Category: STORY

LIBASSE,MANQOBA WANG’ARA TUZO ZA LIGI KUU YA NBC AGOSTI.

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Libasse Gueye, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2026/27, huku Manqoba Mngqithi wa Young Africans, akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Gueye alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Maxi Nzengeli wa Young Africans na Oscar Mwajanga wa Mbeya City, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitano ambayo Simba ilicheza mwezi huo na kushinda yote, huku nyota huyo akifunga bao moja na kuhusika na mengine matano.

Kwa upande wa Manqoba aliyeingia fainali na Steve Barker wa Simba na Florent Ibenge wa Azam, aliiongoza Young Africans kushinda michezo yote mitano iliyocheza mwezi huo na kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi.

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Bukombe uliopo mkoani Geita,Deogratius Dayan kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Agosti kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Kamati pia imeteua mabao matatu ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata bao bora la mwezi Agosti. Mabao hayo ni yaliyofungwa na Shekhan Hamis (Singida BS Vs Polisi Tanzania), Robert Mathias (Geita Gold Vs Kagera Sugar) na Hija Shamte (Mbeya City v Mashujaa)

Imetolewa na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

Septemba 11, 2026

MBIO ZA UBINGWA WA LIGI KUU YA NBC ZIMEANZA ‘ASUBUHI’

Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27 zimeanza mapema kwa kasi huku wapinzani wa jadi timu za Young Africans (Yanga) na Simba, zikionyesha mapema kuwa huenda tena wakawa wahusika wakuu katika vita ya kutwaa taji la ligi msimu huu.

Hadi sasa, baada ya kila timu kucheza michezo mitano, Yanga na Simba zimekusanya alama 15 kila mmoja, zikiwa zimeshinda michezo yote mitano ya mwanzo huku tofauti kati yao ikiwa kwenye mabao ambapo Yanga ikifunga mabao 15 huku Simba ikiwa imefunga tisa ,jambo linalowafanya mabingwa watetezi Yanga kushika nafasi ya kwanza.

Yanga na Simba zimekuwa na mwanzo wa kuvutia kwenye eneo la ulinzi zikiruhusu mabao mawili pekee ambapo timu hizo zinaongozwa na manahodha wao kwenye eneo hilo, Rushine De Reuck akiwa Simba na Bakari Mwamnyeto akiwa Yanga.

Hii ina maana kwamba, katika hatua hii ya mwanzo wa msimu, hakuna hata mmoja kati ya ‘watani’ hawa aliyeko tayari kupoteza mchezo wowote huku pia timu hizo zikiiwakilisha nchi kwenye Kombe la Mabingwa Afrika.

Kwa miaka mingi, pambano la Simba na Yanga limekuwa zaidi ya mechi mbili wanapokutana uwanjani. Ni pambano linaloendelea katika kila mchezo wa msimu, ambapo ushindi wa Yanga unakuwa presha kwa Simba kushinda mechi yake inayofuata, na ushindi wa Simba unaiweka Yanga kwenye wajibu wa kujibu.

Libasse Gueye wa Simba ameendelea kuwa muhimili wa Simba kwenye eneo la ushambuliaji akiwa amefunga bao moja na kutoa pasi za mabao tano huku usajili mpya wa Yanga Peter Shalulile akiwa kinara baada ya kufunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao.

Ligi Kuu ya NBC inaendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa uwanja wa Jamhuri, Dodoma kati ya Dodoma Jiji na Namungo timu hizo zikiwa zimepishana kwa alama moja pekee ambapo Dodoma imekusanya alama saba na Namungo alama sita.

CHAMPIONSHIP 2026/27 KUANZA RASMI LEO.

Ligi ya Championship ya NBC msimu 2026/27 inaanza rasmi leo kwa michezo mitatu itakayochezwa katika viwanja tofauti huku timu zikianza safari ya kuwania nafasi za kupanda Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo kwanza utapigwa katika uwanja wa Ali hassan Mwinyi mkoani Tabora timu ya Rhino Rangers itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye mchezo utakaorushwa mubashara kupitia chaneli ya FIFA+.

Dar es salaam, KMC itawakaribisha Mbuni katika uwanja wa KMC katika mchezo utakaoonyeshwa kupitia Ligi Kuu TV kupitia mtandao wa youtube.

Katika mchezo mwingine katika mkoa wa Dar es salaam kigamboni united itakuwa mwenyeji wa TMA katika uwanja wa uhuru , na michezo yote itapigwa saa 10:00 alasiri.

Ufunguzi huo unatarajiwa kuleta ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuanza msimu zikiwa na malengo mapya huku mashabiki wakisubiri kuona kiwango cha timu zao baada ya maandalizi ya msimu mpya.

