Author: Honest Mwanitega

WARATIBU ‘WANOLEWA’ DAR.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo Septemba 9, imeendesha semina ya waratibu wa michezo iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Benjamin Mkapa Dar es saalam.

Semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwaongezea ufanisi katika kusimamia michezo mbalimbali ya kimashindano iliyo chini ya TFF na TPLB.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Almasi Kasongo amesema lengo la semina hiyo ni kuongeza ufanisi na uwezo wa waratibu katika usimamizi wa michezo inayoendeshwa chini ya TFF na Bodi ya ligi.

Kasongo amewataka waratibu wa michezo kuwa mabalozi Wazuri wa Bodi ya Ligi na TFF katika usimamizi wa michezo.

“Ligi yetu ni ya 5 kwa ubora na hili limefanikiwa kwa mchango wenu katika kusimamia michezo hii vizuri hivyo niwaombe muendelee kuwa bora zaidi kupitia mafunzo haya” alisema Kasongo.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni pamoja na udhamini wa ligi na mipangilio (League sponsorship and branding), taratibu za mchezo (Match Coordination), taratibu za habari siku ya mchezo (Match day media operations) na Kanuni (Regulations).

Semina hiyo imehudhuriwa na waratibu Zaidi ya 30 kutoka mikoa zaidi ya 22 Tanzania Pamoja na watumishi wa Bodi ya Ligi na TFF.

NBC CHAMPIONSHIP KUANZA RASMI LEO

PAZIA la Ligi ya NBC Championship msimu wa 2023/2024 linafunguliwa rasmi leo Septemba 9 kwa michezo mitatu kuchezwa katika viwanja mbalimbali.

Mchezo wa kwanza wa ufunguzi utazikutanisha Mbeya City dhidi ya Green Warriors saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Sokoine, Mbeya mchezo wa pili utazikutanisha Mbeya Kwanza dhidi Polisi Tanzania saa 10:00 alasiri katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mkoani Mtwara na mchezo wa mwisho ni kati ya Copco na Pan Africans saa 10:00 alasiri uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hii ni kwa mara ya kwanza Ligi ya Championship kupata udhamini ambapo Benki ya Taifa ya Biashara, NBC imeandika historia ya kuwa mdhamini wa kwanza na kuifanya Ligi hiyo sasa kutambulika kama Ligi ya NBC Championship.

YANGA YAIPIGISHA ‘KWATA’ JKT.

TIMU ya Yanga imeshinda mchezo wa pili mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kufunga mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Mabao ya Stephane Ki Aziz, Kenedy Musonda, Kouasi Yao, na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili yametosha kuiweka Yanga nafasi ya kwanza msimu huu ikiwa bingwa mtetezi kwa kufikisha alama sita.

Mpaka sasa timu ya Yanga ndio kinara wa kufunga mabao (10) huku ikiwa haijafungwa bao lolote sawa na timu za Mashujaa, Geita Gold na Singida Big Stars.

Yanga imeendeleza ubabe kwa JKT kwa kushinda michezo sita kwenye michezo saba iliyopita wakitoka sare mchezo mmoja .

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Agosti 31, kwa mchezo mmoja wa kukamilisha mzunguko wa pili kati ya Singida Big Stars na Tabora United kwenye uwanja wa Liti, Singida.

MABINGWA WAWILI ‘KUKIWASHA’ LEO AZAM COMPLEX.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Agosti 29 kwa mchezo mmoja kati ya Yanga na JKT Tanzania kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Mchezo huu unaikutanisha Yanga iliyokuwa bingwa wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita na JKT iliyokuwa bingwa wa Ligi ya Championship msimu uliopita.

Timu hizo zinacheza mchezo wa pili wa ligi msimu huu kila moja ikiwa haijafungwa bao lolote na zote zikifanikiwa kushinda michezo yao ya ufunguzi.

Yanga ndiye kinara wa ushindi anapokutana na JKT akishinda michezo mitano kati ya sita waliyokutana huku wakitoka sare katika mchezo mmoja.

AZAM FC YAKAA KILELENI NBCPL.

TIMU ya Azam imepanda mpaka nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Prisons ya Mbeya kwa mabao 3-1.

Mabao ya Prince Dube, Iddy Selemani na Nathaniel Chilambo yameifanya Azam kushika nafasi ya kwanza na kuwa timu kinara wa kufunga mabao (7).

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Agosti 29 kwa mchezo mmoja kati ya Yanga na JKT Tanzania utakaochezwa uwanja wa Azam Complex, Dar saa 1:00 usiku huku timu zote zikifanikiwa kushinda michezo yake ya kwanza msimu huu.