Category: STORY

MTIBWA SUGAR MABINGWA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC 2024/2025.

TIMU ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/2025.

Mtibwa Sugar kwenye mchezo wake wa mwisho hii Leo dhidi ya Kiluvya iliyochezwa kwenye uwanja wa Manungu Complex imefanikiwa kuibuka na kushinda wa mabao 2-0 myaliyofungwa na Raizin Hafidh dakika ya 36 na 46 ya mchezo huo.

Baada ya ushindi huo Mtibwa Sugar inafikisha alama 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote inayoshiriki Ligi ya Championship ya NBC.

Mtibwa Sugar ambayo ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita imefanikiwa kufunga mabao 58 huku ikifungwa mabao 18 hivyo kujihakikisha nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026.

NBC CHAMPIONSHIP KUHITIMISHWA LEO.

PAZIA la Ligi ya Championship ya NBC linafungwa leo Mei 11 kwa michezo nane kupigwa kwenye viwanja nane tofauti kuanzia saa 10:00 alasiri.

Michezo ya Leo itamtambulisha bingwa wa Ligi ya Championship ya NBC Kati ya Mtibwa Sugar au Mbeya City pia kujua ni timu gani itaungana na Biashara United kushuka daraja.

Mtibwa ili kuwa bingwa inahitaji alama moja pekee ili kufikisha alama 69 ambazo haziwezi kufikiwa na Mbeya City na endapo Mbeya City itapata matokeo yoyote tofauti na ushindi Mtibwa itakuwa bingwa.

Kwa upande wa Mbeya City inahitaji kushinda ili kufikisha alama 68 na endapo Mtibwa ikipoteza mchezo wa leo timu hizo zitalingana alama na Mbeya City atakuwa bingwa kwa tofauti ya mabao.

Vita nyengine ni ya kushuka daraja ambapo klabu za African Sports, Cosmopolitan na Transit Camp zipo kwenye hatari ya kushuka na kuungana na Biashara United.

African Sports ina alama 19 wakati Cosmopolitan ina alama 20 na Transit Camp ikiwa na alama 21, michezo ya mwisho hii Leo itatoa hatma ya timu hizo msimu huu

CARGO, KAJUNA ZATAMBA NYUMBANI MTOANO FIRST LEAGUE.

Michezo ya mtoano (PlayOff) kubaki au kupanda ligi ya First League imechezwa Jana Mei 8 ikishuhudiwa timu zilizokuwa nyumbani Cargo ya Dar na Kajuna ya Kigoma zikiibuka na ushindi.

Mchezo wa kwanza katika uwanja wa TFF Center – Kigamboni uliishuhudia Cargo ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tunduru Korosho.

Mchezo wa pili mkoani Kigoma uliishuhudia Kajuna ikiifunga Copco ya Mwanza kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika.

Michezo ya marudiano itapigwa Mei 12 ambapo Tunduru Korosho itaialika Cargo kwenye uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma huku Copco ikiialika Kajuna kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.

AHOUA HASHIKIKI, SIMBA IKIWASHA MOTO LIGI KUU YA NBC

UTAMU wa Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika unazidi kukolea timu ya Simba ikiichapa timu ya Pamba Jiji kutoka jijini Mwanza mabao 5-1.

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa KMC uliopo Mwenge mkoani Dar es Salaam ulishuhudia kiungo wa timu ya Simba Jean Ahoua akifunga Mabao matatu (Hat-Trick).

ilimchukua dakika 16 kufungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati kabla ya kurejea wavuni tena dakika ya 37 hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiongoza 2-0 dhidi ya Pamba Jiji.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Ahoua aliongeza bao la tatu hivyo kukamilisha hat-trick dakika ya 48 ya mchezo na mshambuliaji Leonel Ateba aliongeza mabao mawili kwa timu yake ikiwa ni dakika ya 80 na 82 ya mchezo huo huku mchezaji wa Pamba Jiji.

Mathew Momanyi alifunga bao la kufutia machozi kwa timu yake ya Pamba dakika ya 86 hivyo mchezo huo kumalizika 5-1.

Ushindi huo unaifanya timu ya Simba kufikisha alama 66 ikiendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku Jean Ahoua akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

KIVUMBI CHA LIGI KUU YA NBC KUENDELEA LEO.

IKIELEKEA siku za mwisho za msimu wa 2024/25 Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaokutanisha timu ya Simba itakayokuwa uwanja wa nyumbani wa KMC Complex dhidi ya Pamba Jiji kutoka Mwanza.

Simba iliyoshinda mchezo wake uliopita kwa bao moja ugenini dhidi ya JKT Tanzania inarudi uwanjani leo kucheza na Pamba Jiji iliyolazimishwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Fountain Gate.

Pamba inaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa timu namba tatu kwa kushinda michezo michache ikishinda sita, nyuma ya Kagera iliyoshinda mitano na KenGold iliyoshinda mitatu.

Simba inaingia kwenye mchezo wa leo akiwa imepoteza mchezo mmoja pekee huku ikiwa timu iliyoruhusu mabao machache hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC ikifungwa tisa.