Category: STORY

SIMBA KUWAKARIBISHA NAMUNGO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC iliyo nafasi ya 6 kwa ubora barani Afrika leo inaendelea kwa michezo mitatu itakayochezwa jijini Dar es Salaam na mkoani Singida.

Mchezo wa kwanza utachezwa majira ya saa nane mchana katika Uwanja wa Liti mkoani Singida, ukizikutanisha timu za Singida Black Star na Fountain Gate.

Fountain itawakosa washambuliaji wake wawili muhimu Seleman Mwalimu na Wiliam Edgar ambao wameitwa timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya michezo ya kufuzu CHAN 2024 dhidi ya Sudan .

Mchezo wa pili utachezwa saa 10 jioni katika Uwanja wa KMC Dar es Salaam ambapo timu ya Simba iliyopo nafasi ya 3 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 16 itaikaribisha timu ya Namungo kutoka Ruangwa iliyo nafasi ya 13 ikiwa na alama 6.

Mchezo wa tatu utachezwa majira ya saa 1 jioni Azam inayoshika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 15 itakuwa mwenyeji wa timu ya Ken Gold kutokea Mbeya inayoshika nafasi ya 16 kwenye msimamo ikiwa na alama 4.

TABORA YAIZAMISHA PAMBA JIJI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Tabora United imefanikiwa kuifunga timu ya Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa jana kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

Tabora walipata bao dakika ya 77 ya mchezo huo kupitia kiungo wake Morice Chukwu kwa mkwaju wa penati ambaye alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuiwezesha timu yake kupata pointi 3 muhimu.

Pointi hizo zilifanikiwa kuipeleka Tabora nafasi ya 7 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na pointi 11 nyuma ya Mashujaa yenye pointi 12.

Ligi Kuu itaendelea kesho kwa michezo mitatu Singida Black Star dhidi ya Fountain Gate katika Uwanja wa Liti mkoani Singida ,Simba dhidi ya Namungo katika Uwanja wa KMC Dar es Salaam na Azam wataikaribisha Ken Gold katika Uwanja wa Azam Complex.

YANGA YAENDELEZA UBABE LIGI KUU NBC.

Timu ya Yanga imeendeleza ubabe Ligi Kuu ya NBC kwa kucheza michezo sita bila kupoteza hivyo kufikisha alama 18 na kuwa nafasi ya pili katika msimamo ikiwa nyuma ya Singida Black Stars kwa alama moja.

Yanga jana iliifunga timu ya JKT Tanzania kwa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa jana uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga yalifungwa na wachezaji Pacome Zouzoua ambaye pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kiungo Mshambuliaji wa timu hiyo Clatous Chama ambae pia alitoa asisti ya goli ya goli la kwanza.

Aidha katika mchezo huo kipa wa JKT Tanzania,Dennis Richard alipewa kadi nyekundu baada ya kuucheza mpira kwa mikono akiwa nje ya box hivyo kuifanya JKT kufanya mabadiliko kwa kumtoa Hassan Kapalata na kumuingiza mlinda mlango Omary Gonzo .

Ligi kuu ya NBC inaendelea leo kwa mchezo mmoja utakaochezwa mkoani Tabora ikizikutanisha timu za Tabora United na Pamba Jiji kutoka jijini Mwanza.

SIMBA YAJIPATA LIGI KUU YA NBC.

Timu ya Simba imerudi kwenye njia ya ushindi kwa kuifunga Prisons bao moja baada ya kudondosha pointi 5 katika michezo miwili ya Ligi Kuu ya NBC kwa kutoa sare na timu ya Coastal Union na kufungwa na Yanga katika mchezo wa Derby ya Kariakoo .

Simba jana ikiwa jijini Mbeya ilifanikiwa kuifunga timu ya Prisons dakika ya tano ya mchezo huo lililofungwa na mlinzi wa kati wa Simba Che Malone baada ya kipa wa Prisons Musa Mbisa kushindwa kuudaka mpira wa faulo.

Baada ya mchezo huo simba ilifikisha alama 16 sawa na timu ya Fountain Gate huku Simba ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu tofauti ya mabao ya kufungwa Simba ikiruhusu mabao 3 na Fountain Gate wakiruhusu mabao 13.

PRISONS, YANGA KUJARIBU BAHATI LEO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo kwa michezo miwili ambapo timu ya Prisons inaikaribisha Simba kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri.

Prisons inakuwa mwenyeji wa Simba huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopoita dhidi ya Azam kwenye uwanja wa nyumbani kwa mabao 0-2.

Simba inakwenda ugenini ikiwa ni baada ya kupoteza mchezo uliopita kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya Yanga kwa bao moja.

Mchezo wa mwisho utachezwa uwanja wa Azam Complex, Dar kati ya Yanga itakayoikaribisha JKT Tanzania saa 1:00 usiku.

JKT iliyoshinda mchezo uliopita dhidi ya Tabora United kwa mabao 4-2 inakutana na Yanga ambayo haijapoteza mchezo wowote wala kuruhusu bao hadi sasa kwenye msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC.