SIMBA YAREJEA KILELENI KIBABE,TABORA UNITED HAISHIKIKI LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo mitatu iliyochezwa katika viwanja mbalimbali nchini kuanzia saa kumi alasiri na mchezo wa mwisho ukichezwa saa moja jioni.

Simba waliwakaribisha timu ya Tanzania Prisons katika uwanja wa KMC Complex majira ya saa kumi alasiri ambapo mchezo ulianza timu zote zikicheza kwa tahadhari kubwa hususan Simba .

Dakika ya 29 Jean Ahoua alifungua ukurasa wa mabao  kwa timu yake akipokea pasi ya upendo kutoka kwa beki wa timu hiyo Shomari Kapombe,winga wa timu hiyo Ellie Mpanzu nae aliongeza bao la pili dakika ya 44 huku Ladack akifunga bao la tatu na kuwafanya Simba kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele kwa mabao 3-0.

Kipindi cha pili kilianza ambapo timu ya Tanzania Prisons walifanya mabadiliko na kuamua kucheza kwa kujilinda zaidi ambapo waliweza kufanikiwa lengo lao kutoruhusu bao lolote kipindi cha pili hivyo mchezo kuisha kwa Simba kufanikiwa kubeba alama zote tatu hivyo kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Beki wa Simba Shomari Kapombe alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kutoa pasi mbili za mabao kwa Jean Ahoua na Ladack Chasambi.

Mchezo mwingine  ulikuwa ni timu ya  Mashujaa iliwakaribisha timu ya Coastal Union katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Katika mchezo huo timu zote zilicheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu ya kuzitaka alama tatu  muhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mpaka dakika 90 za mchezo huo zinatamatika ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka 0-0. Mchezaji wa Mashujaa Idrisa Stambuli alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Mchezo wa mwisho ulichezwa saa moja jioni mkoani Kagera ambapo Kagera Sugar iliwakaribisha timu ya Tabora United katika uwanja wa Kaitaba.

Mchezo ulianza vyema huku wachezaji wote wakionyesha ari ya kuzipambania timu zao  ambapo dakika 45 za mchezo huo zilitamatika kwa sare ya kutokufungana .

Kipindi cha pili kilianza ambapo dakika ya 52 mchezaji wa Tabora United, Offen Chikola alifungua ukurasa wa mabao na dakika ya 77 mchezaji  Andy Bikoko aliiongezea bao timu yake ya Tabora United  na dakika chache kabla ya mchezo kutamatika mchezaji wa Kagera Sugar, Cleophace Mkandala aliifungia timu yake bao la kufutia machozi hivyo mchezo kutamatika kwa 2-1.

Mchezaji wa Tabora United Offen Chikola alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kufunga bao moja na kutoa pasi ya mwisho katika mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho kwa mchezo mmoja ambapo timu ya JKT Tanzania itawakaribisha timu ya Singida Black Stars katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni mkoani Dar es Salaam.

 

 

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *