Author: Loveness Bernard

HAUSUNG RASMI LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC

TIMU ya Hausung kutoka Makambako mkoani Njombe imekuwa timu ya kwanza kupanda daraja kwenda Ligi ya Championship ya NBC kutoka kundi A la First League.

Hausung wenye alama 25 huku wakiwa wanaongoza kundi A wamefanikiwa kupanda daraja baada ya kucheza  michezo 13 kati ya 14 ambayo wanapaswa kucheza.

Mbali na alama hizo Hausung wamefanikiwa kufunga mabao 19 huku wakiruhusu mabao 11 katika michezo 13 huku wakiwa wameshida michezo saba wakitoka sare michezo minne na kufungwa mechi nne.

Nyumbu wapo nafasi ya pili katika msimamo huo wakiwa na alama 21 baaba ya kucheza michezo 13 wakishinda michezo sita,wakipata sare tatu na kufungwa michezo minne  huku ukibaki mchezo mmoja ligi hiyo ambao hata kama wakishinda hawataweza kufikia alama ambazo timu ya Hausung  imeweza kuzikusanya.

 

WAKALI WA MGUU WA KUSHOTO LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC inazidi kushika kasi ikiwa ni takribani michezo 183 imeshachezwa huku mabao 406 yakiwa yamefungwa ikiwemo yaliyofungwa kwa mguu wa kushoto na wakali wafuatao.

Ki Azizi ni kiungo mshambuliaji wa Young African katika msimu huu wa 2024/2025 ameshatia wavuni mabao sita kwa mguu wake wa kushoto kati ya mabao saba aliyofunga mpaka sasa.

Winga wa  timu ya Azam, Gibril Sillah, ameshatia wavuni mabao matano  kwa mguu wake wa kushoto kati ya saba ambayo ameshafunga mpaka sasa.

Offen Chikola wa Tabora United ameshatikisa nyavu mara tano kwa mguu wa kushoto kati ya mabao saba aliyofunga msimu huu.

Nassor Saaduni ni mshambuliaji wa Azam akiwa amefanikiwa kuingia langoni mwa wapinzani wao mara tano akitumia mguu wake wa kushoto.

Mchezaji Selemani Bwenzi aliyeingia dirisha dogo kwa timu ya KenGold mkali huyo mpaka sasa amefanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani akitumia mguu wake wa kushoto.

Naye mchezaji wa Namungo Joshua Ibrahimu kafanikiwa kuweka mpira wavuni mara nne akitumia mguu wake wa kushoto.

‘TSHABALALA’ MKALI WA PASI ZA MWISHO LIGI KUU NBC.

BEKI wa timu ya Simba,Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye kinara wa  kutoa pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2024/2025 akiwa nazo nne.

Tshabalala alitoa pasi za mwisho na kuisaidia timu yake kupata alama katika michezo ya Simba dhidi ya timu za Fountain Gate (1),Dodoma Jiji (1),Tabora (1) na Kagera Sugar.

Nafasi ya pili inashikiliwa na beki wa Singida Black Stars, Ande Koffi akiwa ametoa pasi tatu katika mechi za Singida dhidi ya Fountain Gate (1),Pamba Jiji (1) na KenGold (1).

Datius Peter wa Kagera Sugar anafuata akiwa na pasi za mwisho tatu alizotoa katika michezo ya Kagera Sugar dhidi ya timu za Pamba Jiji (1),KenGold (1) na mchezo wa Mashujaa (1).

Beki wa Simba, Shomari Kapombe, amepiga pasi za mwisho tatu alizoweza kutoka katika michezo ya timu yake dhidi ya Prisons (2) na Fountain Gate (1).

Beki na nahodha wa Fountain Gate,Amos Kadikilo anashika nafasi ya tano akiwa na pasi za mwisho tatu alizopata katika michezo ya Fountain Gate dhidi ya Namungo (1) na Tanzania Prisons (2).

FEISAL MKALI WA ‘KUPIKA MABAO’ LIGI KUU YA NBC

KIUNGO wa Azam,Feisal Salum ameendelea kuwa kinara wa kupika mabao katika Ligi Kuu ya NBC kutokana na kuweza kutoa pasi 12 za mwisho kwa msimu wa 2024/2025 katika michezo 23 ambayo timu yake imeshacheza mpaka sasa akivunja rekodi ya msimu uliopita ambapo  Kipre Junior alimaliza na asisti 9.

Feisal ametoa pasi za mwisho katika michezo ya Azam dhidi za Namungo (1),JKT Tanzania (2),Fountain Gate (1),Coastal Union (1),Simba dhidi ya Azam (1),Azam dhidi ya KMC (1)  Tabora dhidi ya Azam (1).

Mechi zingine ambazo Feitoto ameweza kutoa pasi za mwishi ni  Dodoma Jiji dhidi ya Azam (1), Namungo dhidi ya Azam (1), KMC dhidi ya Azam (2).

Ukiachana na Feisal wachezaji Jean Ahoua wa Simba,Max Nzegeli ,Aziz Ki na Prince Dube wa Young Africans wamefanikiwa kutoa pasi za mwisho  saba kila mmoja.

AHOUA HASHIKIKI VITA YA UFUNGAJI BORA LIGI KUU NBC

HASHIKIKI  hivyo ndivyo unavyoweza  kusema kutokana na Kiungo mshambuliaji wa  timu ya Simba,Jean Ahoua, kutokana na mchezaji huyo kuwa na namba nzuri za mabao ndani ya  Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu wa 2024/2025.

Ikiwa ni msimu wake wa kwanza  ndani ya Simba akitokea nchini kwao Ivory Coast mchezaji huyo amefanikiwa kufunga mabao 12  kati ya mabao 52 ambayo timu ya Simba imefunga katika michezo 22 hadi sasa huku akifuatiwa na Clement Mzize mwenye mabao 10 sawa na Prince Dube ambao ni wachezaji Young African.

Ahoua amefunga mabao katika michezo ya Simba dhidi ya timu za Fountain Gate (1), Dodoma Jiji (1), Namungo (1), KMC (2), Kagera Sugar (1), JKT Tanzania (1), Tanzania Prisons (1), Namungo dhidi ya Simba (2) na Simba dhidi ya Dodoma Jiji (2).

Ahoua amekuwa na msimu mzuri kwenye Ligi Kuu ya NBC akishika nafasi ya tatu kwenye vinara wa pasi za mabao baada ya kutoa pasi saba hadi sasa.