Tanzania

Klabu ya Magnet ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la maofisa wake kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi yamchezo (MCM) kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Maofisa hao ilipofika muda wa kikao waligoma kushiriki kikao hicho kwa madai wanamsubiri mwenye timu afike ndipo washiriki kikao hicho, hata alipofika kiongozi huyo (Tuntufye Mwambusi) bado maofisa hao hawakushiriki kikao hicho kwa madai ya kutojibiwa barua yao waliyoiwasilisha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 46A: Green Warriors 1-5 Magnet

Timu ya Magnet ya Mkoani Dar es Salaam imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye uwanja wa mchezo Filbert Bayi Mkoani Pwani. Magnet ilifika saa 8:35 badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo

Imetolewa na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

 

One comment

  1. Mechi kati ya yanga vs namumgo
    Kmc kunyimwa penat mbili za wazi kwa matukio mawili ya foul ndani ya penat area shedrack boka kumsukuma mchezaji wa namungo hilo vip

Join the Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *