Author: Loveness Bernard

GEITA, KAGERA WAREJEA LIGI KUU YA NBC.

TIMU za Geita Gold na Kagera Sugar zimerejea rasmi Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027 baada ya kufikisha alama ambazo hazitaweza kufikiwa na timu zingine katika michezo ya Ligi ya Championship ya NBC iliyosalia.

Geita Gold imefikisha alama 71 baada ya kuifunga Songea United mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa leo na kufanikiwa kurejea Ligi Kuu baada ya takribani misimu miwili wakiwa NBC Championship.

Kagera Sugar imerejea Ligi Kuu baada ya kufikisha alama 68 kwa kuifunga timu ya Ken Gold 3-0 ikiwa ni msimu mmoja tu tangu timu hiyo iliposhuka daraja .

Mbeya Kwanza inayowania kucheza Play off imeifunga Stand United 1-0 huku Bigman ikiifunga timu ya Gunners 2-0.

Barberian imekubali kichapo cha 0-1 kutoka kwa B19 huku Hausung nayo ikipokea kichapo cha 0-1 kutoka kwa Transit Camp.

TMA imaishushia kichapo cha 2-0 timu ya African Sports huku Mbuni ikiifunga 1-0 Polisi Tanzania kwenye mchezo uliokuwa mkali na wa kusisimua.

MZUNGUKO WA 28 NBC CHAMPIONSHIP KUTOA TASWIRA NZIMA LEO

MZUNGUKO wa 28 wa Ligi ya Championship ya NBC unaendelea leo katika viwanja nane nchini ambapo michezo hiyo itachezwa saa kumi alasiri huku michezo miwili ikiwa mbashara kwenye chaneli ya Ligi Kuu Tv inayopatikana Youtube na Fifa+.

Geita Gold itaikaribisha timu ya Songea United katika uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita ambapo pia timu ya Geita Gold ikishinda mchezo huo itakata tiketi ya moja kwa moja kupanda Ligi Kuu ya NBC na mchezo huo utakuwa mbashara chaneli ya Ligi Kuu TV katika mtandao wa Youtube.

Mchezo wa pili ni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Ken Gold katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera huku Bigman ikiikaribisha timu ya Gunners kwenye uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Mbeya Kwanza itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora huku Hausung ikichuana na Transit Camp katika uwanja wa Amani mkoani Njombe.

Timu ya Barberian itakuwa mwenyeji wa timu ya B19 katika uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani huku mchezo huo ukioneshwa mbashara kupitia Fifa +.

Kwa upande wa Mbuni itaikaribisha timu ya Polisi Tanzania katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha huku TMA ikichuana na African Sports katika uwanja wa Usharika mkoani Kilimanjaro.

GEITA ‘WAKALI’ WA KUTUPIA NBC CHAMPIONSHIP.

Geita Gold imeendelea kuonyesha ‘ubabe’ wake kwenye Ligi ya Championship ya NBC baada ya kutupia mabao 60 ikiwa ni idadi kubwa hadi sasa msimu wa 2025/2026.

Timu hiyo iliyopo katika mbio za kurejea Ligi Kuu ya NBC baada ya kushuka msimu wa 2023/2024 ikiwa ni takribani misimu miwili ikicheza Ligi ya Championship huku ikiongoza msimamo na alama 68.

Mbeya Kwanza nayo haiko nyuma ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi hiyo imeweza kutikisa nyavu za wapinzani wake mara 51.

Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo imeweza kufunga mabao 49 ikiwa ni timu ya tatu kwa kufunga mabao mengi zaidi ndani ya Championship.

Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro ipo nafasi ya tatu kwa timu zenye mabao mengi ambapo imefunga mabao 47 yanayoiweka katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Transit Camp haipo mbali ikiwa imetikisa nyavu za wapinzani wao mara 38 huku ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Kwa upande wa ‘wajeda’ wa Mbuni wenye maskani yake mkoani Arusha imefanikiwa kufunga mabao 36 ndani ya Ligi hiyo huku ikiwa nafasi ya sita katika msimamo.

