Author: Yahaya Abushehe

SINGIDA FG, SIMBA NANI KWENDA FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI ?

 

HATUA ya nusu fainali ya kombe la Mapinduzi inamalizika leo januari 10 kwa mchezo kati ya Singida FG na Simba saa 2:15 kwenye uwanja wa New Amaan Complex.

Singida imeingia hatua ya nusu fainali baada ya kuitoa Azam Katika hatua ya robo fainali huku Simba akiitoa Jamhuri.

Singida FG na Simba ndiyo wawakilishi pekee wa Ligi Kuu ya NBC waliobaki ndani ya michuano hii ya Mapinduzi baada ya Azam na Yanga kutolewa katika hatua ya robo faianali.

KEN GOLD TIMU KINARA UFUNGAJI WA MABAO NBC CHAMPIONSHIP.

 

TAYARI mizunguko 16 ya Ligi ya NBC Championship imechezwa na kushudia jumla ya mabao 286 yakifungwa.

Ken Gold ndiyo timu inayoongoza kwa ufungaji wa mabao ikifunga jumla ya mabao 29 katika michezo 16 waliyocheza.

Biashara United ndiyo inafuatia kwa ufungaji wa mabao ikifunga jumla ya mabao 28 kwenye michezo 16, Pamba wanafuata wakiwa na mabao 24 kwenye michezo 16.

Mbeya Kwanza na Mbuni zimefunga jumla ya mabao 23 kwenye michezo yao 16 zikitofautiana kwenye mabao ya kufungwa huku Mbeya kwanza ikifungwa mabao 15 na Mbuni ikifungwa 16.

Ruvu Shooting ndiyo timu iliyofunga mabao machache zaidi kuliko timu nyengine yeyote ikifunga mabao sita pekee.

SINGIDA FG, SIMBA ZATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI.

 

HATUA ya robo fainali ya kombe la mapinduzi imemalizika leo kwa michezo miwili kupigwa.

Robo fainaili ya kwanza kwa leo ilizikutanisha Azam na Singida FG saa 10:15 alasiri kwenye uwanja wa New Amaan Complex na kumalizika kwa Azam kukubali kichapo cha mabao 2-1.

Saa 2:15 usiku Simba ikawakabili Jamhuri na kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 bao pekee la Simba likifungwa na Jean Baleke dakika ya 45+2.

Baada ya matokeo haya Simba na Singida FG watakutana kwenye hatua ya nusu fainali ya pili Jumatano saa 2:15 usiku.

AZAM, SINGIDA, SIMBA KIBARUANI LEO ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI.

 

KOMBE la Mapinduzi hatua ya robo fainali inaendelea leo visiwani Zanzibar huku wawakilishi watatu wa Ligi Kuu ya NBC wakiingia vitani.

Mchezo wa mapema saa 10:15 utawakutanisha wawakilishi wawili wa Ligi Kuu ya NBC Azam wakiwakabili Singida FG.

Azam wamefika hatua ya robo fainali baada ya kuongoza kundi A wakiwa na Alama saba baada ya michezo mitatu huku Singida FG wakimaliza nafasi ya pili kundi B baada ya kujikusanyia alama sita kwenye michezo mitatu.

Mwakilishi mwengine wa Ligi Kuu ya NBC Simba watakuwa na kibarua dhidi ya Jamhuri saa 2:15 usiku.

Simba wamefika hatua hii ya robo fainali baada ya kuongoza kundi B wakiwa na alama Saba baada ya kucheza michezo mitatu huku Jamhuri wakiingia kama best looser baada ya kumaliza nafasi ya tatu kundi C.

BIASHARA, FGA TALENTS, PAMBA ZAONDOKA NA ALAMA 3 NBC CHAMPIONSHIP IKIUNGURUMA.

 

LIGI ya NBC Championship imeendelea kuunguruma hii leo Januari 7 kwa michezo mitatu kupigwa.

Biashara United ya mkoani Mara imewaalika Mbuni ya Arusha katika uwanja wa Karume, Mara saa 8:00 mchana na kumalizika kwa Biashara kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kwa ushindi huu Biashara United inapanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ya NBC Championship wakifikisha alama 33 baada ya michezo 16.

Saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Mabatini mkoani Pwani Cosmopolitan wakawaalika Pamba na mchezo kutamatika kwa Cosmopolitan kukubali kichapo cha mabao 2-1.

Ruvu Shooting ikawa mwenyeji wa FGA Talents saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kushuhudiwa Ruvu Shooting kukubali kichapo cha mabao 3-2.

Michezo ya leo imehitimisha mzunguko wa 16 wa Ligi ya NBC Champioship 2023/2024.