MSHAMBULIAJI wa Young Africans raia wa Uganda Allan Okello ameendelea kuonyesha ubora wake katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 baada ya kuongoza kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwa kutumia mguu wa kushoto.
Nyota huyo anaongoza kwa mabao 10 ya mguu wa kushoto akithibitisha uwezo wake mkubwa wa kumalizia mashambulizi na kuwa silaha muhimu kwa Young Africans katika harakati za kutetea ubingwa wao.
Nyuma yake wapo nyota wawili waliolingana kwa mabao sita kila mmoja ambao ni Libasse Guèye wa Simba na Salehe Karabaka wa JKT waliotoa mchango mkubwa katika safu za ushambuliaji za timu zao.
Katika nafasi ya nne ni Fredrick Magata wa Mtibwa Sugar mwenye mabao matano ya mguu wa kushoto huku Methew Tegisi wa Pamba Jiji akifuatia kwa mabao manne.
Wachezaji wengine waliopo kwenye orodha hiyo ni Selemani Mwalimu, Clatous Chama wa Simba na Prince Dube wa Young africans waliofunga mabao manne kwa kutumia mguu wao wa kushoto kila mmoja.
Hii inaonyesha umuhimu wa wachezaji wenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto kwa ufanisi huku Allan Okello akiendelea kuwa kinara na mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa zaidi kwa ‘wananchi’ katika mashindano ya Ligi Kuu ya NBC.