HATIMAYE timu ya Gunners ya mkoani Dodoma imeungana na Hausung ya mkoani Njombe kupanda moja kwa moja Ligi ya Championship ya NBC kwa msimu unaofuata wa 2025/2026 baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mapinduzi na kufikisha alama 35 hivyo kuongoza msimamo wa First League kundi B.
Baada ya kutamatika kwa Ligi hiyo kinachofuata sasa ni mchezo wa kutafuta Bingwa wa First League kwa msimu wa 2024/2025 ambapo kinara kundi A Hausung atakutana na kinara wa kundi B Gunners sambamba na michezo ya mtoano (PlayOff).
Wakati huo huo timu za African Lyon kutoka kundi A na Ruvu Shooting kutoka Kundi B zimeshuka daraja baada ya kumaliza nafasi za mwisho kwenye makundi yao.
Katika hatua nyengine Ruvu Shooting imekumbana na adhabu ya kushushwa daraja na kufungiwa kushiriki Ligi kwa misimu miwili baada ya ombi lao la kujitoa katika Ligi ya First League kwa kile walichoeleza kuwa ni kushindwa kumudu gharama za uendeshaji kulikosababisha kuondokewa na wachezaji wao kadhaa kukubaliwa na Bodi ya Ligi.
 
					