TIMU ya Transit Camp imerejea katika matokeo ya ushindi baada ya kuifunga KenGold bao moja kwenye uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kusalia na alama zote tatu.
Mchezo huo uliopigwa uwanja wa TFF Center Kigamboni ulishuhudia Adam Uledi wa Transit Camp akiibuka shujaa kwa kuifungia Transit bao pekee kipindi cha pili kwa mkwaju wa penati huku likiwa bao la 11 kwake akiendelea kuongoza kwenye vinara wa mabao katika ligi ya Championship ya NBC.
Ushindi huo unaifanya Transit kufikisha alama 33 na kupanda hadi nafasi ya tatu ya msimamo ikiwa nyuma ya kinara wa ligi hiyo Geita Gold kwa alama nne pekee.
Mkoani Lindi kwenye uwanja wa Ilulu timu ya Bigman ilikuwa mwenyeji wa Geita Gold na kushuhudia mchezo huo ukikamilika kwa timu hizo kutoka sare ya bao moja.
Geita inayoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa alama 37 imeshindwa kukusanya alama zote nyumbani kwa Bigman ambayo imeizidi alama 17 huku timu hiyo (Bigman) ikishika nafasi ya saba kwenye msimamo.
Hii ni sare ya pili mfululizo kwa timu ya Bigman kwenye uwanja wa nyumbani baada ya mchezo uliopita kulazimishwa sare na timu ya African Sports kutoka Tanga.