Category: STORY

MWALIMU HASHIKIKI LIGI KUU YA NBC

KINARA wa mabao ndani ya Ligi Kuu ya NBC Selemani Mwalimu wa timu ya Fountain Gate amendelea kuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani baada ya jana kufunga na kuisaidia timu yake kushinda mchezo wa tano msimu huu.

Fountain iliifunga KMC ya Dar mabao 3-1 kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani manyara huku mchezo huo ukimalizika kwa nyota wa KMC Ibrahim Elias kuonyeshwa kadi nyekundu ikiwa ni dakika tisa baada ya kuingia uwanjani.

Mwalimu amefikisha jumla ya mabao sita ndani ya michezo nane aliyocheza huku pia akitoa pasi moja iliyozaa bao kwa Edgar William hapo jana.

Fountain ndio timu iliyofunga mabao mengi hadi sasa ikifikisha mabao 17 na kufuatiwa na Simba yenye mabao 12.

Mchezo mwingine ulichezwa uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na kushuhudia timu ya Mashujaa ikiifunga KenGold mabao 3-0 na kukwea hadi nafasi ya sita baada ya kufikisha alama 12.

YANGA YAENDELEZA UBABE LIGI KUU YA NBC.

Timu ya Yanga imeendeleza ubabe inapocheza dhidi ya Simba baada ya kushinda kwa bao moja kwenye mchezo uliozikutanisha timu hizo kwenye uwanja wa Mkapa, Dar.

Bao la Yanga limepatikana baada ya mchezaji Kelvin Kijili kushindwa kuokoa mpira na kujifunga hivyo kufanya Yanga kushinda mchezo wa tano mfululizo msimu huu.

Hadi sasa Yanga ndio timu pekee ambayo haijaruhusu bao huku ikifunga mabao tisa na kuwa timu kinara wa wastani mzuri wa mabao sawa na timu ya Simba.

Kwa Matokeo hayo Yanga inapanda hadi nafasi ya pili ya msimamo ikikusanya jumla ya alama 15 nyuma ya kinara Singida Black Stars yenye alama 16 baada ya michezo sita.

KUFA AU KUPONA ‘KARIAKOO DERBY’ LIGI KUU YA NBC LEO.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaokutanisha ‘Miamba’ wa Tanzania kwenye soka timu ya Simba itakayokuwa nyumbani kuikaribusha Yanga kwenye uwanja wa Mkapa, Dar saa 11:00 jioni.

Huu ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu kwa timu hizo huku Simba ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga kwa mabao 2-1.

Simba inaingia kwenye mchezo huu ikiwa imetoka sare ya mabao mawili kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Timu ya Yanga itaingia kucheza ugenini leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuahinda mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya NBC kwa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Pamba.

Yanga haijapoteza mchezo wowote wala kuruhusu bao kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu hadi sasa huku ikiwa na rekodi nzuri ya kushinda michezo yote iliyokutana na Simba msimu uliopita.

MTIBWA INA JAMBO LAKE NBC CHAMPIONSHIP.

 

Mtibwa Sugar imeendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC 2024/2025 baada ya ushindi wa bao moja dhidi ya Songea United Leo kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro.

Mtibwa Sugar imefikisha alama 12 kwenye michezo minne iliyocheza hadi sasa ikifunga mabao Saba bila kuruhusu bao lolote.

Michezo mingine miwili ilichezwa leo, Mapema saa 8:00 Mchana Mbeya kwanza iliialika Green Warriors katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara na Kumalizika kwa Mbeya Kwanza kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mchezo mwingine ulizikutanisha Mbuni na Biashara United na kumalizika kwa sare ya bao 1, mchezo huo ulichezwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

NBC CHAMPIONSHIP KINAWAKA LEO.

 

LIGI ya NBC ya Championship mzunguko wa Nne unaanza Leo kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa ya Mtwara, Arusha na Morogoro.

Mkoani Mtwara Mbeya Kwanza itakuwa mwenyeji wa Green Warriors kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona kuanzia saa 8:00 Mchana.

Mbuni FC ya Arusha itaialika Biashara United ya Mara kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa mwisho kwa leo utazikutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya Songea United kuanzia saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Hadi hivi sasa Mtibwa Sugar inaongoza msimamo wa Ligi ya NBC ya Championship ikiwa na alama tisa sawa na Songea United na Stand United zikitofautiana magoli ya kufunga na kufungwa.