Author: Honest Mwanitega

SIMBA YANGURUMA DAR,GEITA YATAKATA MBEYA

TIMU ya Simba imefanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC likifungwa na Moses Phiri dakika ya 32 kipindi cha kwanza baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Mohammed Hussein ‘Zimbwe Junior’.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 24 na kukalia nafasi ya pili nyuma ya vinara Azam FC wenye alama 26 huku Namungo ikisalia nafasi ya saba na pointi 15.

Bao lililofungwa na Moses Phiri Linamfanya afikishe Mabao sita akizidiwa bao moja na kinara Sixtus Sabilo anaekipiga timu ya Mbeya City mwenye mabao saba.

Mkoani Morogoro majira ya saa nane mchana timu ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kubaki na alama zote tatu nyumbani baada ya kuifunga Coastal Union ya Tanga mabao 2-1 mchezo uliopigwa uwanja wa Manungu.

Mabao ya Mtibwa yamefungwa na Adam Adam dakika ya pili na Juma Nyangi dakika ya 32 huku bao la Coastal likifungwa na Mubarack Amza dakika ya 13.

Matokeo hayo yanaifanya timu ya Mtibwa kufikisha pointi 18 na kupanda nafasi ya tano huku Coastal wakisalia na pointi 12 na kukamata nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu NBC.

Nayo timu ya Geita Gold imefanikiwa kupata karamu ya mabao mkoani Mbeya baada ya kuwafunga maafande wa Prisons mabao 4-2 mchezo uliopigwa uwanja wa kumbukumbu Sokoine.

Mabao ya Geita yamefungwa na Yusuph Kagoma, Danny Lyanga, Shown Oduro na Edmund John huku mabao ya Prisons yakifungwa na Oscar Paul pamoja na bao la kujifunga kwa Shawn Oduro.

Matokeo hayo yanaifanya Geita kukusanya pointi 17 na kukamata nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi huku Prisons ikisalia na pointi 14 na kukamata nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu NBC.

Ligi hiyo itaendelea Leo kwa michezo mitatu katika mikoa miwili tofauti,Mkoani Mbeya Ihefu SC itaikaribisha Polisi Tanzania uwanja wa Highland Estate majira ya saa nane mchana huku majira ya saa 10 alasiri Mbeya City itaikaribisha Kagera Sugar uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine na mchezo wa saa moja usiku utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa timu ya Yanga itaikaribisha Singida Big Stars mchezo wa mwisho kukamilisha mzunguko wa 12 .

AZAM YAKWEA KILELENI,DODOMA JIJI YAZINDUKA

TIMU ya Azam FC imefanikiwa kupanda kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kupata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting kwa bao 1-0.

Bao la Azam limefungwa na Idriss Mbombo dakika ya 72 kwa mkwaju wa penati baada ya Ayoub Lyanga kufanyiwa faulo ndani ya eneo la Penati.

Huu unakua ushindi wa tano mfululizo kwa Azam takribani mwezi mmoja baada ya kumtangaza Kali Ongala kama kaimu kocha mkuu.

Kwa matokeo hayo Azam inafikisha alama 26 na kushika usukani wa Ligi kwa alama tatu zaidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili katika msimamo.

Nayo timu ya Dodoma jiji mapema alasiri ilipata ushindi wa bao 2-1 dhidi ya KMC ya Dar es Salaam mchezo uliochezwa uwanja wa Uhuru mkoani hapa.

Dodoma ilifanikiwa kumaliza mchezo mapema ndani ya dakika 20 za kwanza kwa kufunga mabao mawili kupitia kwa Seif Karihe dakika ya nane na 18.

Kwa Matokeo hayo Dodoma inafikisha alama tisa na kushika nafasi ya 14 huku mchezo unaofuata wakiwa nyumbani Novemba 22 katika uwanja wa Liti Singida kuwaalika Yanga.

AZAM KUISHUSHA YANGA KILELENI LEO?

 

MZUNGUKO wa 12 wa Ligi Kuu NBC unatarajia kuanza leo Novemba 15,kwa michezo miwili itakayopigwa mkoani Dar es Salaam katika viwanja vya Uhuru na Azam Complex.

Mchezo wa saa 10 alasiri utakaochezwa uwanja wa Uhuru KMC watakua wenyeji wa Dodoma Jiji iliyopoteza mchezo dhidi ya Azam huku kwenye uwanja wa Azam Complex timu ya Azam itaikaribisha Ruvu Shooting ya mkoani Pwani.

Azam inaelekea katika mchezo wake ikiwa katika fomu nzuri ya kupata alama tatu kwenye kila mchezo chini ya Kaimu kocha mkuu Kali Ongala baada ya kushinda katika michezo minne mfululizo dhidi ya Simba,Ihefu,Dodoma Jiji na Mtibwa na kufikisha alama 23 sawa na vinara wa msimamo Yanga.

“Jambo muhimu kwetu kwa sasa ni kupata alama tatu muhimu katika kila mchezo kwani kila mechi ya ligi kuu ni mgumu kutokana na kila timu kuwa na maandalizi ya kushindana”alisema Kali.

Naye kocha msaidizi wa Ruvu Shooting Rajab Mohammed amesema kuwa timu yake imejiandaa vizuri na wamefanyia marekebisho makosa yote yaliyojitokeza michezo ya nyuma hivyo wanaamini wataenda kupata matokeo chanya dhidi katika mchezo wa leo.

“Azam ni timu bora iliyokamilika kila idara,tumeawaona ubora na madhaifu yao na tumewaelekeza vijana namna ya kucheza dhidi yao hivyo tunaamini tutapata matokeo chanya katika mchezo wetu dhidi yao.”alisema Rajab.

HOTUBA YA MWENYEKITI – BODI YA LIGI KUU TANZANIA MKUTANO WA TISA WA BARAZA KUU LA BODI YA LIGI KUU TANZANIA

 

Ndugu Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo;

Ndugu Ally Mayay, Mkurugenzi wa Michezo;

Wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania;

Wenyeviti Klabu za Ligi Kuu;

Wenyeviti Klabu za Championship;

Wenyeviti Klabu Za First League;

Ndugu Wilfred Kidao, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania

Ndugu Almasi Jumapili Kasongo, Afisa Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi Kuu Tanzania,

Wenyeviti wa Vyama Vishiriki (FRAT, TAFCA, TASMA, SPUTANZA na TWFA);

Mwakilishi wa Kamati ya Maadili ya TFF (Amin Bakhressa)

Wakurugenzi wote wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania;

Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji;

Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu Tanzania, NBC Bank Limited;

Wadhamini wenye haki za Matangazo ya Runinga, Azam Media Limited;

Wadhamini wenye haki za Matangazo ya Radio, Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC);

Sekretariati ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania;

Ndugu Wenyeviti na Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mabibi na Mabwana,

Ni matumaini yangu kuwa muwazima wa afya na mnaendelea vizuri na shughuli za kila siku za maendeleo na ukuaji wa mpira wa miguu katika nchi yetu.

Rambirambi za kina ziwafikie Marafiki na Familia za Wanamichezo wote waliopoteza wapendwa wao katika kipindi cha ndani ya mwaka mmoja nchini Tanzania na Duniani kwa ujumla wake.

Lakini pia nawaomba tusimame kwa dakika moja kuwaombea wenzetu waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision iliyotokea mkoani Kagera Novemba 6, 2022.

Bodi imeendelea kufanya vizuri tangu tulipokutana kwa mara ya mwisho kwenye Mkutano Mkuu wa kawaida na Uchaguzi uliofanyika Cate Hotels, Morogoro na kuendelea kuweka msingi imara wa ushindani kwa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla wake, lengo kuu likiwa ni kuona kwa namna gani klabu zetu zinaweza kuwa bora na zinaingia kwenye orodha ya klabu 10 bora barani Afrika.

Sisi sote ni mashuhuda kwa mara nyingine tena ligi yetu imeweza kuwa miongoni mwa ligi kumi (10) bora barani Afrika na ligi ya 62 Duniani. Lakini pia tumeweza kutoa uwakilishi wa klabu nne kwenye mashindano ya Klabu Bingwa na Shirikisho Afrika.

Bodi imeendelea na dhamira ya kuhakikisha kwamba michezo yetu yote ya Ligi inachezwa katika viwanja vinavyokidhi matakwa ya KIKANUNI na SHERIA namba moja (UWANJA) katika sheria 17 za mpira wa miguu lakini vinavyokidhi viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika na Duniani (FIFA).

Msingi wake mkubwa ukiwa ni upatikanaji wa HAKI na mechi kuchezwa kwenye viwanja vilivyo salama kwa mazingatio ya ulinzi wa wachezaji na watazamaji kwa ujumla wake kama ambavyo CAF na FIFA wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na viwanja bora na salama kwa nyakati zote.

