Tag: #LIGIKUU #NBCPL #AZAM #YANGA #SIMBA #KMC #JKT #MASHUJAA #KENGOLD #DODOMAJIJI #PAMBAJIJI #KAGERASUGAR #SINGIDABLACKSTARS #FOUNTAINGATE #NAMUNGO

AHOUA ‘HACHEKI NA WOWOTE’ LIGI KUU NBC.

JEAN Ahoua wa timu ya Simba ameendelea kuwa na msimu bora wa Ligi Kuu ya NBC hadi sasa baada ya kuhusika kwenye mabao 19 huku timu yake ikisalia na michezo nane kutamatisha msimu.

Ahoua aliyesajiliwa na Simba akitokea Asec Mimosa mpaka sasa amehusika katika mabao 19  baada ya kufanikiwa  kufunga mabao 12 kutoa pasi zilizozaa mabao saba hivyo kufanya kuwa mchezaji aliyehusika katika mabao mengi kuliko mchezaji yeyote.

Prince Dube  ambaye amesajiliwa  na timu ya Young Africans akitokea Azam  anashikilia nafasi ya pili akiwa amehusika katika mabao 17 baada ya kufunga mabao 10 na kutoa pasi za mabao saba.

Mpinzani wa karibu wa Dube ni Feisal Salum wa Azam akiwa amefanikiwa kutoa pasi za mwisho 12 na kufunga mabao manne  hivyo kuhusika katika mabao 16.

Kwa upande wake Aziz Ki wa Young Africans amefanikiwa kufunga mabao saba na kutoa pasi za mabao saba hivyo kuhusika katika mabao 14.

Pacome Zouzoua na Clement Mzize wa Young Africans wote wamehusika katika mabao 13 kila mmoja  huku Pacome akifunga mabao saba na kutoa pasi za mwisho sita huku Mzize akifunga mabao 10 na kutoa pasi za mwisho tatu.

WAKALI WA MGUU WA KUSHOTO LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC inazidi kushika kasi ikiwa ni takribani michezo 183 imeshachezwa huku mabao 406 yakiwa yamefungwa ikiwemo yaliyofungwa kwa mguu wa kushoto na wakali wafuatao.

Ki Azizi ni kiungo mshambuliaji wa Young African katika msimu huu wa 2024/2025 ameshatia wavuni mabao sita kwa mguu wake wa kushoto kati ya mabao saba aliyofunga mpaka sasa.

Winga wa  timu ya Azam, Gibril Sillah, ameshatia wavuni mabao matano  kwa mguu wake wa kushoto kati ya saba ambayo ameshafunga mpaka sasa.

Offen Chikola wa Tabora United ameshatikisa nyavu mara tano kwa mguu wa kushoto kati ya mabao saba aliyofunga msimu huu.

Nassor Saaduni ni mshambuliaji wa Azam akiwa amefanikiwa kuingia langoni mwa wapinzani wao mara tano akitumia mguu wake wa kushoto.

Mchezaji Selemani Bwenzi aliyeingia dirisha dogo kwa timu ya KenGold mkali huyo mpaka sasa amefanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani akitumia mguu wake wa kushoto.

Naye mchezaji wa Namungo Joshua Ibrahimu kafanikiwa kuweka mpira wavuni mara nne akitumia mguu wake wa kushoto.

‘TSHABALALA’ MKALI WA PASI ZA MWISHO LIGI KUU NBC.

BEKI wa timu ya Simba,Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye kinara wa  kutoa pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2024/2025 akiwa nazo nne.

Tshabalala alitoa pasi za mwisho na kuisaidia timu yake kupata alama katika michezo ya Simba dhidi ya timu za Fountain Gate (1),Dodoma Jiji (1),Tabora (1) na Kagera Sugar.

Nafasi ya pili inashikiliwa na beki wa Singida Black Stars, Ande Koffi akiwa ametoa pasi tatu katika mechi za Singida dhidi ya Fountain Gate (1),Pamba Jiji (1) na KenGold (1).

Datius Peter wa Kagera Sugar anafuata akiwa na pasi za mwisho tatu alizotoa katika michezo ya Kagera Sugar dhidi ya timu za Pamba Jiji (1),KenGold (1) na mchezo wa Mashujaa (1).

Beki wa Simba, Shomari Kapombe, amepiga pasi za mwisho tatu alizoweza kutoka katika michezo ya timu yake dhidi ya Prisons (2) na Fountain Gate (1).

Beki na nahodha wa Fountain Gate,Amos Kadikilo anashika nafasi ya tano akiwa na pasi za mwisho tatu alizopata katika michezo ya Fountain Gate dhidi ya Namungo (1) na Tanzania Prisons (2).

KENGOLD,MASHUJAA HAKUNA MBABE LIGI KUU NBC

MZUNGUKO wa 23 wa Ligi Kuu ya NBC umeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa uwanja wa Sokoine Mbeya majira ya saa kumi alasiri.

Mchezo ulianza kwa timu zote kusomana kwa kuwa zilikuwa zinahitaji kupata alama tatu mhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi.

Iliwachukua dakika 21 kwa Mashujaa kupata bao la kwanza kupitia mchezaji Jafari Kibaya ambapo dakika  ya 26 mchezaji wa Mashujaa, Yusuf Dunia, alijifunga na kufanya mchezo kusomeka 1-1 matokeo yaliyobaki mpaka mwisho wa kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa ambapo dakika ya 47 mchezaji wa KenGold, Mishamo Daudi, aliiongezea timu yake bao la pili kabla ya Ally Nassor wa Mashujaa kuongeza bao la pili kwa mashujaa  hivyo ubao kusomeka 2-2 mpaka mwisho wa mchezo.

KenGold walifikisha alama 16 wakiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku Mashujaa wakifikisha alama 24 wakiwa nafasi ya 10.

Mchezaji wa Mashujaa,Ally Nassor ‘Ufudu’ alitangazwa kuwa nyota wa mchezo huo.Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo mitatu.

KENGOLD ,MASHUJAA HAPATOSHI SOKOINE LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo kwa mzunguko wa 23 kuanza rasmi katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya majira ya saa kumi alasiri.

Timu ya KenGold ndio mwenyeji wa mchezo huo ikiikaribisha timu ya Mashujaa kutoka Kigoma ambapo timu zote mbili zikitaka alama tatu muhimu.

KenGold  iko nafasi ya 16  kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama 15 huku wakifunga mabao 18 na kuruhusu mabao 38 .

Mashujaa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama 23 kufungaa mabao 17 na kuruhusu mabao 26.

Mchezaji wa kuchungwa katika mchezo huo wa kikosi cha  KenGold  ni Seleman Bwenzi akiwa amecheza michezo sita na kufunga mabao matano ikiwa ni mchezaji aliyeingia kwenye dirisha dogo la usajili.

Kwa upande wa Mahujaa mchezaji wa kuchungwa ni David Ulomi akiwa amefunga mabao manne.