MACHO na masikio ya mashabiki wa soka Tanzania leo yataelekezwa Azam Complex, Chamazi, ambapo vigogo wa Dar es Salaam, Azam na Simba watakutana katika pambano kubwa linalojulikana kama Mzizima Derby.
Mchezo huu unasubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na ushindani wa kihistoria wa timu hizi mbili na umuhimu wake kwenye mbio za juu ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Azam FC wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na morali kubwa baada ya ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars, huku Simba SC nao wakija na kujiamini kufuatia ushindi wa 2-0 walioupata dhidi ya Coastal Union katika mchezo wao uliopita.
Hali hiyo inafanya mechi ya leo kutabirika kuwa ya ushindani mkali, presha kubwa na vita ya mbinu kutoka makocha na mabenchi ya ufundi ya timu zote.
Kwa upande wa msimamo, Simba wanaonekana kuwa na presha ya kutafuta ushindi ili kuendelea kusogea karibu na kileleni, wakati Azam wakitaka kutumia faida ya kucheza nyumbani kuimarisha nafasi yao kwenye timu za juu.
Hii si mechi ya kawaida, bali ni mchezo wenye uzito wa alama tatu ambazo zinaweza kubadili kabisa sura ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu.
Historia ya timu hizi imekuwa na ushindani wa hali ya juu, huku Simba mara nyingi wakiwa na rekodi nzuri zaidi kwenye mechi zao za ligi dhidi ya Azam.
Hata hivyo, Azam walionyesha ubora kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Japhte Kitambala ma Iddy Seleman jambo ambalo linaifanya Simba kuingia leo wakiwa na kiu ya kulipa kisasi mbele ya mashabiki wao ugenini.
Kinachoongeza ladha zaidi ni ubora wa vikosi vya timu zote mbili ambapo Simba wanaingia na nguvu ya safu yao ya ushambuliaji pamoja na uzoefu mkubwa wa mechi za presha, wakati Azam wana kikosi chenye nidhamu ya kiufundi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, jambo linaloweza kufanya mchezo huu kuamuliwa kwa makosa madogo sana.
Kwa kifupi, leo Chamazi kutakuwa hapatoshi. Ni mechi ya heshima, pointi na tambo za Dar es Salaam. Mashabiki wanatarajia kuona soka la kiwango cha juu, mabao, kasi na ‘udambwi’ wa derby halisi ya Mzizima.
Wakati huo huo mkoani Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid timu ya TRA itaialika Singida Black Stars kwenye mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri ikiwa ni sambamba na mchezo wa Mzizima Derby utakaopigwa usiku.