Lakini pia napenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole sana Wenyeviti wenzangu pamoja nami binafsi kwa viwanja vyetu kufungiwa kutumika kwa michezo ya ligi mpaka pale maboresho yatakapofanyika ili kukidhi matakwa ya Kanuni na Sheria za mpira wa miguu. Kwa taarifa niliyonayo viwanja vingi vilivyokuwa vimefungiwa sasa vimefunguliwa na vinaendelea na matumizi yake kama kawaida isipokuwa viwanja vya Jamhuri (Dodoma) na Mabatini (Pwani) vinavyotumiwa na Dodoma Jiji na Ruvu Shooting kwa mfuatano.

Bodi kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tumeendelea kuimarisha eneo la UAMUZI na WAAMUZI kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali kupitia wakufunzi wa ndani na nje ya nchi ambao wanatambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Duniani (FIFA).

Mijadala na mipango mbalimbali ya namna gani ya kuimarisha eneo la UAMUZI na WAAMUZI imeendelea na lengo ni kuona UHURU, UADILIFU, HESHIMA na UAMINIFU kwa UAMUZI na WAAMUZI yanakuwa kipaumbele cha kwanza kwa MWAMUZI na bila kumsahau KAMISAA kwa wakati wote.

Pamoja na   juhudi zote hizo, tunakiri kuwa eneo la uamuzi limeendelea kuwa na changamoto katika kutafsiri sheria 17 za mpira wa miguu. Lakini pamoja na juhudi kubwa tunazofanya kuhusiana na kuondoa changamoto tulizokuwa nazo ndugu Wenyeviti wenzangu na wajumbe wa Mkutano Mkuu ni ukweli usiopingika kwamba matumizi ya Teknolojia (VAR, Goal line technology na Communication tools) yamekuwa ni kitu cha MUHIMU na LAZIMA katika kuwasaidia waamuzi wanapokuwa kwenye majukumu yao ya kutafsiri Sheria 17 za mpira wa miguu.

Bodi inaamini kuwa huu ni wakati sahihi wa kuanza kutumia TEKNOLOJIA tajwa hapo juu.

Bodi kwa kushirikiana na TFF tumejielekeza kwenye utekelezaji wa masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations) kwa asilimia 100 kama tulivyokubaliana na kuazimia kwenye Mkutano Mkuu wa Klabu uliofanyika Desemba 15, 2020 tukiamini kuwa utekelezaji wa Kanuni tajwa hapo juu ndiyo dawa pekee ya kuondoa changamoto nyingi tulizokuwa nazo kwenye mpira wa miguu.

Utekelezaji wa Kanuni ya Leseni ya Klabu ni moja ya vipaumbele vyangu vikuu katika kuhakikisha ligi zetu na mpira wa miguu kwa ujumla wake unapiga hatua. Hivyo basi ni matarajio yangu kuwa utekelezaji wa Kanuni ya Leseni za Klabu tutausimamia na kuuchukulia kwa uzito mkubwa ili uweze kuja kutusaidia kuondoa changamoto nyingi tulizokuwa nazo katika usimamizi na uendeshaji wa ligi.

Mafanikio na ukuaji wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea mafanikio na ukuaji wa klabu zetu hivyo basi ili tuweze kufikia mafanikio hayo Bodi, Klabu, Vyama vishiriki vya mpira wa miguu (FRAT, TAFCA, TASMA, SPUTANZA na TWFA), vyama vya mpira wa miguu vya mikoa/wilaya hatuna budi kuajiri wafanyakazi wenye uzoefu na sifa katika nafasi wanazozifanyia kazi ili tuweze kuleta tija katika taasisi zetu.

Bodi itaendelea kusimamia na kuboresha mahusiano na wadau wake wote klabu, vyama vishiriki, vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa/Wilaya, Wadhamini, Wamiliki wa Viwanja, Kampuni/Mashirika, Vyombo vya habari, Waandishi, Mashabiki bila kusahau mdau mkubwa na namba moja, Serikali.

Kupungua kwa idadi ya watu wanaoingia viwanjani kutazama mechi za ligi zetu hasa Ligi Kuu ni eneo jingine muhimu ambalo Bodi tumeanza kulifanyia kazi kwa umakini mkubwa ili tuweze kupata njia mbadala ya kurejesha watu viwanjani kama ilivyokuwa katika siku za nyuma.

