Author: Yahaya Abushehe

NBC CHAMPIONSHIP KINAWAKA LEO.

 

LIGI ya NBC ya Championship mzunguko wa Nne unaanza Leo kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa ya Mtwara, Arusha na Morogoro.

Mkoani Mtwara Mbeya Kwanza itakuwa mwenyeji wa Green Warriors kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona kuanzia saa 8:00 Mchana.

Mbuni FC ya Arusha itaialika Biashara United ya Mara kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa mwisho kwa leo utazikutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya Songea United kuanzia saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Hadi hivi sasa Mtibwa Sugar inaongoza msimamo wa Ligi ya NBC ya Championship ikiwa na alama tisa sawa na Songea United na Stand United zikitofautiana magoli ya kufunga na kufungwa.

SIMBA YATAKATA ZANZIBAR.

 

MCHEZO wa Ligi Kuu ya NBC Mzizima ‘DERBY’ umemalizika hapa Visiwani Zanzibar Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 0-2 dhidi ya Azam FC.

Mabao Leonel Ateba na Fabrice Ngoma yalitosha kuipa alama tatu Simba SC mbele ya Azam FC huku Mlinda Mlambo wa Simba SC Mousa Camara akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Mchezo.

Kwa matokeo hayo Simba inapanda mpaka nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya NBC ikifikisha alama tisa huku Azam FC ikishuka mpaka nafasi ya nne.

Historia mpya imeandikwa kwenye Ligi Kuu kwenye mchezo wa Mzizima ‘Derby’ kuwa ndiyo mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu kuchezwa visiwani Zanzibar.

AZAM, SIMBA NANI KUTAMBA ZANZIBAR LEO ?

 

MCHEZO wa Ligi Kuu ya NBC Mzizima ‘Derby’ kati ya Azam FC na Simba SC unapigwa leo Septemba 26 saa 2:30 usiku New Amaan Complex hapa Visiwani Zanzibar.

Azam FC inaingia kwenye mchezo huu ikiwa tayari imecheza michezo minne ya Ligi Kuu ya NBC ikishinda miwili na kupata sare michezo miwili, huku ikifunga mabao matano na haijaruhusu bao kwenye michezo hiyo minne.

Kwa upande wa Simba SC imecheza michezo miwili ya Ligi Kuu ya NBC na kushinda michezo yote ikiwa na mabao Saba ya Kufunga na kutoruhusu bao.

Mchezo wa mwisho kukutana kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu ulioisha Azam FC ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani Benjamin Mkapa ilikubali kichapo cha mabao 3-0, Je Azam kulipa kisasi au Simba kuendeleza ubabe ? Majibu yatapatikana baada ya dakika tisini kumalizika.

Hii ni kwa mara ya kwanza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kuja kuchezwa visiwani Zanzibar, hii ni baada ya maboresho ya kanuni ya msimu 2024/2025.

Kanuni ya 6(4) Michezo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaweza kuchezwa kwenye viwanja vilivyopo Tanzania Visiwani (Zanzibar) kwa mazingatio ya kanuni ya 9 kuhusu uwanja.

MTIBWA YAANZA NBC CHAMPIONSHIP KIBABE, MBEYA CITY IKIBANWA NYUMBANI.

 

LIGI ya NBC Championship imeanza rasmi kwa michezo miwili ya ufunguzi ikizihusisha timu za Mtibwa na Green Warriors, Mbeya City na Big Man FC.

Mtibwa imeanza Ligi ya NBC Championship kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Green Warriors mabao yote yakifungwa na Raizin Hafidh, mchezo uliochezwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa manungu, Morogoro.

Mbeya City ikiwa nyumbani ikalazimishwa sare ya mabao 2 na Big Man FC mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine saa 10:00 alasiri.

Mchezaji wa Mbeya City Malick Joseph anaingia kwenye kumbukumbu za Ligi ya NBC Championship msimu huu kuwa mchezaji aliyefunga bao la kwanza la Ligi hiyo.

FOUNTAIN GATE YAPAA, KAGERA SUGAR IKIPETA NYUMBANI.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Tabora na Kagera.

Mkoani Tabora, Tabora UTD ilikuwa mwenyeji wa Fountain Gate katika uwanja wa Ali hassan Mwinyi saa 10:00 alasiri na kushuhudia Tabora ikikubali kichapo cha mabao 1-3.

Kwa matokeo hayo Fountain Gate imefikisha alama 10 kwenye michezo mitano ambazo zinaipandisha hadi nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Singida Black Stars.

Mkoani Kagera, Kagera Sugar ikaiadhibu Kengold kwa mabao 2-0 mabao yaliyofungwa na Peter Lwasa dakika ya 1 na 65, huu ni ushindi wa kwanza msimu huu kwa Kagera Sugar.

Kengold inaendelea kusota nafasi ya mwisho katika msimamo ikiwa ndiyo timu pekee ndani ya Ligi Kuu ya NBC msimu huu ambayo haijapata alama yoyote.