IKITAMATIKA kwa mzunguko wa 30 ligi ya Championship ya NBC na kushuhudia Mtibwa Sugar ikiibuka mabingwa wa ligi hiyo na Mbeya City kupanda daraja timu za Stand United ya Shinyanga na Geita Gold ya Geita bado zina nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.
Stand iliyomaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itacheza michezo ya mtoano kwenye uwanja wa nyumbani na ugenini dhidi ya Geita Gold na mshindi wa mchezo huo atacheza na timu ya Ligi Kuu ya NBC itakayopoteza mchezo wake wa mtoano.
Mchezo wa mwisho timu hizo kukutana ulikuwa mchezo wa kufunga pazia la ligi ya Championship ya NBC mzunguko wa 30 na kumalizika kwa sare ya 1-1 timu ya Stand ikiwa nyumbani kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Mshindi wa jumla wa michezo yote miwili atacheza na timu itakayopoteza mchezo wake wa mtoano kutoka Ligi Kuu ya NBC na endapo timu ya Championship itashinda itapanda Ligi Kuu na endapo timu ya Ligi Kuu itashinda basi itasalia kwenye ligi hiyo kwa msimu wa 2025/26.
 
					