Tag: #LIGIKUU #NBCPL #AZAM

NBC CHAMPIONSHIP MZUNGUKO WA 16 KUPIGWA MIKOA MITATU LEO.

MZUNGUKO wa 16 wa Ligi ya Championship ya NBC unaanza kuchezwa leo Januari 24 kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Mchezo wa kwanza utazikutanisha Mbeya Kwanza dhidi ya Songea United kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa pili utazikutanisha African Sports dhidi ya Cosmopolitan kwenye uwanja wa TFF Center, Mnyanjani – Tanga kuanzia saa 10 alasiri.

Mkoani Pwani Green Warriors itaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Mabatini mchezo ambao utachezwa kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mtibwa Sugar ndio kinara wa Ligi ya Championship ya NBC mpaka sasa ikiwa na alama 38 kwenye michezo 15 ya kwanza huku Biashara United ikiburuza mkia ikiwa na alama moja baada ya michezo 15.

LIGI KUU NBC YA NNE KWA UBORA AFRIKA

Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu ya Tanzania (NBC Premier League) kuwa Ligi ya nne kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024.

Ligi hiyo imepanda kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya sita mwaka 2023 hadi nafasi ya nne ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia.

Kwa mujibu wa taarifa ya IFFHS kwa upande wa Afrika nchi zilizoko chini ya Shirikisho la Soka (CAF) Ligi Kuu ya Misri inayofahamika kama Nile Premier League ndio kinara kwa ubora Afrika.

Nafasi ya pili inashikiliwa na Botola Pro ambayo ni Ligi Kuu ya Morocco huku League 1 ya Algeria ikishika nafasi ya tatu kwa ubora mwaka 2024.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania imekwea hadi nafasi ya nne barani Afrika kutokana na ligi hiyo kuwa na usimamizi bora kuanzia Serikali, Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Klabu zinazoshiriki ligi hiyo, wadhamini mbalimbali wanavyounga mkono pamoja na mashabiki.

FEISAL BINGWA WA KUPIKA MABAO LIGI KUU YA NBC.

KIUNGO wa Azam FC Feisal Salum ameendelea kuonyesha ubora aliokuwa nao msimu uliopita ambapo hadi sasa kiungo huyo anaongoza msimamo wa kutoa pasi nyingi zilizozaa mabao (9).

Feisal hadi sasa ameongeza pasi mbili za mabao zaidi ya alizimaliza nazo msimu uliopita ambapo alitoa pasi saba huku kinara akiibuka Kipre Junior aliyekuwa akicheza timu moja na Feisal.

Jean Ahoua wa Simba anamfuatia Feisal kwa karibu akiwa nazo tano sawa na winga wa Fountain Gate Salum Kihimbwa.

Ki Aziz, Pacome Zouzoua na Clement Mzize wa timu ya Yanga wanafuatia wakiwa na pasi nne kila mmoja sawa na Josephat Arthur Bada wa Singida Black Stars mwenye pasi nne pia.

Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kurejea Machi, 2025 kushuhudia namna vita hii ya kupika mabao itakavyokamilika ikipisha michuano ya CHAN inayoandaliwa Tanzania.