Author: Honest Mwanitega

TMA KINARA NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU ya TMA FC ya Arusha imeendeleza mwanzo mzuri wa Ligi ya Championship ya NBC kwa ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Pan African ya Dar .

TMA imecheza mchezo wa nne mfululizo bila kupoteza ikifikisha alama nane na kuongoza msimamo wa Ligi ya Championship huku ikiwa mojawapo ya timu zilizopanda daraja msimu huu.

Mkoani Mara timu ya Biashara United imeshindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani na kulazimishwa sare ya bao moja dhidi ya Pamba ya Mwanza.

Ligi hiyo itaendelea tena Septemba 30 kwa michezo mitatu kati ya Stand United na Copco saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga huku Transit Camp ikicheza na Polisi Tanzania kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Green Warriors dhidi ya FGA Talents kwenye uwanja wa Uhuru, Dar michezo itakayochezwa saa 10:00 alasiri.

MASHUJAA, YANGA MILANGO MIGUMU

TIMU ya Mashujaa ya mkoani Kigoma na Yanga ya Dar zimetimiza michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC bila kuruhusu bao lolote.

Yanga imecheza michezo mitatu nyumbani ikikusanya alama zote tisa na kuongoza msimamo wa ligi pasipo kuruhusu bao huku ikifunga mabao 11 ambapo tisa kati ya hayo yamefungwa kipindi cha pili.

Mashujaa iliyopanda daraja baada ya kuiondoa Mbeya City ya Mbeya kwenye michezo ya mtoano imeendelea kuonesha ubabe ikicheza michezo mitatu kwenye uwanja wa nyumbani bila kupoteza wala kufungwa bao huku ikiwa na alama saba katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi

LIGI KUU KUENDELEA LEO.

MZUNGUKO wa tatu wa Ligi Kuu ya NBC unatarajiwa kutamatika leo kwa michezo miwili kupigwa kwenye viwanja viwili tofauti vya mkoa wa Dar es Salaam.

Saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Uhuru, Dar timu ya Simba iliyoshinda michezo yote miwili mpaka sasa itakuwa mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga ambayo bado haijapata ushindi katika mchezo wowote wa ligi msimu huu.

Timu ya Azam itakua mwenyeji wa Singida BS saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar ikiwa ni mchezo wa mwisho kuchezwa kwenye mzunguko wa tatu.

Azam inacheza na Singida huku ikiwa na rekodi ya kushinda michezo yote kwenye uwanja wa nyumbani huku Singida ikiwa haijapata ushindi wala kufunga bao kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

TMA, KEN GOLD, COPCO ZAPETA NBC CHAMPIONSHIP

TIMU za TMA ya Arusha, Ken Gold ya Mbeya na Copco FC ya Mwanza zimefanikiwa kushinda michezo yao kwenye Ligi ya NBC Championship kwa mara ya kwanza msimu huu.

TMA ilicheza mapema saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na kushinda 1-0 dhidi ya Biashara ya Mara.

Ushindi huo umeifanya TMA kufikisha alama nne na kukaa nafasi ya nne ikiwa haijafungwa mchezo wowote mpaka sasa huku ikiwa mojawapo ya timu tatu zilizopanda daraja kutoka First League.

Ken Gold imeifunga Green Warriors ya Dar kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya na kufikisha alama nne zinazowaweka nafasi ya tatu huku wakiwa hawajapoteza mchezo mpaka mzunguko wa pili.

Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Copco imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Cosmopolitan ya Dar I’m na kusogea mpaka nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship.

Cosmopolitan imeshindwa kupata alama yoyote mpaka mzunguko wa pili ikipoteza michezo yote miwili na kuruhusu jumla ya mabao saba.

Ligi ya NBC Championship itaendelea tena kesho Septemba 17, kwa michezo mitatu huku kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mbuni itacheza na Stand United saa 8:00 mchana, FGA Talents dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Mbeya City dhidi ya Transit Camp kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya huku michezo hiyo miwili ikianza saa 10:00 alasiri .

KMC YAANZA VYEMA NYUMBANI

TIMU ya KMC ya Dar imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC kwa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania ikicheza katika uwanja wake wa Uhuru, Dar.

Awesu Awesu na Waziri Junior ndio waliofunga mabao mawili na kuifanya JKT Tanzania kuwa timu iliyoruhusu mabao mengi mpaka sasa kwenye Ligi kuu ya NBC (7) sawa na KMC huku bao la JKT likifungwa na Edward Songo.

Ushindi huo umeipeleka KMC mpaka nafasi ya nane ikifikisha alama nne huku JKT ikisalia nafasi ya 10 nyuma ya Ihefu ya Mbeya.