Author: Honest Mwanitega

POLISI YAONESHA MAKALI, PAMBA HAIKAMATIKI

TIMU ya Polisi Tanzania imepata ushindi wa kwanza kwenye Ligi ya NBC Championship dhidi ya Ruvu Shooting kwa bao 1-0.

Ushindi huo ulihakikishwa mapema dakika ya 15 kwa bao la Denis Mushi na kufanya Ruvu Shooting kupoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya kufungwa dhidi ya FGA Talents mabao 2-1 katika mchezo wa ufunguzi.

Pamba ya Mwanza imeendeleza makali yake kwenye Ligi ya Championship baada ya leo kupata ushindi wa pili mfululizo kwa kuifunga Pan African ya jijini Dar es Salaam bao 1-0.

Bao pekee la Pamba katika mchezo huo likifungwa na Jamal Mtegeta kwa mkwaju wa penalti dakika ya 80.

Bao hilo ni la pili mfululizo kwa Jamal Mtegeta aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Dodoma Jiji, ambapo bao lingine alilifunga katika mchezo uliopita dhidi ya Cosmopolitan na Pamba ilishinda kwa mabao 4-0.

Ushindi huo unaifanya Pamba, kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo ikivuna pointi sita huku ikiwa haijaruhusu bao, wakati Pan African inarejea Dar es Salaam na pointi tatu ilizozivuna kwenye ushindi wa mabao 3-2 mbele ya Copco FC.

TABORA UTD YATAMBA

Mkoani Tabora Tanzania Prisons imepoteza mchezo wa pili mfululizo dhidi ya Tabora United kwa mabao 3-1.

Tabora UTD iliyopoteza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Azam kwa mabao 4-0 imepata ushindi huo wa kwanza kwa mabao ya John Ben aliefunga mawili na Erick Okutu huku bao la Prisons likifungwa na Samson Mbangula.

Prisons imeruhusu mabao sita kwenye michezo miwili iliyopita huku wakiwa na alama moja pekee waliyopata suluhu dhidi ya Singida Fountain Gate inayowaweka nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

PAMBA YAANZA KIBABE NBC CHAMPIONSHIP

LIGI ya NBC Championship imeendelea leo Septemba 11 kwa mchezo mmoja kuchezwa kati ya Pamba Jiji ya Mwanza na Cosmopoilitan ya Dar uliomalizika kwa Cosmo kupoteza kwa mabao 4-0.

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza umeshuhudiwa Cosmo waliokuwa mabingwa wa First League msimu wa 2022-2023 wakienda mapumziko wakiwa wameruhusu mabao matatu.

“Hii timu ina malengo yake, niliwaambia wachezaji tunahitaji sana kupanda Ligi Kuu ya NBC na endapo tukifungwa sana isiwe zaidi ya mechi mbili na wametekeleza majukumu tumeweza kupata ushindi” amesema kocha mkuu wa Pamba Mbwana Makata.

Kwa ushindi huo Pamba imepanda moja kwa moja kileleni mwa msimamo wa Ligi ya NBC Championship kwa tofauti ya idadi ya mabao juu ya timu za Mbeya City, Pan Africans na FGA Talents walioshinda michezo yao kwanza kama ilivyo kwa Pamba.

NBC CHAMPIONSHIP YAPAMBA MOTO

LIGI ya NBC Championship imeendelea Leo Septemba 10 kwa michezo minne kuchezwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana ulizikutanisha TMA na Stand United katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na kumalizika kwa suluhu.

Mchezo mwengine ulizikutanisha Mbuni na Biashara United saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na kumalizika kwa sare ya bao moja.

KenGold wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani Sokoine mkoani mbeya wakagawana alama na Transit Camp kwa sare ya bao moja.

FGA Talents imekuwa timu pekee kwa siku ya leo kuondoka na alama tatu baada ya kuwafunga Ruvu shooting mabao 2-1 kwenye uwanja wa Jamnhuri mkoani Morogoro.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho Septemba 11 kwa mchezo mmoja kuchezwa Pamba wakiwaalika Cosmopolitan kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.

NBC CHAMPIONSHIP KUENDELEA TENA LEO.

PAZIA la Ligi ya NBC Championship lilifunguliwa rasmi jana septemba, 9 kwa michezo mitatu kuchezwa.

Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa michezo minne kati ya TMA na Stand United kwenye uwanja Sheikh Amri Abeid,Arusha saa 8:00 mchana.

Mchezo wa pili utazikutanisha Ken Gold dhidi ya Transit Camp uwanja wa Sokoine, Mbeya saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa tatu ni Kati ya FGA Talents na Ruvu Shooting uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro saa 10:00 alasiri na Mchezo wa mwisho Mbuni atakuwa mwenyeji wa Biashara United kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha saa 10:00 alasiri.