Author: Honest Mwanitega

KMC YAPATA USHINDI WA JIONI

TIMU ya KMC imefungua pazia la Ligi Kuu NBC duru ya pili kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Coastal Union ya mkoani Tanga kwa bao la George Makan’ga dakika 85.

Huu ni ushindi wa kwanza kwa KMC katika michezo nane mfululizo iliyopita unaowafanya kukusanya pointi 19 na kusogea mpaka nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu.

Coastal Union imepata ushindi katika mechi mbili pekee kati ya 10 zilizopita huku ikishindwa kuzuia bao katika michezo nane mfululizo .

Coastal inakua timu ya pili iliyopoteza michezo mingi katika Ligi (9) huku timu za Ihefu, Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zikipoteza mechi kumi kila moja.

Matokeo hayo yanaifanya Coastal kufikisha mechi saba za ugenini huku wakipata ushindi katika mechi moja pekee na kusalia nafasi ya 12 katika msimamo wakifikisha pointi 15.

Ligi Kuu NBC itaendelea tena desemba 16 kwa michezo mitatu Mtibwa Sugar itakua wenyeji wa Namungo saa 10:00 alasiri uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, Kagera Sugar dhidi ya Azam katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera saa 1:00 usiku huku Ruvu Shooting itakua mwenyeji wa Ihefu katika uwanja wa Azam Complex saa 3:00 usiku.

AZAM YAWEKA REKODI MPYA

TIMU ya Azam imekua ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu NBC kupata matokeo ya ushindi katika mechi nane mfululizo baada ya kuifunga  Polisi Tanzania bao 1-0 ugenini.

Likiwa bao la kwanza kufunga msimu huu kwa Ayoub Lyanga dakika ya 15 limetosha kuifanya timu ya Azam kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi katika nafasi ya pili kwa kushinda mechi 11 kutoa sare mbili na kupoteza mbili.

Ushindi huo umeendelea kuididimiza timu ya Polisi mkiani katika msimamo wa Ligi ikisalia na pointi tisa katika nafasi ya 16 baada ya kukamilisha michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa Kocha wa zamani wa timu ya Yanga Mwinyi Zahera kuongoza timu ya Polisi huku mchezo wake wa pili akitarajiwa kukutana na timu yake ya zamani Disemba 17 katika uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam.

Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu NBC unatarajiwa kumalizika Disemba 7 kwa michezo miwili, mapema saa 8:00 mchana timu ya Singida Big Stars itakuwa mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga kwenye uwanja wa Liti, Singida huku uwanja wa Majaliwa, Lindi Namungo itaikaribisha Yanga majira ya saa 1:00 usiku.

 

POLISI TANZANIA KUTOKA MKIANI LEO ?

TIMU ya Polisi Tanzania ikiwa imeshinda michezo michache (2) kuliko timu yoyote katika Ligi Kuu NBC msimu huu leo inawakaribisha Azam FC katika uwanja wa Ushirika, mkoani Kilimanjaro saa 10:00 alasiri.

Polisi imeshinda mchezo mmoja katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Namungo ya mkoani Lindi kwa bao 1-0 na mchezo mmoja ugenini dhidi ya Ihefu ya Mbarali, Mbeya kwa mabao 2-1.

Mchezo wa mwisho kucheza katika uwanja wa nyumbani Polisi ilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Simba na endapo timu hiyo itashinda katika mchezo wa leo itajinasua kutoka nafasi ya mwisho katika msimamo na kupanda kwa nafasi mbili.

Wapinzani wa Polisi katika mchezo wa leo timu ya Azam imepata ushindi katika michezo saba mfululizo chini ya kaimu kocha mkuu Kali Ongala na kukusanya pointi 32 wakishika nafasi ya tatu.

Azam ikipata ushindi katika mchezo huo itakusanya jumla ya pointi 35 sawa na kinara wa msimamo wa Ligi Yanga wakizidiwa kwa mabao tisa huku vinara hao wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

SIMBA YAPANDA KILELENI, PHIRI, MAYELE WAENDELEZA VITA

TIMU ya Simba imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu NBC kwa kicheko baada ya kuichapa Coastal Union mabao 3-0 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa ushindi huo wa ugenini Simba imefikisha pointi 34 na kuwa vinara wakiwazidi mahasimu wao Yanga kwa pointi mbili na michezo miwili.

Mabao ya Moses Phiri dakika ya 53 na 61 na moja la Clatous Chama dakika ya 89 yameibakisha timu ya Coastal Union nafasi ya 13 ikiwa na point 12 baada ya michezo 14.

Mabao mawili ya Moses Phiri yamemfanya kufikisha mabao 10 sawa na Fiston Mayele wa Yanga na kuungana kuwa vinara wa mabao.

Pasi ya Clatous Chama iliyozaa bao la kwanza la Moses Phiri inamfanya kufikisha pasi saba na kuwa kinara wa pasi zilizozaa mabao.

Mchezo wa mapema Ruvu Shooting imeendelea kusota kwa kushindwa kupata matokeo katika michezo saba mfululizo baada ya kufungwa na timu ya Dodoma Jiji mabao 2-1.

Mabao ya Hassan Mwaterema na Salum Kipaga aliyejifunga yameisogeza Dodoma mpaka nafasi ya 12 kwa kufikisha pointi 15 huku bao pekee la Ruvu lililofungwa na Ally Bilali likiibakiza Ruvu nafasi ya 15 na alama 11 baada ya michezo 15.

