Category: STORY

LAKE TANGANYIKA KUWAKA MOTO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kwa mchezo kati ya Mashujaa itakayokuwa mwenyeji wa Simba saa 10:00 alasiri.

Mashujaa iliyopoteza mchezo mmoja pekee msimu huu sawa na Simba inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Fountain Gate ugenini.

Mashujaa imeshinda michezo mitatu na kutoa sare minne hadi sasa inakutana na Simba iliyoshinda michezo sita ya Ligi Kuu ya NBC na kutoka sare mchezo mmoja pekee.

Simba inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kuishusha Singida Black Stars na kupanda hadi nafasi ya pili kwa tofauti ya wastani wa mabao.

YANGA YAKWEA KILELENI KWENYE MSIMAMO WA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Yanga imeendeleza ubabe msimu huu baada ya kushinda mchezo wa nane mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC kwa bao moja ugenini dhidi Singida Black Stars.

Bao pekee la Yanga lilifunga na Pacome Zouzoua na kufanya Singida kupoteza mchezo wake wa kwanza msimu huu.

Yanga imecheza mchezo wake wa nane msimu huu bila kuruhusu bao lolote huku ikiwa imefunga jumla ya mabao 13.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha jumla ya alama 24 na kuongoza Ligi Kuu ya NBC baada ya kucheza michezo nane.

Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa kwenye uwanja wa KMC, Dar kati ya KMC na Namungo

COASTAL YATAMBA, KENGOLD, DODOMA HAKUNA MBABE

 

LIGI Kuu ya NBC jana iliendelea katika viwanja vya Sokoine jijini Mbeya katika mchezo uliozikutanisha KenGold na Dodoma Jiji na kwenye uwanja Sheikh Amri Abeid Arusha Coastal Union wakiwakaribisha Kagera Sugar michezo iliyopigwa saa 10:00 alasiri.

Katika michezo hiyo KenGold iligawana alama na timu ya Dodoma Jiji baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 yalifungwa na Mishamo Daud kwa upande wa KenGold huku Dissan Galiwango na Zidane Sereri wakifunga mabao ya Dodoma Jiji.

Kwa upande wa Coastal Union Kiungo Mshambuliaji Charles Semfuko alifanikiwa kufunga bao dakika ya 85 ya mchezo huo ambao uliisha kwa Coastal kuibuka washindi na kukusanya alama zote tatu za mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo Visiwani Zanzibar timu ya Singida Black Star watawakaribisha Yanga katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja saa 2:30 usiku.

VITA YA KITAMBI NA GAMONDI NANI KUKAA KILELENI?

Ligi Kuu ya NBC kesho itaendelea Zanzibar kwa mchezo namba 40 utakaozikutanisha timu za Singida Black Star na Yanga utakaochezwa saa 2:30 usiku katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Katika mchezo huo timu mbili zinazoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC zitakutana, Singida Black Star iliyocheza michezo nane ikiongoza msimamo kwa kuwa na alama 22, ikifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zao ‘kutikiswa’ mara tatu huku ikiwa imeshinda mechi saba na kupata  sare moja.

Kwa upande wa Yanga inayoshikilia nafasi ya pili katika msimamo huo imecheza michezo saba imeshinda mechi zote kwa kufunga mabao 12 na kuvuna alama zote 21 huku ikiwa haijaruhusu nyavu zao ‘kutikiswa’ na wapinzani wao.

Ikumbukwe kuwa utakuwa ni mchezo huo utaamua nani kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kati ya Singida ikiongozwa na kocha wake Dennis Kitambi ama Yanga chini ya Miguel Gamondi.

NAMUNGO YAIZAMISHA PAMBA, FOUNTAIN GATE, MASHUJAA HAKUNA MBABE.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea na kushuhudia michezo miwili ikichezwa katika viwanja vya Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara na Majaliwa mkoani Lindi.

Mchezo wa kwanza uliochezwa majira ya jioni timu ya Fountain Gate iliikaribisha timu ya Mashujaa na kushuhudia sare ya mabao 2-2.

Mabao ya Fountain Gate yalifungwa na Nicholas Gyan na Salum Kihimbwa huku magoli ya Mashujaa yakifungwa na Seif Karihe na Hassan Ali.

Mchezo wa pili uliochezwa Uwanja wa Majaliwa Lindi timu ya Namungo waliwakaribisha Pamba Jiji ya Mwanza katika mchezo ambao wenyeji Namungo walifanikiwa kubaki na alama tatu muhimu za mchezo huo baada ya mchezaji wao Ibrahim Abdallah kufunga goli pekee dakika ya 14 ya mchezo huo.

Ligi ya NBC leo itaendelea kwa michezo miwili ambapo KenGold watawakaribisha Dodoma Jiji katika Uwanja wa Sokoine Mbeya na Coastal Union watawakaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sheikhe Amri Abeid jijini Arusha huku michezo yote ikitarajiwa kuanza saa 10:00 alasiri.