Mzunguko wa Ligi Kuu ya NBC uliendelea kwa michezo mitatu iliyotoa burudani, ushindani mkubwa na matokeo yenye athari kwenye msimamo wa ligi hiyo huku Young Africans ikiendelea kuonyesha ubora wake kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 na kuwa timu pekee iliyopata matokeo ya ushindi kwa siku ya jana.
Katika mchezo uliovuta hisia za mashabiki wengi, Young Africans iliitandika Tanzania Prisons mabao 3-0 katika mechi ambayo mabingwa hao watetezi walionyesha tofauti mkubwa wa ubora kuanzia dakika za kwanza hadi mwisho.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao Young Africans ilirejea kwa kasi kubwa kipindi cha pili na kufungua pazia dakika ya 50 kupitia kwa Allan Okello raia wa Uganda aliyemalizia vizuri krosi ya Israh Mwenda.
Dakika ya 68 Mudathir Yahya aliandika bao la pili kabla ya Pacome Zouzoua kuweka msumari wa mwisho dakika ya 86 na kufanya matokeo kuwa 3-0 huku golikipa wa Young Africans Abutwalib Mshery akiondoka bila kuruhusu bao.
Ushindi huo unaendelea kuipa Yanga nguvu kubwa katika mbio za ubingwa ikifikisha alama 41 huku ukiweka presha kwa wapinzani wao wa karibu kwenye kilele cha msimamo.
Katika mchezo mwingine uliokuwa na ushindani mkali, Namungo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na JKT Tanzania kwenye mechi iliyokuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya matokeo.
Namungo walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Jacob Masawe dakika ya 25, kabla ya JKT Tanzania kusawazisha kupitia Salehe Karabaka dakika ya 66.
Namungo walionekana kurudi mchezoni tena baada ya Herbert Lukindo kufunga bao la pili dakika ya 63 lakini JKT Tanzania hawakukata tamaa na walipata bao muhimu la kusawazisha kupitia Valentino Mashaka dakika ya 90+4 bao lililozima furaha ya wenyeji na kuwafanya wagawane alama muhimu.
Katika mechi ya tatu timu ya Mashujaa na Pamba Jiji walitoka sare tasa ya 0-0 matokeo ambayo yanaonyesha jinsi timu zote zilivyokuwa na tahadhari kubwa zaidi kuliko hatari langoni.
Licha ya kila upande kupata nafasi chache za kufunga umakini wa safu za ulinzi na makipa ulifanya mchezo huo kumalizika bila mshindi.
Kwa ujumla, mechi za jana zimeendelea kuongeza joto la Ligi Kuu ya NBC hasa katika mbio za ubingwa na vita ya kujiokoa mkiani.
Ushindi wa Young Africans unaendelea kuwatengenezea mazingira mazuri ya kutetea taji lao, wakati sare za Namungo na Mashujaa zinaacha maswali kwa timu hizo kuhusu uwezo wao wa kutumia vyema mechi za nyumbani.
Kadri ligi inavyozidi kuelekea mwisho, kila alama imekuwa ya thamani kubwa, na matokeo ya jana ni ishara kuwa ushindani bado ni mkali sana katika kila nafasi ya msimamo.
Ligi inazidi kuwa kwenye kiwango cha juu lakini kwa timu kubwa clab ya young Africans inazidi kuonyesha ukubwa wa ligi yetu na kuifanya premier league ni bora barani Afrika hata duniani lakini timu zote zinatakiwa kuonyesha upinzani kama tra ya tabora mm Alan mussa kutoka Shinyanga,