MBEYA CITY YAJIPATA, AZAM YAILIZA PAMBA JIJI LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kushika kasi ikiwa ni mzunguko wa tatu wa ligi hiyo ambapo timu ya Mbeya City ilikuwa mwenyeji wa timu ya Mashujaa huku Azam ikiikaribisha timu ya Pamba Jiji.

Mchezo wa kwanza ulikuwa katika uwanja wa Sokoine ambapo mwenyeji Mbeya City aliikaribisha Mashujaa kwa kasi kubwa ikiwa kila timu ilikuwa ikizitaka alama tatu muhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku timu hizo zikienda mapumziko bila kufungana mabao.

Kipindi cha pili kilirejea na timu zote zilikuwa zikionyesha ushindani ambapo iliwachukua dakika 52 timu ya Mashujaa kufungua ukurasa wa mabao kupitia mchezaji wao Hijjah Shamte huku Adilly Buha wa Mbeya City akisawazisha kupitia mkwaju wa penati na dakika ya 79 na Oscar Mwajanga aliiongezea bao la pili timu ya Mbeya City hivyo mchezo kuisha kwa 2-1.

Mchezaji wa Mbeya City Ismail Aziz alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kiwangzzo kizuri alichoonyesha.

Mchezo wa pili ulichezwa majira ya saa moja jioni katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam ambapo mwenyeji timu ya Azam aliikaribisha timu ya Pamba Jiji.

Mchezo ulianza kwa timu zote kucheza kwa tahadhari kubwa ili kuhakikisha hazipotezi alama ambapo iliwachukua dakika 24 timu ya Azam kufunga bao la kwanza kupitia mchezaji wao Enock Molia huku Pamba jiji ikisawazisha dakika ya 45 ya mchezo huo kupitia mchezaji wao Nonyem Okorocha na timu hizo zilienda mapumziko 1-1.

Kipindi cha pili kilirejea na mchezaji wa Azam, Abdul Suleiman alifunga bao la pili kupitia mkwaju wa penati baada ya Iddi Seleman kuchezewa madhambi na mchezaji wa Pamba Jiji na mchezo ulitamatika kwa 2-1 mchezaji wa Azam Iddy Seleman alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

GEITA ‘YAUA’ BUKOMBE, SIMBA IKIENDELEZA UBABE LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo miwili iliyotoa burudani kubwa kwa mashabiki, Singida Black Stars waliwakaribisha simba na kupoteza 1-2 kwenye uwanja wa Airtel mkoani Singida huku Geita Gold ikianza vyema kwenye uwanja wake mpya kwa ushindi mnono wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Clatous Chama aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 12, Sheikhah Ibrahim wa singida akaweka mzani sawa dakika ya 22 na kuwainua mashabiki wa Singida.

Hata hivyo, Simba ilirejea ikiwa na nguvu zaidi kipindi cha pili na kufanikiwa kuongoza mchezo kupitia Rushine De Reuck, aliyefunga dakika ya 62.

Mchezo huo pia ulishuhudia Simba ikicheza ikiwa pungufu baada ya Anthony Mligo kuonyeshwa kadi nyekundu na kuwa mchezo wa tatu mfululizo Simba kupata kadi nyekundu tangu ligi ianze.

Katika mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa kisasa wa Bukombe, mkoani Geita, ambapo Geita Gold ilianza kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo huo ulikuwa wa kipekee kwa timu hizo mbili ambazo zimepanda kutoka Championship na kushiriki Ligi Kuu, huku ikiwa pia ni mara ya kwanza kwao kucheza katika uwanja huo mpya uliopo Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, ambao Geita Gold inautumia kama uwanja wake wa nyumbani.

Geita Gold ilianza kuandika historia hiyo dakika ya 10 kupitia Richard N’gondya, kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 23 kupitia Obrey Chirwa kwa mkwaju wa penalti.

Yussufu Mhilu aliendelea kuipa Geita Gold nguvu kwa kufunga dakika ya 34 na 46, huku Richard N’gondya akifunga bao lake la pili katika mchezo huo dakika ya 63.

Chirwa alikamilisha siku yake nzuri kwa kufunga bao la pili dakika ya 69 na kuifanya Geita Gold kufikisha mabao sita.

Kagera Sugar ilipata mabao mawili ya kufutia machozi, yakifungwa na Hassan Mwatelema dakika ya 40 na Robert Mkandya dakika ya 90+1.

Ushindi huo unaifanya Geita Gold kuanza safari yake ya Ligi Kuu kwa kiwango cha kuvutia, huku mchezo huo ukitoa burudani kubwa kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia historia ya timu hizo kwenye uwanja mpya.