MCHEZAJI wa Namungo Anthony Mligo amesema kuwa ubora wa Ligi Kuu ya NBC umefanya ligi hiyo kuwa ngumu kutokana na kila timu kupambana kuhakikisha inapata matokeo ya ushindi.
Akizungumza wakati wa siku ya kuongea na vyombo vya Habari kwa timu ya Namungo, Mligo amesema kuwa Ligi ya NBC imekuwa ngumu na hili linajidhihirisha ubora wake kutokana na ubora uliosababishwa na ligi hiyo kupanda viwango vya ubora barani Afrika.
“Timu nyingi zipo vizuri kwa sababu zina wachezaji wazuri ndio maana ushindani ni mkubwa hivyo sisi tunaendelea kupambana japokuwa hali yetu sio nzuri “Amesema Mligo.
“Sisi kama wachezaji tunaendelea kujituma na tusikate tamaa kwani Kocha anajua nini anatakiwa kutupatia ili tuweze kurejesha ubora wetu na kuifanya timu yetu irudi kuwa imara zaidi’’ Aliongeza.
Aidha mchezaji huyo amesema kuwa ushindani wa namba uliopo Namungo unamfanya azidi kupambana zaidi ili aweze kuwa chaguo namba moja la kocha na kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
“Kwenye kila timu kuna ushindani wa namba hivyo mimi sihofii ushindani bali nachukulia kama chachu yakupambana zaidi ili niweze kuzidi kupata nafasi ya kucheza kwani mchezaji anaecheza nae nafasi moja ni mzuri pia.
Tukio ambalo mchezaji huyo hawezi kulisahau amesema ni wakati akianza kucheza alipata timu ya Ligi daraja la pili Zanzibar akaenda kucheza lakini ukata wa timu hiyo ulimfanya afyeke majani katika eneo la Fumba ili aweze kupata nauli ya kurudi nyumbani Pamoja na pesa ya kujikimu.
“Nilipohitimu kidato cha nne nilimwomba Mama aniruhusu niende nikacheze Zanzibar ligi daraja la pili kwa bahati mbaya timu hiyo ilikuwa na ukata ilinilazimu kuacha mpira nikajikuta nafyeka majani ili niweze kupata mahitaji yangu na pesa ya nauli ya kurudi nyumbani Tanga mpaka sasa sijawahi kumwambia Mama kilichonikuta kwani alijua nilikuwa nacheza huko” Alisema Mligo.