Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Machi 26, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Ligi Kuu ya NBC
Mechi Namba 85: Pamba Jiji FC 1-1 Simba SC

Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi) kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu wakati wakitoka kiwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo huo.Hii ni mara ya pili ndani ya kipindi cha miezi miwili ambapo Februari 25, 2026 mashabiki wa klabu hiyo walimrushia chupa za maji mchezaji wa klabu ya Dodoma Jiji, William Edgar wakati mchezo huo ukiendelea kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu na mazingatio ya kosa la kujirudia.
Mechi Namba 110: TRA United FC 0-0 Young African SC
Klabu ya TRA United ya mkoani Tabora imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la wachezaji wake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano (5) katika mchezo mmoja, ambapo wachezaji hao walionyeshwa jumla ya kadi sita (6) kwenye mchezo tajwa hapo juu.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:10 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 126: Mtibwa Sugar FC 1-1 Young Africans SC

Mchezaji Djigui Diarra wa klabu ya Young Africans amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la kumshambulia mwamuzi wakati wa mchezo tajwa hapo juu, mara baada ya mchezo huo kumalizika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.Mchezaji Djigui Diarra wa klabu ya Young Africans ametozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la kuonesha kidole cha kati wakati akitoka uwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo tajwa hapo juu.
Diarra ametenda kosa kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.4) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji, kwa sababu kitendo hicho kinaashiria matusi na dharau.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Gilbert Mrina kutoka Kilimanjaro,ameshushwa Daraja la Uamuzi kwa kosa la kushindwa kuchukua hatua stahili kwa mchezaji Djigui Diarra kwa kitendo chake cha utovu wa nidhamu (kumshambulia mwamuzi) kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kuwa ni kosa la kujirudia ambapo mwamuzi Gilbert Mrina alitenda kosa la aina hiyo katika mchezo namba 65 wa Ligi Kuu ya NBC (Mbeya City vs Namungo) na akaadhibiwa kwa kufungiwa mizunguko mitatu (3).Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Mwamuzi msaidizi namba mbili (2) wa mchezo tajwa hapo juu, Abdulaziz Ally kutokaArusha, amefungiwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheriaza mpira wa miguu ambapo katika dakika ya 36 ya mchezo alinyoosha kibendera juu kuashiria kulikuwa na kosa la kuotea kabla ya mchezaji Emmanuel Mwanengo wa Young Africans kupokea pasi kutoka kwa Pacome Zouzoua. Hata hivyo, hakukuwa na kosa la kuotea kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwaWaamuzi.
Imetolewa na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
Tuwasiliane kisaikolojia na marefa wetu wanafanya kazi nzuri sana tukifanya hivyo kabla ya michezo kutawaongezea kujiamini nakuona Wao ndo wenye mamlaka na mchezo husika kuwa wenye mvuto Kwa wapenzi wa soka ndani na nje ya nchi