MICHEZO mitatu ya Ligi ya Championship ya NBC itachezwa leo Aprili 10 kwenye mikoa ya Songea, Pwani na Tanga ikichezwa kuanzia saa 10:00 alasiri.
Mkoani Songea, timu ya Songea United inaialika Stand United kwenye uwanja wa Majimaji.
Songea inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi hiyo ikiwa na alama 43 huku Stand United ikiwa nafasi ya tatu na alama 52.
Kiluvya ya mkoani Pwani itakuwa mwenyeji wa Mbeya Kwanza ya mkoani Mtwara kwenye uwanja wa Mabatini mkoani Pwani huku mchezo wa duru la kwanza Mbeya kwanza iliifunga kiluvya kwa mabao 2-1 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Mchezo wa mwisho leo unazikutanisha African Sports dhidi ya TMA kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani Tanga.
Hii ni kwa mara ya kwanza msimu huu African Sports inautumia uwanja wa CCM Mkwakwani kama uwanja wake wa nyumbani tangu ulipofanyiwa marekebisho makubwa.
Mapema wiki hii mzunguko wa 26 ulianza kwa mchezo kati ya Biashara United na Mbeya City ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao moja.