LIGI Kuu ya NBC imezidi kushika kasi JKT Tanzania iliwakaribisha timu ya Young Africans katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam jana.
Mchezo huo ulipigwa majira ya saa kumi na robo ambapo timu zote zilionekana kuzitaka alama zote ili ziweze kuwa katika nafasi nzuri
Yanga walizitaka alama hizo ili waweze kuendelea kukaa kileleni huku JKT ikitamani kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mpaka dakika 45 zinatamatika timu zote zilienda mapumziko bila ya kufungana hivyo kuwapa kazi ngumu makocha wao kujiuliza nini cha kufanya kwa kipindi cha pili ili kuweza kupata matokeo.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na timu zote zilifanya mabadiliko ya vikosi mara kwa mara ili kuweza kuona kama wanaweza kushinda mchezo huo.
Mpaka dakika 90 za mchezo huo zinatamatika sio wenyeji JKT Tanzania ama wageni Young Africans walioambulia goli lolote hivyo mchezo kumalizika kwa sare pacha ya kutokufungana ikiwa ni msimu wa pili kwa Young Africans kutokushinda katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo mitatu ambapo Mashujaa watawakaribisha Coastal Union katika uwanja wa Lake Tanganyika,Simba ikiumana na Tanzania Prisons uwanja wa KMC Complex na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Tabora United uwanjani Kaitaba mkoani Kagera.