TIMU ya Simba imefanikiwa kufuzu fainali ya Ngao ya Jamii kwa ushindi wa penati 4-2 dhidi ya Singida Big Stars baada ya kumalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90.
Simba itakutana na Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii kwa mara ya tatu mfululizo huku ikiwa imefungwa katika mara zote mbili zilizopita.
Penati zilizofungwa na Luis Miquisone, Saidi Ntibazonkinza, Mzamiru Yassin na Moses Phiri zilitosha kuipeleka Simba fainali na kuifanya Singida kukutana na Azam katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.
Shindano hilo litatamatika Agosti 13 kwa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya Azam na Singida huku mchezo wa mwisho ukiwa kati ya Simba na Yanga kutafuta bingwa wa Ngao ya Jamii msimu wa 2023/24.