Category: STORY

YANGA YAIPIGISHA ‘KWATA’ JKT.

TIMU ya Yanga imeshinda mchezo wa pili mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kufunga mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Mabao ya Stephane Ki Aziz, Kenedy Musonda, Kouasi Yao, na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili yametosha kuiweka Yanga nafasi ya kwanza msimu huu ikiwa bingwa mtetezi kwa kufikisha alama sita.

Mpaka sasa timu ya Yanga ndio kinara wa kufunga mabao (10) huku ikiwa haijafungwa bao lolote sawa na timu za Mashujaa, Geita Gold na Singida Big Stars.

Yanga imeendeleza ubabe kwa JKT kwa kushinda michezo sita kwenye michezo saba iliyopita wakitoka sare mchezo mmoja .

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Agosti 31, kwa mchezo mmoja wa kukamilisha mzunguko wa pili kati ya Singida Big Stars na Tabora United kwenye uwanja wa Liti, Singida.

MABINGWA WAWILI ‘KUKIWASHA’ LEO AZAM COMPLEX.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Agosti 29 kwa mchezo mmoja kati ya Yanga na JKT Tanzania kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Mchezo huu unaikutanisha Yanga iliyokuwa bingwa wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita na JKT iliyokuwa bingwa wa Ligi ya Championship msimu uliopita.

Timu hizo zinacheza mchezo wa pili wa ligi msimu huu kila moja ikiwa haijafungwa bao lolote na zote zikifanikiwa kushinda michezo yao ya ufunguzi.

Yanga ndiye kinara wa ushindi anapokutana na JKT akishinda michezo mitano kati ya sita waliyokutana huku wakitoka sare katika mchezo mmoja.

AZAM FC YAKAA KILELENI NBCPL.

TIMU ya Azam imepanda mpaka nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Prisons ya Mbeya kwa mabao 3-1.

Mabao ya Prince Dube, Iddy Selemani na Nathaniel Chilambo yameifanya Azam kushika nafasi ya kwanza na kuwa timu kinara wa kufunga mabao (7).

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Agosti 29 kwa mchezo mmoja kati ya Yanga na JKT Tanzania utakaochezwa uwanja wa Azam Complex, Dar saa 1:00 usiku huku timu zote zikifanikiwa kushinda michezo yake ya kwanza msimu huu.

YANGA YAENDELEZA UBABE.

TIMU ya Yanga imeanza Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/24 kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar kwa kishindo baada ya kuifunga KMC mabao 5-0.

Dickson Job, Ki Aziz, Hafiz Konkoni, Midathir Yahya, na Pacome Zouzoua ndio walioifanya timu ya Yanga kuwa timu iliyofunga mabao mengi katika mchezo mmoja mpaka sasa katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

Yanga ilimaliza msimu uliopita kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons na kutwaa ubingwa ikiwa imepoteza michezo miwili pekee dhidi ya Ihefu na Simba.

Ligi hiyo itaendelea tena Agosti 28 kwa mchezo utakaochezwa uwanja wa Azam Complex, Dar kati ya Azam na Tanzania Prisons saa 3:00 usiku.

GEITA YATAMBA UGENINI.

TIMU ya Geita Gold imeendelea kung’ara ikicheza ugenini baada ya kupata suluhu dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Geita imeanza vema Ligi Kuu ya NBC kwa kukusanya alama nne katika michezo miwili bila kuruhusu bao lolote tofauti na msimu uliopita waliporuhusu mabao manne katika michezo miwili ya mwanzo.

Mashujaa iliyopanda daraja msimu huu imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Kagera Sugar na suluhu ya leo inaifanya timu hiyo kufikisha alama nne na kukaa nafasi ya pili ya msimamo wa ligi nyuma ya Simba.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Agosti 22 kwa mchezo mmoja kati ya Singida Big Stars na Tanzania Prisons utakaochezwa uwanja wa Liti, Singida saa 10:00 alasiri.