Category: STORY

MBILI ZA MOTO LEO LIGI KUU YA NBC.

MZUNGUKO wa 26 wa Ligi Kuu ya NBC unatamatika leo kwa michezo miwili itakayochezwa mkoani Dar es Salaam na Mbeya.

Wachezaji wa Simba.

Simba iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC inayosaka nafasi ya kutwaa ubingwa itakuwa mwenyeji wa timu ya Pamba Jiji kutoka jijini Mwanza inayoshika nafasi ya saba ambapo timu hiyo inatafuta kujiimarisha katika nafasi nzuri huku mchezo huo ukitarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa KMC Complex majira ya saa kumi jioni.

Wachezaji wa Pamba Jiji

Sambamba na mchezo huo Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikisaka kujinasua kushuka daraja itaikaribisha timu ya Dodoma Jiji inayoshika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi hiyo ambayo pia inatafuta kujiweka katika nafasi nzuri.

NBC CHAMPIONSHIP YA MOTO LEO.

MZUNGUKO wa 29 wa Ligi ya NBC Championship unaendelea leo kwa michezo nane itakayochezwa majira ya saa kumi jioni.

Mchezo wa kwanza utakuwa uwanja wa Majimaji ambapo Songea United itakuwa mwenyeji wa timu ya Hausung huku Ken Gold ikichuana na B19 kwenye uwanja wa Chunya mkoani Mbeya.

Polisi Tanzania itaikaribisha timu ya Mbeya Kwanza katika uwanja wa Usharika mkoani Kilimanjaro mchezo utakaokuwa mbashara kwenye chaneli ya FIFA +, huku African Sports ikimenyana na Bigman kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Kagera Sugar itachuana na Gunners katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera huku Stand United ikicheza na Geita Gold katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

TMA na Barberian zitacheza katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha huku Transit Camp ikichuana na Mbuni kwenye uwanja wa TFF Kigamboni.

MBEYA CITY, YOUNG AFRICANS, SINGIDA ZATAMBA LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo mitatu iliyokuwa na ushindani mkubwa, huku vinara Young Africans wakiendelea kuimarisha nafasi yao kileleni mwa msimamo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Kiungo Mudathir Yahya aliwatanguliza ‘wananchi’ mbele dakika ya 29 kabla ya beki Bakari Mwamnyeto kufunga bao la pili dakika ya 90+1 na kuhakikisha mabingwa watetezi wanaondoka na alama tatu muhimu.

Ushindi huo umeifanya Young Africans kuendelea kushikilia nafasi ya kwanza kwa alama 63.

Katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya City ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwa bao pekee la mchezo lilifungwa na Adili Buha dakika ya 35 kwa mkwaju wa penati huku matokeo hayo yakiipa Mbeya City alama muhimu katika harakati za kujinasua kutoka maeneo ya hatari.

Mchezo mwingine uliopigwa jijini Dar es Salaam uliwakutanisha JKT Tanzania na Singida Black Stars, ambapo wageni waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Horso Muaku aliifungia Singida Black Stars bao la kwanza dakika ya 23 kabla ya Emmanuel Keyekeh kuongeza la pili dakika ya 75 na JKT Tanzania wakipata bao la kufutia machozi kupitia Valentino Mashaka dakika ya 80.

Ushindi huo umeifanya Singida Black Stars kuendelea kusalia nafasi ya nne kwenye msimamo huku JKT Tanzania wakibaki nafasi ya sita.

Matokeo ya jana yameongeza ushindani katika mbio za nafasi za juu pamoja na vita ya timu zinazopambana kubaki Ligi Kuu.

MIKOA MITATU KINAPIGWA LEO LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo, kwa michezo mitatu muhimu ambayo inaweza kuathiri mbio za ubingwa, nafasi za juu kwenye msimamo pamoja na vita ya kujiokoa dhidi ya kushuka daraja.

Mbeya City na Mtibwa Sugar watacheza Saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku ‘wababe’ hao wa ‘Green city’ wakisaka alama muhimu ili kujiimarisha kwenye vita ya kuendelea kusalia Ligi Kuu.

Mashujaa na Young Africans watakutana Saa 10:15 alasiri kwenye dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Vinara wa ligi Young Africans watalenga kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo huku Mashujaa nao wakihitaji matokeo mazuri mbele ya mashabiki wao ili kuboresha nafasi yao kwenye jedwali.

JKT Tanzania na Singida Black Stars watakutana Saa 12:30 jioni kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam.

Huu unatarajiwa kuwa mchezo wa ushindani mkubwa kati ya timu mbili zinazowania nafasi za juu.

JKT Tanzania wanaingia wakiwa nafasi ya sita, huku Singida Black Stars wakishika nafasi ya nne, hivyo ushindi utakuwa muhimu kwa kila upande katika mbio za kumaliza msimu ndani ya nafasi za juu.

Mashujaa, Mbeya City na Mtibwa Sugar wanapatikana katika nusu ya chini ya msimamo na wanaendelea kupambana kujinusuru dhidi ya kushuka daraja.

Michezo ya leo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikiwa na malengo tofauti na baadhi zikisaka ubingwa, nyingine nafasi za juu, na nyingine zikihitaji pointi muhimu ili kuendelea kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC.

AZAM YATAKATA ARUSHA, KMC IKISHUKA DARAJA.

TIMU ya Azam imetakata katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuvuna alama tatu na mabao mawili baada ya kuichapa timu ya Fountain Gate katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid .

Mchezo huo uliopigwa saa kumi jioni ulianza kwa timu zote kushambuliana kwani kila timu ilizitaka alama tatu muhimu.

Ilimchukua dakika 36 mshambuliaji wa Azam Jean Ngita kufungua ukurasa wa mabao ambapo timu hiyo ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa 0-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Fountain wakitaka kusawazisha ambapo dakika ya 64 mshambuliaji wa Azam Jephte Kitambala aliongeza bao la pili kwa timu yake na hadi mchezo huo unatamatika matokeo ni 0-2.

Mkwakwani Tanga wenyeji Coastal Union waliikaribisha Namungo
ambapo timu zote zilihitaji alama ili kujiweka katika nafasi nzuri na dakika 37 ziliwatosha Coastal kupata bao la kuongoza kupitia mchezaji Robert Savilla kabla ya timu ya Namungo kusawazisha kipindi cha pili dakika ya 62 kupitia mchezaji Geofrey Luzindaze hivyo mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.

Saa mbili usiku KMC ilikuwa na kibarua kizito cha kuikaribisha timu ya TRA katika uwanja wa KMC Complex mchezo ulioanza kwa KMC kuonekana ikizitaka alama tatu muhimu hata hivyo haikuweza kufanikiwa baada ya kukubali kipigo cha 0-1z

Ilimchuka dakika 12 beki wa TRA Chamou Karaboue kuipatia bao timu yake ambalo limebaki kuwa bao pekee kufungwa katika mchezo huo mpaka dakika 90 zilipotamatika na hivyo timu ya KMC kushuka daraja kwani hata ikishinda michezo yake iliyosalia haitaweza kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja.