Category: STORY

ISAMUHYO, KAITABA HAKUNA MBABE LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI KUU ya NBC imeendelea leo Machi 13 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye viwanja viwili tofauti.

Mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri ulizikutanisha JKT Tanzania dhidi ya Tanzania Prisons na kumalizika kwa sare ya bao 1.

Bao la JKT Tanzania lilifungwa dakika ya 40 na Daniel Lyanga huku lile la Tanzania Prisons likifungwa na Samson Mbangula dakika ya 46 ya mchezo.

Kwa matokeo hayo JKT Tanzania inafikisha alama 20 ikiendelea kusalia nafasi ya 15 kwenye msimamo huku Tanzania Prisons ikifikisha alama 28 ikipanda hadi nafasi ya nne.

Mchezo wa mwisho ulizikutanisha Kagera Sugar dhidi ya Mtibwa Sugar saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera na kumalizika kwa suluhu, kwa matokeo haya Kagera inasogea hadi nafasi ya saba ikifikisha alama 24 huku Mtibwa Sugar ikiendelea kusalia nafasi ya mwisho kwenye msimamo.

VITA YA KISASI LIGI KUU YA NBC LEO.

 

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Machi 11 kwa mchezo mmoja kuchezwa Kati ya timu ya Yanga na Ihefu kwenye uwanja wa Azam Complex mkoani Dar es salaam.

Yanga inaingia kwenye mchezo Huu ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwenye mchezo wa mwisho timu hizi zilipokutana msimu huu kwa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Highland Estates mkoani Mbeya.

Ihefu ndiyo timu pekee iliyoifunga Yanga kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu huku Yanga ikiwa haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa baada ya kipigo hicho.

Yanga inashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 46 baada ya michezo 17 huku Ihefu ikiwa nafasi ya nane na alama 23 baada ya kucheza michezo 19.

SIMBA KUJIULIZA KWA COASTAL, MECHI 3 KUPIGWA LEO.

 

Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo Machi 9 kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Mkoani Morogoro Mtibwa Sugar itaialika Tanzania Prisons saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Manungu huku timu zote mbili zikipata ushindi kwenye michezo yao iliyopita Mtibwa ikiifunga Singida Fountain Gate huku Tanzania Prisons ikiifunga Simba.

Saa 12:00 jioni Coastal Union itaialika Simba katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

Mchezo wa kwanza timu hizo zilipokutana kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es salaam Coastal Union ilipoteza mabao 3-0.

Mchezo wa Mwisho kwa leo utazikutanisha Dodoma Jiji dhidi ya Geita Gold saa 2:15 usiku kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma huku Geita Gold ikiwa nafasi ya 15 moja kutoka mwisho na alama 18 huku Dodoma Jiji ikiwa nafasi ya 9 na alama 23 na kuufanya mchezo kuwa wa ushindani.

YANGA KUREJEA KILELENI LEO ?

 

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Machi 8 kwa mchezo mmoja Kati ya Namungo na Yanga saa 12:00 jioni kwenye uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Ikiwa Yanga itapata matokeo ya Sare au Ushindi itarejea moja kwa moja kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC nafasi ambayo inashikiliwa na Azam kwa sasa iliyopata sare kwenye mchezo wake wa mwisho dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Ushindi katika mchezo huu unaweza kuipeleka timu ya Namungo hadi nafasi ya nne kwenye msimamo kwani itafikisha alama 27 na kuizidi Coastal Union katika tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

HAWA HAPA WAKALI WA MECHI ZA NYUMBANI NBC CHAMPIONSHIP.

 

JUMLA ya michezo 184 ya Ligi ya NBC Championship imechezwa kwenye viwanja mbalimbali kwenye mikoa 11 tofauti ikihusisha michezo ya nyumbani na ugenini kwa kila timu shiriki.

Biashara United inaongoza msimamo kwa timu zilizoshinda mechi nyingi nyumbani ikifanya hivyo mara 10 kwenye michezo 12 iliyocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani Karume mkoani Mara.

Mbeya Kwanza, Mbuni na Mbeya City zinafuata kila timu ikishinda michezo nane zikitofautiana kwenye michezo ya kucheza ambayo Mbeya kwanza imecheza michezo 10, Mbuni ikicheza 11 na Mbeya City ikicheza 12.

Ruvu Shooting ndiyo timu iliyoshinda michezo michache zaidi nyumbani ikishinda mchezo mmoja pekee.