LIGI Kuu ya NBC imeendelea mkoani Mbeya ambapo timu ya Tanzania Prisons iliikaribisha timu ya Coastal Union katika uwanja wa Sokoine na kukusanya alama zote tatu baada ya ushindi wa 2-1.
Mchezo huo ulianza saa 10:00 alasiri timu zote zilionyesha ari ya kupambania alama tatu muhimu ili kuweza kujiweka katika mazingira ya kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.
Iliwachukua dakika 27 timu ya Tanzania Prisons kufungua ukurasa wa mabao kupitia mchezaji wao Ezekia Mwashilindi hivyo kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa 1-0.
Kipindi cha pili kilianza ambapo Coastal Union walionekana kuliandama zaidi lango la Prisons hata hivyo juhudi zao zilizimwa na mchezaji Beno Ngasa aliyeongeza bao la pili kwa timu yake dakika ya 74.
Dakika ya 89 Coastal Union ilipata bao la kufutia machozi kupitia mchezaji wao Bakari Msimu hivyo mchezo kutamatika kwa matokeo ya 2-1.
Tanzania Prisons ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imevuna alama 30 katika michezo 28 huku Coastal Union ikiwa nafasi ya 9 na alama 31 katika michezo 28 ya Ligi Kuu msimu wa 2024/2025.