CHIRWA HAKAMATIKI NBC CHAMPIONSHIP.

MSHAMBULIAJI wa timu ya Kagera Sugar Obrey Chirwa hakamatiki hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuwa kinara kwa kufunga mabao akiwa nayo 16 hadi sasa ndani ya Ligi ya Championship ya NBC.

Ligi hiyo imeshachezwa mizunguko 27 huku ikiwa imesalia mizunguko mitatu ili Ligi hiyo kufikia ukingoni ambapo pia mchezaji huyo ameisaidia timu yake kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwania kurejea Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 65.

Maulid Shaban wa Geita Gold hayupo mbali akiwa amefanikiwa kuifungia mabao 14 timu yake ambayo ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikikusanya alama 68.

Ramadhani Kalanje wa timu ya B19 nae ameweza kutikisa nyavu za wapinzani wao mara 13 huku timu hiyo ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo ikikusanya alama 31.

Abdereheman Mussa wa Transit Camp iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo na Emmanuel Mpuka wa Polisi Tanzania iliyopo nafasi ya tatu wameweza kufunga mabao 12 kila mmoja.

Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp kabla ya kuhamia KMC ya Ligi Kuu ya NBC, Boniface Brown wa Mbeya Kwanza na Samson Kassian wa KenGold wamefanikiwa kufunga mabao 11 kila mmoja hadi sasa kwenye ligi hiyo.

DODOMA YAISIMAMISHA YOUNG AFRICANS, COASTAL IKIILIZA MBEYA CITY.

TIMU ya Dodoma Jiji imemaliza utemi wa timu ya Young Africans wa kucheza michezo zaidi ya 40 bila kufungwa katika Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga 3-2 kwenye uwanja wa Airtel Stadium, Singida huku timu ya Mbeya City ikikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa timu ya Coastal Union.

Dakika mbili zilimtosha kiungo wa Young Africans,Allan Okello kufungua ukurasa wa mabao kwa kuitanguliza Young Africans lililodumu kwa dakika 27 kabla ya beki wa wababe hao wa Kariakoo Bakari Mwamunyeto kujifunga na kufanya ubao usome 1-1 kabla ya Okello kurejea tena nyavuni dakika ya 41 na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko ‘Wananchi’ wakiongoza 1-2.

Kipindi cha pili Dodoma Jiji walirejea kwa kasi kubwa ikiwa azma yao kubwa n kuhakikisha alama zinabaki nyumbani na dakika ya 89 Mwana Kibuta alifunga bao la pili kwa Dodoma kabla ya Waziri Junior kupeleka kilio ‘Jangwani’ kwa bao la tatu ndani ya dakika za nyongeza hivyo mchezo kuisha kwa matokeo ya 3-2.

Young Africans imesalia kileleni ikiwa na alama 54 huku Dodoma Jiji ikipanda nafasi ya saba na alama 32.

Mchezo mwingine wa mapema ulichezwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo Mbeya City iliikaribisha timu ya Coastal Union ya Tanga mchezo na kushuhudia ‘Wagosi wa kaya’ wakiondoka na alama zote tatu baada ya ushindi wa mabao 2-0.

Ilimchuka dakika 35 mshambuliaji wa Coastal Maabad Maabad kufungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati hivyo kwenda mapumziko wakiongoza na kujitengenezea nafasi nzuri kwao kujinasua kutoka nafasi za chini ya msimamo.

Kipindi cha pili dakika ya 74 Saad Mwanza aliiongezea bao la pili Coastal hivyo mchezo kumalizika wakiwa kifua mbele kwa mabao mawili na alama zote tatu.

Matokeo hayo yanaiweka Coastal nafasi ya 11 na alama 25 huku Mbeya City ikiwa nafasi ya 13 na alama 21 ikiwa ni nafasi ya timu zinazocheza mtoano wa kusalia Ligi Kuu ya NBC.