MZUNGUKO wa 27 Ligi ya NBC Championship unahitimishwa leo kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Shinyanga na Morogoro.
Mkoani Shinyanga Stand United itaialika Green Warriors kwenye uwanja wa CCM Kambarage saa 8:00 mchana.
Stand United na Green Warriors zinapambana kutoka katika mstari wa kucheza mtoano wa kushuka daraja hivyo kufanya mchezo wa leo kuwa wa muhimu kwa pamde zote mbili.
Stand United ipo nafasi ya 11 na alama 30 kwenye michezo 26 iliyocheza huku Green Warriors ikiwa nafasi ya 12 na alama 27 kwenye michezo 26.
Mkoani Morogoro Transit Camp itaialika Biashara United kwenye uwanja wa Jamhuri saa 10:00 alasiri.
Transit Camp ipo nafasi mbaya kwenye msimamo ikiwa nafasi ya 13 na alama zake 23 kwenye michezo 26 huku Biashara ikihitaji ushindi ili kuzidi kuweka hai mbio za kuwania kupanda Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 ikiwa na alama 53 kwenye michezo 26 mpaka sasa.