TAARIFA KUTOKA BODI YA LIGI TANZANIA

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Disemba 1, 2022 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

 

Ligi Kuu ya NBC (NBCPL)

Mechi Namba 37: Mbeya City FC 1-1 Simba SC

Timu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la baadhi ya wachezaji wake kuingia uwanjani kwa kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo tajwa hapo juu uliofanyika kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya Novemba 23, 2022.

Simba walilazimisha baadhi ya wachezaji wao waruhusiwe kuingia uwanjani kupitia mlango wa kuingilia jukwaa la watu maalum na walipozuiwa na walinzi wa uwanjani (stewards), Simba walitumia nguvu kutimiza nia yao.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:(21 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mchezaji wa timu ya Simba, Gadiel Michael amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kulazimisha kuingia uwanjani saa 4:25 asubuhi ya siku ya mchezo tajwa hapo juu kwa kile alichoeleza alitaka kukagua kiwanja.

Licha ya walinzi wa uwanja huo kumzuia Gadiel (ambaye alikuwa ameongozana na watu kadhaa waliovalia fulana zenye nembo ya klabu ya Simba), kwasababu haukuwa muda rasmi kwa ajili ya zoezi hilo na Simba hawakufanya mawasiliano yoyote na Kamishna wala Mratibu wa Mchezo wakieleza jambo hilo, Gadiel alitumia hila na kufanikiwa kuwakwepa walinzi hao kisha kuingia kiwanjani.

Mchezaji huyo alipoingia kiwanjani hakuonesha dalili yoyote ya kukagua eneo la kuchezea na badala yake alionekana kwenda moja kwa moja hadi eneo la katikati ya kiwanja na kumwaga vitu vyenye asili ya unga.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni 41:5(5.5) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Wachezaji.

 

Kamati imeikumbusha Timu ya Mbeya City kuhakikisha viongozi wake waliofungiwa wanatekeleza adhabu zao kikamilifu ikiwemo kutojihusisha na masuala ya timu hiyo hadi pale adhabu zao zitakapomalizika.

Katika mchezo tajwa hapo juu, kiongozi wa Mbeya City, Frank Mfundo ambaye anatumikia adhabu ya kufungiwa, alionekana kufanya kazi za klabu hadi pale walipomuondoa kwa haraka baada ya kuelezwa juu ya jambo.

Klabu ina wajibu wa kuhakikisha viongozi na wachezaji wao walioadhibiwa wanatekeleza masharti ya adhabu zao kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 47:5 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Timu ya Mbeya City imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la baadhi ya viongozi wake kumtolea lugha chafu Mratibu Msaidizi wa Mchezo tajwa hapo, wakilazimisha kuingia katika eneo la kimashindano mara baada ya mchezo kumalizika na wakati makochwa wa timu zote mbili wakiendelea kuhojiwa na Azam TV.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:(21 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mchezo tajwa hapo juu ulikuwa na mapungufu katika uamuzi hivyo Kamati imepeleka shauri la waamuzi wa mchezo huo kwenye Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu, TFF kwa ajili kujadiliwa na kutolewa ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanyika kwa maamuzi.

 

Mechi Namba 38: Ihefu SC 2-1 Young African SC

Kocha wa timu ya Young African, Nasreddine Nabi amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuwashambulia kwa maneno mwamuzi wa kati na mwamuzi wa akiba wa mchezo tajwa hapo juu.

Kocha Nabi aliendelea kufanya kitendo hicho hata baada ya kuonywa kwa kadi ya manjano.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 42:2(2.1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

 

Mechi Namba 106: Ruvu Shooting FC 0-1 Singida Big Stars FC

Klabu ya Ruvu Shooting imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani kuelekea mchezo tajwa hapo juu.

Ruvu Shooting waliwasili uwanjani saa 8:42 mchana badala ya saa 8:30 mchana kama ilivyoainishwa kwenye kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:60 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi Namba 109: Polisi Tanzania FC 1-3 Simba SC

Klabu ya Polisi Tanzania imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo tajwa hapo juu uliofanyika kwenye uwanja wa Ushirika uliopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Novemba 27, 2022.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:(21 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi Namba 110: Azam FC 3-2 Coastal Union FC

Mchezaji wa klabu ya Coastal Union, Maabadi Maabadi amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kumshambulia mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu kwa kumrushia chupa ya maji na baadaye kiatu.

Mchezaji huyo ambaye alikuwa kwenye benchi baada ya kufanyiwa mabadiliko, alionekana akiingia kiwanjani na kumrushia chupa mwamuzi wa kati wakati mchezo ukiendelea kisha kwenda kumshambulia mwamuzi huyo kwa kutumia kiatu baada ya mchezo kumalizika.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 41:5(5.3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

 

Klabu ya Coastal Union imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la baadhi ya wachezaji wake na viongozi wa benchi la ufundi kurusha chupa za maji kiwanjani wakati mchezo ukiendelea.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Klabu ya Azam imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la shabiki wake aliyekuwa ameketi kwenye jukwaa la watu maalum, kurusha chupa ya maji kwa hasira katika eneo hilo mara baada ya timu ya Coastal Union kupata bao la kusawazisha katika mchezo tajwa hapo juu uliomalizika kwa Azam kupata ushindi wa mabao 3-2.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Kamati imepeleka shauri la waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kwenye Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu, TFF kwa ajili kujadiliwa na kutolewa ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanyika kwa maamuzi.

 

Ligi ya Championship

Mechi Namba 86: Pan Africans FC 2-0 Biashara United FC

Klabu ya Pan Africans imepewa onyo kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Pan Africans iliwakilishwa na maafisa wanne (4) badala ya watano (5) walioainishwa kikanuni.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:2(2.2) na 17:60 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Imetolewa na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

Disemba 2, 2022