Category: STORY

PAZIA LA NBC CHAMPIONSHIP KUFUNGWA LEO.

KILELE cha ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/25 kinatarajiwa kufikiwa leo kwa mchezo wa kukabidhi ubingwa kati ya Mtibwa Sugar na Mbeya City utakaopigwa leo kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam saa 2:00 usiku.

Ligi hiyo ilifika tamati Mei 11, kwa michezo nane kupigwa na Mtibwa Sugar kumaliza bingwa na kupanda daraja akifikisha jumla ya alama 71 huku Mbeya City ikimaliza nafasi ya pili na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 sambamba na Mtibwa.

Mtibwa Sugar imerejea Ligi Kuu ya NBC ikiwa ni msimu mmoja pekee tangu kushuka daraja huku Mbeya City ikitumia misimu miwili kurejea ligi hiyo.

Mchezo wa leo utarushwa mubashara TV3 na utakuwa sambamba na sherehe za kukabidhi ubingwa kwa timu ya Mtibwa Sugar baada ya kumaliza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi ya Championship ya NBC.

TABORA, KMC KUFUNGA MZUNGUKO WA 28 LIGI KUU YA NBC.

MZUNGUKO wa 28 unatarajiwa kukamilika leo kwa mchezo mmoja utakaozikutanisha timu za Tabora United kutoka mkoani Tabora dhidi ya KMC ya Dar es Salaam saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

KMC itashuka ugenini ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Simba kwa mabao 1-2 kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Hadi sasa ikicheza viwanja vya ugenini KMC imeshinda mchezo mmoja pekee, kufungwa michezo saba huku ikitoka sare minne na kukusanya alama saba pekee.

Tabora inashuka uwanjani ikiwa haijafanikiwa kupata ushindi kwenye michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu ya NBC na mara ya mwisho kushinda ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao moja lililofungwa na Offen Chikola kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

AZAM YAFANYA ‘MAUAJI’ LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Azam kutoka Dar es Salaam imeishushia kipigo kizito Dodoma Jiji cha mabao 5-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa uwanja wa Azam Complex, Dar.

Hiki ni kipigo kikubwa zaidi hadi sasa kwenye mzunguko wa 28 ukisalia mchezo mmoja pekee utakaopigwa leo kukamilisha mzunguko huo.

Nahodha wa Azam Lusajo Mwaikenda alikuwa mfano wa kuigwa na wenzake baada ya kufungua ukurasa wa mabao kwa timu yake dakika ya sita ya mchezo huku Abdul Sopo, Gibril Sillah, Nassor Saadun na Frank Tiesse wakifunga bao moja kila mmoja na kukamilisha karama hiyo ya mabao.

Dodoma Jiji imepoteza mchezo wa 12 ikisalia nafasi ya saba baada ya kukusanya alama 34 ikiwa imeshinda michezo tisa hadi sasa huku ikihitaji alama tatu pekee kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

Baada ya kufunga mabao matano Azam imefikisha jumla ya mabao 48 na kushika nafasi ya tatu kwa idadi kubwa ya mabao nyuma ya Simba yenye mabao 62 na Young Africans inayoongoza ikiwa na mabao 71.

YOUNG AFRICANS YASHIKILIA ‘USUKANI’ LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inazidi kushika kasi Iikielekea ukingoni huku timu ya Young Africans ikiendelea ilipoishia baada ya kuichapa Namungo 3-0 kwenye uwanja wa KMC Complex mkoani Dar es Salaam.

Ilimchukua dakika 27 kiungo wa Young Africans Aziz Ki kufungua ukurasa wa mabao na dakika nne baadae mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Zimbabwe Prince Dube aliipatia timu yake bao la pili hivyo kwenda mapumziko ikiongoza 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi timu ya Namungo ikionekana kusaka namna ya kupata bao ambapo juhudi zao hazikuzaa matunda na dakika ya 74 mchezaji wa Young Africans Maxi Nzegeli aliipatia timu yake bao la tatu na mpaka dakika 90 zinatimia ubao wa matokeo ulikuwa unasoma 3-0.

Matokeo hayo yanaifanya Young Africans kufikisha alama 73 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu ya NBC huku timu hiyo ikisaliwa na michezo mitatu kuhitimisha Ligi hiyo.

Mchezaji wa Young Africans Maxi Nzegeli alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kiwango kizuri alichoonyesha katika mchezo huo akifunga bao na kutoa pasi ya bao la Stephane Aziz Ki.

KAGERA SUGAR RASMI NBC CHAMPIONSHIP

 

 

TIMU ya Kagera Sugar imeaga rasmi Ligi Kuu ya NBC baada ya timu ya Pamba Jiji kuifunga KenGold 0-2 ugenini na kufikisha alama 30 ambazo haziwezi kufikiwa na Kagera ikiwa itashinda michezo yake miwili iliyosalia.

Pamba Jiji ilipata bao lake la kuongoza kipindi cha kwanza lililofungwa na mchezaji Yonta Camara dakika ya 30 anayecheza kwa mkopo kwenye timu hiyo kutokea Singida Black Stars.

Kipindi cha pili Yonta Camara kwa mara nyingine aliipatia bao la pili timu yake Dakika ya 60 na kufanya matokeo kuwa 0-2 hivyo kuzamisha matumaini ya Kagera kuendelea kusalia Ligi Kuu ya NBC .

Pamba jiji imefikisha alama 30 ikiwa nafasi ya 11 huku KenGold ikiwa tayari imeshuka daraja baada ya kukusanya alama 16 ikicheza msimu mmoja pekee wa Ligi Kuu ya NBC tangu kupanda ligi ya NBC championship.