Hivyo basi nawaomba Wenyeviti wote tujifikirishe namna ya kutafuta njia bora ya kufanya ili tuweze kuleta watu viwanjani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika Mikoa yetu. Rejea taarifa ya mapato na mashabiki walioingia uwanjani kwa kila timu msimu 2021/2022.

Rasilimali fedha kimeendelea kuwa kipaumbele cha kwanza katika kutimiza majukumu ya Bodi na Klabu zetu. Ni matarajio yangu kuwa kuimarika kwa eneo la rasilimali fedha ni kuimarika kwa usimamizi, uendeshaji na utekelezaji wa majukumu ya Bodi na klabu kwa ujumla. Hivyo basi katika kipindi changu cha uongozi nitaendelea kuhakikisha Ligi zetu zote zinakuwa na wafadhili wengi iwezekanavyo ili kuweza kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea.

Lakini naomba nichukue nafasi hii kuwaomba Wenyeviti wenzangu tuweze kuajiri watu wa masoko wazoefu na wenye sifa katika Klabu zetu ili tuweze kuondokana na changamoto ya Rasilimali Fedha.

Napenda kuwaasa Wenyeviti wenzangu kuweza kusimamia na kutekeleza Kanuni za Ligi zetu zote tatu kama zilivyopitishwa. Kumekuwa na changamoto kubwa kwa Klabu kutozingatia na kuheshimu Kanuni za Ligi jambo linalosababisha uwepo wa matukio mengi yasiyo ya kimichezo na yanayochafua taswira ya Ligi zetu lakini matukio hayo yamekuwa yakisababisha Klabu ziadhibiwe mara kwa mara kwa kutozwa faini ama viongozi/wachezaji kufungiwa kwa mujibu wa Kanuni.

Ni matarajio yangu baada ya Mkutano huu Wenyeviti tutarudi kwenye klabu zetu na kuona namna gani tunaweza kuelimishana na kusimamia kanuni tulizojiwekea.

Nina hakika kwamba msingi imara na maendeleo mazuri tuliyopata tangu tukutane kwa mara ya mwisho katika Mkutano Mkuu uliofanyika Cate Hotels, Morogoro, muda si mrefu ligi zetu na mpira nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla zitakuwa na ushindani zaidi na kuvutia kwa Mashabiki, Wafadhili na Wadau wengine wa Mpira wa Miguu Duniani kote.

Mwisho tunatambua nguvu ya kipekee ya mpira wa miguu katika Kuwaunganisha watu wa jinsia zote, rika zote, kabila, dini na tamaduni mbalimbali katika nchi yetu. Hivyo basi tutambue tuna jukumu la kuendelea kuwaunganisha watanzania na Afrika kwa ujumla kupitia malengo yetu makuu ya kuhakikisha ligi zetu zote tatu tunazisimamia kwa uweledi na ufanisi mkubwa.

Pamoja Tunaweza.

Ahsanteni Sana.

Steven J. Mnguto

MWENYEKITI – TPLB

SINGIDA,SIMBA ZATOSHANA NGUVU,AZAM YAPETA

TIMU za Singida Big Stars ya mkoani Singida na Simba SC ya Dar es Salaam zimeshindwa kutambiana kwenye uwanja wa CCM Liti baada ya kutoka sare ya bao moja.

Katikati ya watazamaji Zaidi ya elfu 11 waliofurika uwanjani kutazama mchezo huo wa Ligi Kuu NBC, Singida ilikuwa ya kwanza kupata bao lililowapeleka mapumziko kifua mbele kupitia kwa Deus Kaseke dakika ya 11, akiunganisha krosi ya mchezaji wa zamani wa Simba, Said Ndemla.

Simba walipata bao lao la kusawazisha dakika ya 58 kupitia kwa Peter Banda aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Jonas Mkude.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha alama 18 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo sawa na Singida waliopo nafasi ya tatu wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam FC imepata ushindi wa tatu mfululizo katika Ligi Kuu NBC baada ya kuifunga timu ya Dodoma Jiji mabao 2-1 kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mabao ya Azam katika mchezo huo yamefungwa na Ismael Aziz Kader dakika ya 37 na Idris Mbombo dakika ya 89 huku bao pekee la Dodoma likifungwa na Collins Opare dakika 41.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kufikisha alama 20 sawa na vinara wa Ligi Yanga wakitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa huku Dodoma ikisalia na alama sita katika nafasi ya 14 ya msimamo wa ligi ya NBC.

Ligi Kuu NBC itaendelea tena Novemba 10 katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya kwa mchezo kati ya Tanzania Prisons na Coastal Union ya Tanga.