Author: Yahaya Abushehe

TABORA UTD, FOUNTAIN GATE ZATAKATA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

 

MICHEZO miwili ya Ligi Kuu ya NBC imechezwa Septemba 11 katika mikoa ya Tabora na Manyara na kushuhudia timu mwenyeji wa mikoa hiyo Tabora UTD na Fountain Gate zikitakata.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana Tabora UTD iliialika Kagera Sugar kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora na kumalizika kwa Tabora kushinda kwa bao 1 likifungwa kwa mkwaju wa penati na Asiegbu Shedrack.

Saa 10:00 jioni katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa Mkoani Manyara Fountain Gate ikaibamiza Kengold kwa mabao 2-1.

Kengold ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Joshua Ibrahim dakika ya 8 huku bao la kusawazisha la Fountain Gate likifungwa na Kassim Abdallah dakika ya 45, Selemani Mwalimu akafunga ukarasa wa mabao kwenye mchezo huo akifunga bao la pili na la ushindi kwa Fountain Gate.

Kwa matokeo hayo timu ya Tabora United imekwea mpaka nafasi ya nne baada ya kufikisha alama sita huku Fountain ikipanda hadi nafasi ya tatu ikiwa na alama sita zikitofautiana kwa mabao ya kufunga

RATIBA YA NBC CHAMPIONSHIP YATANGAZWA.

 

RATIBA ya Ligi ya NBC Championship imetangazwa leo Septemba 9, na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ikitarajiwa kuanza Septemba 20, 2024.

Mechi za ufunguzi zitawakutanisha Mbeya City dhidi ya Bigman FC katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya saa 10:00 alasiri huku mchezo wa pili ukizikutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya Green Warriors saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Ligi ya NBC Championship inajumuisha jumla ya timu 16 ambazo zitacheza michezo 30 ya nyumbani na ugenini hivyo kufanya ligi hiyo kuwa na jumla ya michezo 240.

Kusoma na kupakua ratiba nzima bonyeza kiunganishi hapa chini.

RATIBA-YA-NBC-CHAMPIONSHIP-2024-2025

BODI YA LIGI KUU TANZANIA YATETA NA WATENDAJI WAKUU WA KLABU ZA LIGIKUU YA NBC.

 

BODI ya Ligi Kuu Tanzania Septemba 5, 2025 imefanya kikao cha majadiliano na watendaji wakuu wa klabu za Ligi Kuu ya NBC ambapo mambo mbalimbali yanayohusu klabu hizo yalijadiliwa.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Steven Mnguto amewataka watendaji wakuu wa klabu hizo kuyafanyia kazi watakayoyapata lakini pia kuwasisitiza juu ya umuhimu wao katika utendaji kazi wa kila siku wa klabu.

“Hii ni semina ambayo ukiwa mtulivu na ukiwa na nia ya kujifunza basi itakuwa ni semina ambayo itakusaidia katika kuendesha klabu yako na pia itakusaidia katika kuendesha mpira wetu kwa ujumla” alisema Mnguto.

Mada mbalimbali katika kikao hicho ziliwasilishwa na wakuu wa idara mbalimbali za bodi ya Ligi Kuu Tanzania.

Mada hizo ni udhibiti na usimamizi wa klabu, Rasilimali watu, usimamizi wa fedha, habari na mawasiliano, masoko na ubunifu, uendeshaji na usimamizi wa Ligi.

Akizungumza baada ya kikao hicho Afisa Mtendaji Mkuu amesema lengo la kikao hicho limefikiwa kwa asilimia mia moja kwani hii ni mara ya kwanza kufanya kikao cha namna hiyo na watendaji wakuu wa klabu.

Miongoni mwa washiriki wa kikao hicho Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate Thabitha Kidawawa ameishukuru Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuwa na kikao cha namna hiyo na kuendelea kuzisaidia klabu katika changamoto mbalimbali zinazozikabili.

SINGIDA BS YATAMBA UGENINI, SIMBA IKIPANDA KILELENI.

 

MICHEZO miwili ya Ligi Kuu ya NBC imechezwa leo Agosti 18, ambapo mapema saa 8:00 mchana Singida BS ikiwa ugenini mkoani Mbeya kwenye uwanja wa Sokoine imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji wao KenGold.

Matokeo ya Singida BS yaliwapandisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC kwa muda kabla ya matokeo ya mchezo wa pili uliozikutanisha Simba dhidi ya Tabora UTD.

Simba iliwakaribisha Tabora UTD katika uwanja wa KMC saa 10:15 jioni na kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 yakifungwa na Che Malone, Valentino Mashaka Kusengama na Awesu Awesu.

Kwa matokeo hayo Simba imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikitofautiana kwa idadi ya mabao na Singida BS na Mashujaa ambao wote wana alama tatu.

LIGI KUU YA NBC KUENDELEA LEO

LADHA ZA LIGI KUU KUENDELEA TENA LEO, NANI KUMTOA MASHUJAA KILELENI ?

 

LADHA za Ligi Kuu ya NBC zinaendelea tena leo Agosti 18, kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Mbeya na
Dar es salaam.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana utawakutanisha mabingwa wa championship msimu uliopita KenGold dhidi ya Singida Black Stars kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Mchezo wa pili utachezwa saa 10:15 alasiri utazikutanisha Simba dhidi ya Tabora United kwenye uwanja wa KMC, Dar es salaam.

Mashujaa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1 dhidi ya Dodoma Jiji bao la kujifunga la Mlinda mlango Daniel Mgore.

Je ni nani kumshusha kileleni Mashujaa leo ? au msimamo utabaki kama ulivyo, majibu tutayapata baada ya dakika 90.