Author: Honest Mwanitega

TABORA, COASTAL KUKIWASHA LEO, AZAM KUJIULIZA NYUMBANI.

TIMU ya Tabora United iliyopo kwenye muendelezo mzuri wa matokeo leo inashuka dimbani kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora dhidi ya Coastal union ya Tanga saa 10:00 alasiri.

Tabora inaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata matokeo ya ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wake uliopita nyumbani dhidi ya Azam ya Dar es Salaam.

Coastal inakutana na Tabora ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya Fountain kwa mabao 3-2 kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.

Mchezo wa mwisho leo utakuwa kati ya Azam FC dhidi ya Fountain Gate FC kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar saa 1:00 usiku.

Azam itajaribu kupata ushindi leo ikiwa ni baada ya kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya Tabora United huku Fountain ikijaribu kuendeleza matokeo mazuri ya ushindi baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Coastal nyumbani.

MTIBWA, TMA, MBEYA CITY WABABE WA MABAO NBC CHAMPIONSHIP.

IKITIMIZA mizunguko tisa tangu kuanza Ligi ya NBC ya Championship inazidi kushika kasi huku timu za Mtibwa Sugar, TMA na Mbeya City zikiongoza kwa kufunga mabao hadi sasa.

Hadi sasa timu hizo zimefanikiwa kufunga mabao 15 huku Mtibwa ikiruhusu mabao manne, TMA ikiruhusu nane na Mbeya City ikiruhusu mabao 11.

Kiluvya iliyopanda daraja kutoka Ligi ya First League ndio timu iliyofunga mabao machache hadi sasa ikifunga manne huku ikiwa timu iliyofungwa mabao mengi (15) na kushika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi ya NBC championship hadi sasa.

Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu ya NBC msimu uliomalizika hadi sasa inashikilia uongozi wa NBC Championship ikiwa na alama 20 sawa na Geita Gold iliyoshuka kutoka Ligi Kuu pia.

YANGA KUJIULIZA KWA TABORA LEO.

BAADA ya kupoteza dhidi ya Azam, leo timu ya Yanga inashuka uwanjani kuikaribisha Tabora United ya Tabora saa 12:00 jioni kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar.

Yanga iliyopoteza mchezo uliopita nyumbani leo itakuwa tena mwenyeji wa Tabora iliyopata ushindi kwenye mchezo wake uliopita dhidi ya Mashujaa kwa bao 1-0.

Yanga itajaribu kupata ushindi leo ili kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kupoteza nafasi hiyo inayoshikiliwa na Simba kwa sasa baada ya kushinda mchezo wa jana dhidi ya KMC.

Hadi sasa Yanga imefungwa mchezo mmoja na bao moja pekee ikiwa timu ya pili kwa wastani mzuri wa mabao (12) nyuma ya Simba yenye (18).

LAKE TANGANYIKA KUWAKA MOTO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kwa mchezo kati ya Mashujaa itakayokuwa mwenyeji wa Simba saa 10:00 alasiri.

Mashujaa iliyopoteza mchezo mmoja pekee msimu huu sawa na Simba inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Fountain Gate ugenini.

Mashujaa imeshinda michezo mitatu na kutoa sare minne hadi sasa inakutana na Simba iliyoshinda michezo sita ya Ligi Kuu ya NBC na kutoka sare mchezo mmoja pekee.

Simba inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kuishusha Singida Black Stars na kupanda hadi nafasi ya pili kwa tofauti ya wastani wa mabao.

YANGA YAKWEA KILELENI KWENYE MSIMAMO WA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Yanga imeendeleza ubabe msimu huu baada ya kushinda mchezo wa nane mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC kwa bao moja ugenini dhidi Singida Black Stars.

Bao pekee la Yanga lilifunga na Pacome Zouzoua na kufanya Singida kupoteza mchezo wake wa kwanza msimu huu.

Yanga imecheza mchezo wake wa nane msimu huu bila kuruhusu bao lolote huku ikiwa imefunga jumla ya mabao 13.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha jumla ya alama 24 na kuongoza Ligi Kuu ya NBC baada ya kucheza michezo nane.

Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa kwenye uwanja wa KMC, Dar kati ya KMC na Namungo