Author: Yahaya Abushehe

MAFUNZO YA ‘VAR’ YAFUNGWA DAR ES SALAAM.

Kozi maalum ya Teknolojia ya Msaidizi wa Video (VAR) iliyofanyika kwa takribani siku 5 kwenye ukumbi wa uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam imefungwa rasmi Jana Aprili 18, 2025 ikijumisha waamuzi 20 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ikiwa ni mwendelezo wa Kozi hiyo yenye jumla ya moduli 6 mpaka kutamatika.

Kozi hiyo ambayo ni sehemu ya mkakati wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha nchi inakuwa na waamuzi waliobobea kwenye matumizi ya teknolojia hiyo ya kisasa inayotumika kusaidia kutoa maamuzi sahihi uwanjani imefungwa rasmi Kwa awamu ya pili na Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF Boniface Wambura ambaye pia ndiye msimamizi Mkuu wa Kozi hiyo inayowezeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Akizungumza baada ya kufunga rasmi awamu ya pili ya Kozi hiyo Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura aliwapongeza waamuzi waliomaliza mafunzo hayo na kuwataka kwenda kutumia vyema ujuzi walioupata kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

Aidha Wambura alieleza kuwa Kozi hiyo ni muendelezo na kwamba TFF itaendelea kuwekeza kwenye teknolojia hiyo Kwa kutoa elimu Kwa waamuzi wengi zaidi na hata kuzalisha wakufunzi wazawa ili kuhakikisha usimamizi wa mechi nchini unaendana sawa na mabadiliko kulingana na wakati Kwa kufuata viwango vya kimataifa.

Ikumbukwe kozi hiyo ni hatua muhimu kuelekea maandalizi ya matumizi rasmi ya VAR katika mechi za ligi kuu ya NBC na mashindano mbalimbali yatakayofanyika ndani ya Tanzania.

MTIBWA KUREJEA LIGIKUU

ALAMA TANO KUIREJESHA MTIBWA LIGI KUU YA NBC.

VINARA wa Ligi ya Championship ya NBC Mtibwa Sugar inahitaji alama tano pekee kujihakikishia nafasi ya kurejea Ligi Kuu ya NBC kwa Mara nyengine tena msimu wa 2025/2026.

Mtibwa Sugar imekusanya jumla ya alama 63 kwenye michezo 26 ya Ligi ya Championship ya NBC ambapo alama tano zitamfanya kufikisha alama 68 huku ikiwa timu moja pekee yenye uwezo wa kufikia alama hizo (Mbeya City).

Ikumbukwe timu mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC zinapanda moja kwa moja Ligi Kuu ya NBC.

Timu zinazoshika nafasi ya tatu na nne kwenye Ligi ya Championship ya NBC zinacheza mchezo wa mtoano kumtafuta mshindi mmoja wa kucheza mchezo wa mtoano wa kupanda (Promotion PlayOff) kwa timu ya Championship au kushuka (Relegation PlayOff) kwa timu ya Ligi Kuu.

‘MBUNGI’ TATU MIKOA MITATU NBC CHAMPIONSHIP LEO.

MICHEZO mitatu ya Ligi ya Championship ya NBC itachezwa leo Aprili 10 kwenye mikoa ya Songea, Pwani na Tanga ikichezwa kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mkoani Songea, timu ya Songea United inaialika Stand United kwenye uwanja wa Majimaji.

Songea inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi hiyo ikiwa na alama 43 huku Stand United ikiwa nafasi ya tatu na alama 52.

Kiluvya ya mkoani Pwani itakuwa mwenyeji wa Mbeya Kwanza ya mkoani Mtwara kwenye uwanja wa Mabatini mkoani Pwani huku mchezo wa duru la kwanza Mbeya kwanza iliifunga kiluvya kwa mabao 2-1 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Mchezo wa mwisho leo unazikutanisha African Sports dhidi ya TMA kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani Tanga.

Hii ni kwa mara ya kwanza msimu huu African Sports inautumia uwanja wa CCM Mkwakwani kama uwanja wake wa nyumbani tangu ulipofanyiwa marekebisho makubwa.

Mapema wiki hii mzunguko wa 26 ulianza kwa mchezo kati ya Biashara United na Mbeya City ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao moja.

AZAM, YANGA NANI KUONDOKA NA ALAMA TATU LEO ?

USIKU wa deni haukawii kukucha ndivyo unavyoweza kusema, baada ya kusuburi wiki, Siku hatimaye yamesalia masaa kuelekea mchezo wa ‘Derby’ ya Dar es Salaam ambapo Azam FC itaialika Young Africans kwenye uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1:00 usiku.

Mara ya mwisho kukutana kwenye Ligi Kuu ya NBC Young Africans ilikubali kichapo cha bao 0-1 likifungwa na Gibril Sillah kwenye uwanja wa Azam Complex.

Young Africans inaingia kwenye mchezo huu ikiwa kinara wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na jumla ya alama 64 kwenye michezo 24 huku Azam FC ikiwa nafasi ya 3 na alama zake 51.

Viingilio vya mchezo huo ni 10,000 kwa mzunguko, 15,000 kwa VIP B na 20,000 kwa VIP A na zinapatikana kupitia wakala yeyote wa N-Card.

GUNNERS MABINGWA WA FIRST LEAGUE 2024/2025

TIMU ya Gunners kutoka mkoani Dodoma imefanikiwa kuwa Bingwa wa First League msimu wa 2024/2025 baada ya kuifunga Hausung mabao 3-0 kwenye mchezo wa Fainali uliochezwa jana Azam Complex, Dar es salaam.

Gunners ilimaliza kinara wa Kundi B ikiwa na alama 35 kwenye michezo 14 hivyo kupata nafasi ya kucheza mchezo wa Fainali ulioipa timu hiyo ubingwa.

Kwa upande wa Hausung ilimaliza kinara wa kundi A ikiwa na alama 25 kwenye michezo 14, alama ambazo ziliipa timu hiyo nafasi ya kucheza mchezo huo wa fainali kumtafuta bingwa wa jumla wa First League 2024/2025.

Timu zote mbili zimekata tiketi ya kushiriki Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/2025 baada ya kumaliza vinara wa makundi yao.