Category: STORY

YANGA, SIMBA ZAENDELEZA REKODI LIGI KUU YA NBC.

 

TIMU za Yanga na Simba zinashikilia rekodi za kipekee hadi hivi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu 2023/2024 zinapocheza viwanja vya nyumbani na ugenini kwa timu hizi.

Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote wa nyumbani kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu katika michezo 10 ya nyumbani Kati ya 20 iliyocheza mpaka sasa.

Simba inashikilia rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu 2023/24 kwenye uwanja wa ugenini kwenye michezo 9 iliyocheza ugenini Kati ya 19.

Timu zote mbili Simba na Yanga zimepoteza michezo miwili kila mmoja ambapo Yanga ilipoteza dhidi ya Ihefu kwa mabao 2-1 Highland Estates mkoani Mbeya na 2-1 pia dhidi ya Azam FC kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa huku Simba ikipoteza dhidi ya Yanga 5-1 uwanja wa Benjamin Mkapa na 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons mkoani Morogoro.

KIPRE JR KINARA WA PASI ZA MABAO LIGI KUU YA NBC.

 

JUMLA ya mabao 364 yameshafungwa hadi hivi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC huku jumla ya wachezaji 137 wakihusika kwenye kuyatengeneza mabao hayo.

Kipre JR ndiye kinara wa kutoa pasi za mabao akifanya hivyo mara nane kwenye mabao 47 ya Azam FC msimu huu.

Kouassi Yao na Stephane Aziz Ki wanafuatia kila mmoja akitoa pasi saba za mabao na kuwa na jumla ya pasi 14 za mabao kwenye mabao 49 ya Yanga msimu huu.

Clatous Chama wa Simba, Feisal Salum wa Azam, Impiri Mbombo wa Tabora, Rahimu Shomari na Awesu Awesu wa KMC wanafuatia kila mmoja akitoa pasi 5 za mabao.

AZİZ KI, FEITOTO WAKALI WA MABAO LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC imesimama kwa muda kupisha kalenda ya FIFA ya michezo ya kimataifa ya kirafiki kwa timu za taifa ambapo Tanzania Itacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Bulgaria na Mongolia.

Hadi Ligi hiyo inasimama jumla ya mabao 364 yamefungwa huku Yanga ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi (49).

Stephane Ki Aziz wa Yanga na Feisal Salum wa Azam ndiyo wanaoongoza kwa upachikaji wa mabao kila mmoja akifunga mabao 13 yakiwemo mabao matatu “Hat trick” kwenye mchezo mmoja, Ki Aziz akifunga dhidi ya Azam na Feisal Salum akifunga dhidi ya Tabora United.

Waziri Junior wa KMC anafuatia akifunga mabao 11 kwenye mabao 23 ya timu yake msimu huu yakiwemo mabao matatu “hat trick” dhidi ya Tabora United.

Maxi Nzengeli wa Yanga anakamilisha idadi ya wakali wanne wa juu kwenye upachikaji mabao akifunga mabao 9.

Kagera Sugar ndiyo timu iliyofunga mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu ya NBC ikifunga mabao 13 kwenye michezo 21.

NANI KUIBUKA MBABE ‘DAR ES SALAAM DERBY’ LEO?

 

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo kwa mchezo mmoja wa Ligi Kuu ya NBC Kati ya Azam na Yanga saa 2:30 usiku kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Azam inaingia kwenye mchezo huu unaotambulika kama ‘Dar es Salaam Derby’ ikiwa nafasi ya tatu na alama 44 baada ya michezo 20 huku Yanga ikiwa nafasi ya kwanza na alama 52 kwenye michezo 19.

Azam inahitaji kushinda mchezo huu ili kupunguza tofauti ya alama na Yanga na kuendeleza mbio za ubingwa huku Yanga ikihitaji kujikita kileleni mwa msimamo na kuongeza utofauti wa alama na timu zinazofuata.

Yanga inaongoza kwa ufungaji wa mabao ikifunga 48 kwenye michezo 19 na kuruhusu mabao tisa pekee huku Azam ikifuata kwa upachikaji wa mabao ikifunga 45 na kuruhusu 15.

Mchezo huu utakuwa wa mwisho kupisha michezo ya kalenda ya kimataifa ya FIFA kwa timu za taifa kabla ya kurejea tena Aprili 12, 2024.

MZUNGUKO WA 25 NBC CHAMPIONSHIP KUANZA LEO.

 

LIGI ya NBC Championship inaendelea leo kwa michezo mitatu ya mzunguko wa 25 kupigwa leo.

Mkoani Mtwara Mbeya Kwanza itakuwa mwenyeji wa Stand United saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona huku Mbeya Kwanza ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na alama 47 kwenye michezo 24.

Saa 10:00 alasiri Pamba itakuwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.

Pamba imejikusanyia alama 51 kwenye michezo 24 ikiwa nafasi ya pili huku Mbeya City ikiwa nafasi ya saba na alama 38.

Mchezo wa mwisho utazikutanisha Polisi Tanzania dhidi ya TMA kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha saa 10:00 alasiri.

Michezo hii ya Ligi ya NBC Championship itaoneshwa mubashara kupitia chaneli ya TV3 na ST Bongo kwenye king’amuzi cha Startimes.