Author: Yahaya Abushehe

SIMBA KUJIULIZA KWA COASTAL, MECHI 3 KUPIGWA LEO.

 

Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo Machi 9 kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Mkoani Morogoro Mtibwa Sugar itaialika Tanzania Prisons saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Manungu huku timu zote mbili zikipata ushindi kwenye michezo yao iliyopita Mtibwa ikiifunga Singida Fountain Gate huku Tanzania Prisons ikiifunga Simba.

Saa 12:00 jioni Coastal Union itaialika Simba katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

Mchezo wa kwanza timu hizo zilipokutana kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es salaam Coastal Union ilipoteza mabao 3-0.

Mchezo wa Mwisho kwa leo utazikutanisha Dodoma Jiji dhidi ya Geita Gold saa 2:15 usiku kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma huku Geita Gold ikiwa nafasi ya 15 moja kutoka mwisho na alama 18 huku Dodoma Jiji ikiwa nafasi ya 9 na alama 23 na kuufanya mchezo kuwa wa ushindani.

YANGA KUREJEA KILELENI LEO ?

 

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Machi 8 kwa mchezo mmoja Kati ya Namungo na Yanga saa 12:00 jioni kwenye uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Ikiwa Yanga itapata matokeo ya Sare au Ushindi itarejea moja kwa moja kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC nafasi ambayo inashikiliwa na Azam kwa sasa iliyopata sare kwenye mchezo wake wa mwisho dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Ushindi katika mchezo huu unaweza kuipeleka timu ya Namungo hadi nafasi ya nne kwenye msimamo kwani itafikisha alama 27 na kuizidi Coastal Union katika tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

HAWA HAPA WAKALI WA MECHI ZA NYUMBANI NBC CHAMPIONSHIP.

 

JUMLA ya michezo 184 ya Ligi ya NBC Championship imechezwa kwenye viwanja mbalimbali kwenye mikoa 11 tofauti ikihusisha michezo ya nyumbani na ugenini kwa kila timu shiriki.

Biashara United inaongoza msimamo kwa timu zilizoshinda mechi nyingi nyumbani ikifanya hivyo mara 10 kwenye michezo 12 iliyocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani Karume mkoani Mara.

Mbeya Kwanza, Mbuni na Mbeya City zinafuata kila timu ikishinda michezo nane zikitofautiana kwenye michezo ya kucheza ambayo Mbeya kwanza imecheza michezo 10, Mbuni ikicheza 11 na Mbeya City ikicheza 12.

Ruvu Shooting ndiyo timu iliyoshinda michezo michache zaidi nyumbani ikishinda mchezo mmoja pekee.

KENGOLD HASHIKIKI NBC CHAMPIONSHIP.

 

MZUNGUKO wa 23 wa Ligi ya NBC Championship umemalizika na kushuhudiwa jumla ya mabao 15 yakifungwa kwenye michezo 8.

kenGold inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi hiyo ikıwa na alama 53 tofauti ya alama nne na timu ya Biashara United huku kila timu ikisalia na michezo saba.

Biashara United inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 49 ikifuatiwa na Pamba yenye alama 48 huku nafasi ya nne ikishikiliwa na Mbeya Kwanza yenye alama 46.

Ruvu Shooting inaendelea kusota nafasi ya mwisho kwenye msimamo licha ya ushindi wake iliyoupata dhidi ya Copco ikiwa na alama 11 kwenye michezo 23.

TANZANIA KINARA IDADI YA TIMU ZILIZOTINGA ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

 

WAWAKILISHI wawili wa Ligi Kuu ya NBC Simba na Yanga wameipaisha Tanzania katika historia ya kuwa nchi pekee Afrika iliyoingiza timu mbili hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/2024.

Yanga imeingia hatua ya robo fainali baada ya kujikusanyia alama nane kwenye michezo sita ikishinda michezo miwili ikipata sare kwenye michezo miwili na kufungwa michezo miwili huku Simba ikiingia hatua hii na alama tisa kwenye michezo sita ikishinda miwili ikipata sare michezo mitatu na kufungwa mchezo mmoja pekee.

Yanga inatarajiwa kukutana na Mamelodi Sundowns, Petro de Luanda au Asec Mimosas huku Simba ikitarajiwa kukutana na Al Ahly, Petro de Luanda au Mamelodi Sundowns.

Hatua ya robo fainali itachezwa Kati ya Machi 29-31 kwa timu zote mbili kuanzia kwenye uwanja wa Nyumbani Benjamin Mkapa.