Category: STORY

GEITA YATAMBA UGENINI.

TIMU ya Geita Gold imeendelea kung’ara ikicheza ugenini baada ya kupata suluhu dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Geita imeanza vema Ligi Kuu ya NBC kwa kukusanya alama nne katika michezo miwili bila kuruhusu bao lolote tofauti na msimu uliopita waliporuhusu mabao manne katika michezo miwili ya mwanzo.

Mashujaa iliyopanda daraja msimu huu imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Kagera Sugar na suluhu ya leo inaifanya timu hiyo kufikisha alama nne na kukaa nafasi ya pili ya msimamo wa ligi nyuma ya Simba.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Agosti 22 kwa mchezo mmoja kati ya Singida Big Stars na Tanzania Prisons utakaochezwa uwanja wa Liti, Singida saa 10:00 alasiri.

SIMBA YAENDELEA ILIPOISHIA, MTIBWA, COASTAL HAKUNA MBABE.

TIMU ya Simba imepata ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 2-0 na Kukwea kileleni mwa msimamo kwa mara ya kwanza msimu huu.

Dodoma iliyoanza Ligi vema msimu huu kwa kuifunga Coastal Union mabao 2-1 imeshindwa kutamba mbele ya ‘Mnyama’ kwa mabao yaliyofungwa na Jean Baleke kipindi cha kwanza na Moses Phiri kipindi cha pili.

Mabao hayo yanaifanya Simba iliyofunga mabao sita kuwa kinara kwa kufunga mabao msimu huu mpaka sasa.

Mkoani Morogoro timu ya Mtibwa imeshindwa kutamba kwa mara nyingine ikiwa nyumbani baada ya kutoka sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga.

Bao la mpira wa adhabu lililofungwa na Ibrahim Ajibu kwa Coastal na bao la Kassim Haruna yamefanya timu hizo kutoshana nguvu na kuendelea kusubiri kwa michezo inayofuata kupata ushindi wa kwanza msimu huu.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Agosti 21, kwa mchezo mmoja kati ya Mashujaa itakayokuwa mwenyeji wa Geita Gold saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

KAGERA NA MKOSI WA MSIMU ULIOPITA

TIMU ya Kagera Sugar imeendeleza rekodi mbaya ya mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kufungwa bao 1-0 na Ihefu ya Mbeya.

Kagera Sugar tayari imepoteza michezo miwili msimu huu dhidi ya Mashujaa na Ihefu idadi sawa na michezo miwili ya mwanzo msimu uliopita ilipofungwa na timu za Azam na Simba.

Bao la Ihefu limefungwa na Moubarack Amza na kuifanya Ihefu kupata ushindi wa kwanza msimu huu baada ya kufungwa na Geita Gold mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Timu ya Namungo imeendelea kusota uwanja wa nyumbani baada ya kushindwa kupata ushindi na kuambulia sare ya bao moja dhidi ya KMC ya Dar.

Namungo iliyopoteza mchezo wa ufunguzi dhidi ya JKT iliyopanda daraja kwa bao moja imeambulia alama moja pekee ikiwapeleka nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu NBC.

Ligi hiyo itaendelea kesho Agosti 20 kwa michezo miwili kati ya Mtibwa na Coastal Union uwanja wa Manungu, Morogoro saa 8:00 mchana na Simba itakakua mwenyeji wa Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Uhuru, Dar saa 10:00 alasiri.

SIMBA YANGURUMA MANUNGU.

TIMU ya Simba imeanza Ligi Kuu ya NBC kwa kishindo baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 4-2 kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro.

Msimu uliopita Jean Baleke aliifunga Mtibwa mabao matatu na leo ameendeleza ubabe kwa timu hiyo baada ya kufunga bao moja huku mabao mengine yakifungwa na Fabrice Ngoma, Esomba Onana na Clatous Chama.

Mabao ya kufutia machozi ya Mtibwa yamefungwa na Matheo Anthony aliyecheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC kama mchezaji wa Mtibwa Sugar.

Simba imepata ushindi huo siku nne baada ya kutwaa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa ushindi wa mikwaju ya penati 3-1.

Ligi hiyo itaendelea tena Agosti 19 kwa michezo miwili itakayochezwa kati ya Ihefu na Kagera Sugar uwanja wa Highland Estates na Namungo dhidi ya KMC itakayochezwa uwanja wa Majaliwa, Lindi.

MASHUJAA YAANZA LIGI KUU KISHUJAA.

TIMU ya Mashujaa ya Kigoma iliyopanda Ligi Kuu ya NBC ikitokea Ligi ya championship imeanza kibabe baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Mashujaa ilipata mabao yake kupitia kwa Adam Adam dakika ya 15 na Othman Dunia dakika ya 73 kwa mashuti yaliyopigwa kwa mguu wa kushoto.

Timu ya Kagera imepoteza mchezo wa kwanza wa ligi kwa misimu miwili mfululizo baada ya kupoteza pia kwa Azam ya Dar msimu uliopita kwa mabao 2-1.

Mchezo wa pili siku ya leo haukuweza kuendelea na kumalizwa dakika ya 18 baada ya wachezaji wawili wa Kitayosce kuumia na kusalia sita pekee ambao kikanuni hawaruhusiwi kuendelea na mchezo.

Hadi mchezo huo unamalizwa Azam ilikuwa inaongoza kwa mabao 4-0 yaliyofungwa na Prince Dube na Feisal Salum ‘Feitoto’ aliyefunga mabao matatu ‘Hat-trick’.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaokutanisha timu za Mtibwa Sugar na Simba utakaochezwa uwanja wa Manungu, Morogoro.