Author: Honest Mwanitega

‘KIVUMBI’ CHA LIGI KUU YA NBC KUENDELEA.

BAADA ya Tabora United na Fountain Gate kupata ushindi hapo jana Ligi Kuu ya NBC inaendelea tena leo kwa michezo miwili itakayopigwa mikoa miwili tofauti.

Saa 10:00 alasiri timu ya Singida BS ya Singida itakuwa mwenyeji wa KMC ya Dar kwenye uwanja wa Liti, Singida.

Singida imeshinda michezo yote miwili ya kwanza msimu huu iliyocheza ugenini na leo itaikaribisha KMC kwenye mchezo wa kwanza katika uwanja wa nyumbani.

Mchezo wa pili utachezwa saa 10:00 alasiri kama mchezo wa awali kati ya timu ya Dodoma Jiji na Namungo ya Lindi kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.

Timu zote mbili hazijapata ushindi kwenye mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC hadi sasa na hivyo kufanya mchezo huu kuwa na ushindani mkubwa.

LIGI KUU YA NBC KUENDELEA LEO.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo miwili baada ya kusimama kwa takribani siku 13 kupisha michezo ya kimataifa.

Mchezo wa kwanza utachezwa saa 8:00 mchana kati ya timu ya Tabora United itakayokuwa nyumbani kuikaribisha Kagera Sugar kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora ukiwa mchezo wa kwanza wa Tabora kwenye uwanja wa nyumbani.

Mchezo wa mwisho utapigwa saa 10:15 alasiri kati ya Fountain Gate na KenGold kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mkoani Manyara wilaya ya Babati.

Huu ni mchezo wa kwanza kwa timu ya Fountain kucheza nyumbani ukiwa pia mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC kuchezwa mkoani Manyara kwenye wilaya ya Babati.

HAWA HAPA WABABE WA AGOSTI LIGI KUU YA NBC.

TUZO za Ligi Kuu ya NBC zimetangazwa huku timu ya Simba ikishinda tuzo mbili za mchezaji bora wa mwezi na kocha bora wa mwezi Agosti.

Mchezaji Jean Ahoua ameshinda tuzo ya mchezaji bora mwezi Agosti baada ya kufanikiwa kufunga bao moja na kutoa pasi tatu za mabao na kuifanya timu yake kuongoza msimamo baada ya kucheza michezo miwili bila kupoteza.

Kocha wa Simba Davids Fadlu ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwazidi Patrick Aussems wa Singida Black Stars na Abdallah Mohamed wa mashujaa alioingia nao fainali katika mchakato huo.

Kwa upande wa tuzo ya Meneja Bora wa uwanja imeenda kwa Ashraf Omar wa uwanja wa Meja Isamuhyo unaomilikiwa na timu ya JKT Tanzania kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti na miundombinu ya uwanja.

AFRICAN SPORTS BINGWA FIRST LEAGUE 2023/24.

TIMU ya African Sports ya Tanga imefanikiwa kuwa bingwa wa Ligi ya First League msimu wa 2023/24 baada ya kuifunga Kiluvya ya Dar es Salaam bao 1-0.

African Sports imefanikiwa kutwaa ubingwa huo bila kupoteza mchezo wowote katika mashindano ya First League Nane Bora yaliyofanyika Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani.

African Sports imefanikiwa kupanda daraja hadi Ligi ya Championship ya NBC baada ya kushuka msimu uliopita kwa kupoteza mchezo wa mtoano dhidi ya TMA ya Arusha.

Timu ya Kiluvya iliyopoteza fainali imefanikiwa kuibuka mshindi wa pili na kupanda Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/25.

Timu za Malimao iliyoibuka mshindi wa tatu na Mwadui iliyokuwa mshindi wa nne zitacheza michezo ya mtoano na timu zilizopoteza michezo yake ya mtoano kwenye ligi ya Championship ya NBC ili kutafuta nafasi ya kucheza ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/25.

KILUVYA, AFRICAN SPORTS ZATINGA FAINALI YA FIRST LEAGUE NANE BORA.

TIMU za Kiluvya ya Dar es Salaam na African Sports ya Tanga zimefanikiwa kutinga fainali ya mashindano ya First League Nane Bora baada ya kushinda michezo yao ya nusu fainali.

Kiluvya iliyocheza dhidi ya Malimao ya Dar es Salaam imeshinda kwa mikwaju ya penati 4-2 baada ya kutoka suluhu katika dakika 120.

African Sports ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Mwadui ya Shinyanga kwenye mchezo ulioshuhudia Mwadui wakionyeshwa kadi mbili nyekundu huku moja ikionyeshwa baada ya vurugu zilizotokea uwanjani dakika chache kabla ya mchezo kumalizika.

Matokeo hayo yanazifanya timu za Kiluvya na African Sports kufuzu moja kwa moja kucheza Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/25 huku fainali ya mashindano hayo ikitarajiwa kupigwa Mei 11, kwenye uwanja wa Mkwakwani ili kupata bingwa wa First League msimu wa 2023/24.

Timu za Mwadui na Malimao zitacheza mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu Mei 11 huku pia zikiwa na nafasi ya kupanda daraja msimu ujao ikiwa zitashinda michezo ya mtoano dhidi ya timu za Ligi ya Championship zitakazofungwa michezo ya mtoano.