Category: STORY

STAND, GEITA KUISAKA LIGI KUU YA NBC.

IKITAMATIKA kwa mzunguko wa 30 ligi ya Championship ya NBC na kushuhudia Mtibwa Sugar ikiibuka mabingwa wa ligi hiyo na Mbeya City kupanda daraja timu za Stand United ya Shinyanga na Geita Gold ya Geita bado zina nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

Stand iliyomaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itacheza michezo ya mtoano kwenye uwanja wa nyumbani na ugenini dhidi ya Geita Gold na mshindi wa mchezo huo atacheza na timu ya Ligi Kuu ya NBC itakayopoteza mchezo wake wa mtoano.

Mchezo wa mwisho timu hizo kukutana ulikuwa mchezo wa kufunga pazia la ligi ya Championship ya NBC mzunguko wa 30 na kumalizika kwa sare ya 1-1 timu ya Stand ikiwa nyumbani kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mshindi wa jumla wa michezo yote miwili atacheza na timu itakayopoteza mchezo wake wa mtoano kutoka Ligi Kuu ya NBC na endapo timu ya Championship itashinda itapanda Ligi Kuu na endapo timu ya Ligi Kuu itashinda basi itasalia kwenye ligi hiyo kwa msimu wa 2025/26.

NYASI ‘KUWAKA’ MOTO LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC leo inatimua vumbi kwa michezo miwili itakayopigwa kwenye viwanja vya Sokoine, Mbeya na Kaitaba, Kagera.

Mchezo wa saa 10:00 alasiri utakuwa kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Coastal Union ambapo Prisons inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kujiondoa kwenye nafasi ya kucheza michezo ya mtoano.

Endapo Prisons inayoshika nafasi ya 14 itashinda itafikisha alama 30 na itakuwa nyuma ya Coastal Union inayoshika nafasi ya nane kwa tofauti ya alama moja pekee.

Mchezo wa mwisho utapigwa mkoani Kagera kwenye uwanja wa Kaitaba saa 12:30 jioni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Mashujaa.

Kagera inayoshika nafasi ya 14 inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kufufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu 2025/26 huku Mashujaa ikihitaji alama tatu muhimu kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye ligi hiyo.

AHOUA MKALI WA ‘KUCHEKA NA NYAVU’ LIGI KUU YA NBC.

KIUNGO wa timu ya Simba Jean Ahoua ameendelea kujiimarisha kwenye mbio za ufungaji bora baada ya kufikisha mabao 15 ikiwa ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Ahoua amefanikiwa kufunga mabao hayo akiwa amecheza mechi 24 kwa jumla ya dakika 1773 katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025.

Clement Mzize wa Young Africans anafuata akiwa amefanikiwa kufunga mabao 13 huku mchezaji mwenzake Prince Dube wa timu hiyo akifanikiwa kucheka na nyavu za wapinzani wao mara 12 sawa na Leonel Ateba wa Simba.

Steven Mukwala wa Simba na Jonathan Sowah wa Singida Black Stars wamefanikiwa kufunga mabao 11 kila mmoja huku Elvis Rupia wa Singida Black Stars akitupia nyavuni mabao 10.

COSMOPOLITAN YAAGA NBC CHAMPIONSHIP

TIMU ya Cosmopolitan kutoka Dar es Salaam imeshuka daraja kutoka Ligi ya Championship ya NBC na kuungana na Biashara United ya Mara hivyo rasmi timu hizo zitashiriki ligi ya First League msimu wa 2025/26.

Cosmopolitan imeshuka daraja baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Songea United kwenye mchezo wa mwisho wa ligi hiyo.

Timu hiyo imeshuka daraja huku ikiwa imefunga mabao machache (19) sawa na timu ya Kiluvya kutoka Dar es Salaam itakayocheza hatua ya mtoano kutafuta nafasi ya kusalia ligi ya Championship ya NBC.

Cosmopolitan imeaga ligi ya Championship ya NBC ikiwa imeshinda michezo michache (5) sawa na timu ya Transit Camp inayotafuta nafasi ya kusalia kwenye ligi hiyo endapo itashinda mchezo wake wa hatua ya mtoano dhidi ya Kiluvya.

SIMBA ‘YAIBAMIZA’ KMC LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea leo kwa mchezo mmoja uliochezwa uwanja wa KMC Complex, mkoani Dar es Salaam kati ya KMC ikiikaribisha timu ya Simba na kushuhudia ‘Mnyama’ akishinda 1-2 ugenini.

Mchezo huo ulianza majira ya saa kumi alasiri kwa timu zote kuwa na ari ya kuzitaka alama tatu muhimu KMC ikitaka kujihakikishia nafasi ya kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu ujao huku Simba ikijiimarisha kwenye mbio za ubingwa.

Dakika nane ziliitosha timu ya KMC kufungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Rashid Chambo kabla ya timu ya Simba kusawazika kupitia mshambuliaji wake Steven Mukwala dakika ya 15 ya mchezo na dakika 46 aliongeza bao la pili hivyo mchezo kumalizika kwa 1-2.

Simba imefikisha alama 69 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifunga mabao 62 na kuruhusu mabao 11 katika michezo 26 ambayo timu hiyo imecheza huku KMC ikiwa nafasi ya 11 na alama 30 ikifunga mabao 23 na kuruhusu mabao 41 katika michezo 27 ambayo timu hiyo imeshacheza.