Author: Honest Mwanitega

MICHEZO YA JKT LIGI KUU YA NBC YAAHIRISHWA.

MCHEZO wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Simba dhidi ya JKT Tanzania uliopaswa kuchezwa kesho Oktoba 29 umeahirishwa kutokana na timu ya JKT Tanzania kupata ajali ya basi eneo la Mbweni Dar es Salaam wakitokea Dodoma jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Afisa Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Ligi Tanzaia (TPLB), Karim Boimanda amesema kuwa baada ya kupokea taarifa ya ajali hiyo Bodi ya Ligi ilifanya mawasiliano na timu ya JKT na pia ilipokea taarifa ya Daktari aliyewapokea majeruhi na iliwasiliana na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF kupitia kamati ya Tiba ya Shirikisho hilo ambapo Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Manfred Limbanga alikwenda hospitali kuwaona majeruhi ambapo alikuta wanaendelea vizuri.

Sambamba na hilo Boimanda alisema kuwa mchezo wa Ligi Kuu kati ya Namungo dhidhi ya JKT uliopaswa kuchezwa November 4 katika Uwanja wa Majaliwa Ruangwa Lindi umeahirishwa na michezo yote miwili itapangiwa tarehe nyingine.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inawatakia kheri majeruhi wote wa ajali hiyo na kuwaombea wapone haraka waweze kurejea katika majukumu yao ya kila siku.

LIGI KUU NBC YAZIDI KUSHIKA KASI

LIGI Kuu ya NBC inazidi kushika kasi ikiwa ni mzunguko wa 9 wa ligi hiyo ambayo ni Ligi ya 6 kwa ubora barani Afrika na ya kwanza kwa ubora katika ukanda wa CECAFA na pili kwa ukanda wa nchi za kusini mwa Afrika ikiwa nyuma ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Ubora wa Ligi Kuu ya NBC umeletwa na ushindani wa klabu 16 zinazoshiriki Ligi hiyo ambazo kila mmoja amekuwa akicheza kwa malengo ya kuleta ushindani huku kila timu ikitaka kuondoka na pointi 3 kwa kila mchezo husika.

Mpaka sasa timu hizo 16 za Ligi Kuu ya NBC zimeweza kufanikiwa kufunga mabao 133 ikiwa ni katika michezo 68 iliyochezwa katika ligi hiyo.

Fountain Gate ndio kinara wa kufunga mabao wakiwa wamefanikiwa kufunga mabao 17 na kuruhusu mabao 15 huku Simba wakiwa na mabao 16 wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu, timu ya tatu ni Singida Black Stars wakiwa na bao 13 wakiruhusu mabao matatu na Yanga wamefunga mabao 12 sawa na Azam huku yanga wakiwa hawajaruhusu bao lolote na Azam wakiwa wameruhusu mabao matatu.

Timu zenye mabao machache ni KenGold iliyofungwa mabao matano na kufungwa 17, Pamba jiji imefunga matatu na kuruhusu 11, Kagera Sugar imefunga manne na kufungwa tisa huku Namungo ikifunga manne na kufungwa 11.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo jumatatu kwa michezo miwili ambapo mchezo wa kwanza utachezwa saa 10 alasiri kati ya Fountain Gate na Mashujaa katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara na Saa 1:00 usiku Namungo watawakaribisha Pamba Jiji katika Uwanja wa Majaliwa Ruangwa.

BALEKE AIBEBA YANGA LIGI KUU YA NBC

MSHAMBULIAJI wa Yanga Jean Baleke ameibeba timu yake baada ya kufunga bao na kuiwezesha timu hiyo kupata pointi 3 muhimu kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Coastal Union uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana.

Ilimchukua dakika 25 Baleke kuipa timu yake bao katika mchezo ulioonekana mgumu kwa timu zote ambapo zilikuwa zikishambuliana kwa nguvu kabla ya kona kupigwa kuelekea lango la Coastal na kumfanya Baleke kuweza kufunga mpira huo .

Aidha mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa Kocha Juma Mwambusi aliyetangazwa hivi karibuni kama Kocha Mkuu wa Coastal Union ambaye baada ya mchezo huo alisema kuwa amepoteza mchezo kwa mpinzani mgumu anarudi kukaa na timu yake kujitathimini wapi walikosea ili waweze kujirekebisha.

Kwa upande wa Kocha wa Yanga Miguel Gamondi alisema kuwa Ligi Kuu ya NBC msimu huu imekuwa ngumu zaidi kupata matokeo ya kufunga mabao mengi kwani timu zote zinajiandaa vizuri na ikumbukwe kuwa Ligi Kuu ya NBC ni ligi ya 6 kwa ubora barani Afrika.

SIMBA YAMKARIBISHA MGUNDA, AZAM, SINGIDA ZIKITAMBA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Simba imemkaribisha kwenye Ligi Kuu ya NBC kocha mpya wa Namungo Juma Mgunda baada ya kuifunga timu hiyo 3-0 katika mchezo uliochezwa uwanja wa KMC Dar es Salaam.

Ilimchukua dakika 5 tu mlinzi wa kulia wa Simba Shomari Kapombe ambaye pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kufungua ukurasa wa mabao baada ya kufunga kabla ya kiungo wa timu hiyo Jean Ahoua kufunga bao la pili dakika ya 34 hivyo kuifanya Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo kiungo wa timu hiyo Debora Fernandes aliweza kuongeza bao la 3 dakika ya 84 ya mchezo huo hivyo kufanya matokeo kuwa 3-0 ikiwa ni mechi ya kwanza mara baada ya Juma Mgunda kutajwa kurithi mikoba ya Mwinyi Zahera kama kocha mkuu wa timu hiyo.

Michezo mingine iliyopigwa imeshuhudia Singida Black Stars ikiifunga Fountain Gate mabao 2-0 kwenye uwanja wa Liti, Singida huku Azam ikipata ushindi mnono wa mabao 4-1 nyumbani dhidi ya timu ya KenGold ya Mbeya kwenyw uwanja wa Azam Complex, Dar.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho ambapo Coastal Union itawakaribisha Yanga katika Uwanja wa Sheikhe Amri Abeid jijini Arusha,Prisons watawakaribisha KMC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Dodoma Jiji watawakaribisha JKT Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma

SIMBA KUWAKARIBISHA NAMUNGO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC iliyo nafasi ya 6 kwa ubora barani Afrika leo inaendelea kwa michezo mitatu itakayochezwa jijini Dar es Salaam na mkoani Singida.

Mchezo wa kwanza utachezwa majira ya saa nane mchana katika Uwanja wa Liti mkoani Singida, ukizikutanisha timu za Singida Black Star na Fountain Gate.

Fountain itawakosa washambuliaji wake wawili muhimu Seleman Mwalimu na Wiliam Edgar ambao wameitwa timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya michezo ya kufuzu CHAN 2024 dhidi ya Sudan .

Mchezo wa pili utachezwa saa 10 jioni katika Uwanja wa KMC Dar es Salaam ambapo timu ya Simba iliyopo nafasi ya 3 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 16 itaikaribisha timu ya Namungo kutoka Ruangwa iliyo nafasi ya 13 ikiwa na alama 6.

Mchezo wa tatu utachezwa majira ya saa 1 jioni Azam inayoshika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 15 itakuwa mwenyeji wa timu ya Ken Gold kutokea Mbeya inayoshika nafasi ya 16 kwenye msimamo ikiwa na alama 4.