MZUNGUKO wa 26 wa Ligi ya Championship ya NBC unaendelea tena leo kwa michezo mitatu na itakayorushwa mubashara kupitia chaneli za TV3 na ST BONGO ndani ya king’amuzi cha StarTimes.
Mapema saa 8:00 mchana Polisi Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mbuni kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.
Mchezo unaosubiriwa kwa hamu leo ni kati ya Ken Gold na Pamba utakaopigwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.
Mchezo huu unatazamwa sana kutokana na nafasi ya kila timu kwenye msimamo Ken Gold ikiwa nafasi ya kwanza na Pamba ikiwa nafasi ya pili huku timu hizo zikipishana kwa alama tano.
Ken Gold inahitaji ushindi kwenye mchezo Huu ili kuzidi kujikita kileleni na kuendelea kushikilia rekodi yake ya kutopoteza mchezo wowote nyumbani huku Pamba ikihitaji ushindi ili kupunguza utofauti wa alama uliopo.
Mchezo wa mwisho leo utapigwa saa 10:00 alasiri ukizikutanisha Copco dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.