Author: Honest Mwanitega

TRANSIT YASHINDWA KUIZUIA STAND NBC CHAMPONSHIP.

LIGI ya NBC ya Championship imeendelea kwa mchezo mmoja uliopigwa uwanja wa Mabatini, Pwani kati ya Transit Camp ya Dar iliyochezea ‘kichapo’ cha mabao 3-0 kutoka kwa Stand United ya Shinyanga.

Mchezo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku Stand ikitangulia kupata bao mapema lililoipa uongozi hadi kipindi cha kwanza kwanza kinamalizika likifungwa kwa mkwaju wa penati kupitia kwa Kigi Makasi.

Kipindi cha pili Stand ilijihakikishia ushindi kwa mabao mawili yaliyofungwa na Seleman Seif na Omar Issa na kuifanya Stand kumaliza mchezo huo kwa kukusanya alama zote tatu na bila kuruhusu wavu wao kuguswa.

Matokeo hayo yanaifanya Stand kupaa hadi nafasi ya nne ya msimamo wa ligi ya NBC ya Championship baada ya kukusanya jumla ya alama 35 nyuma ya vinara Mtibwa Sugar wanaoshikilia usukani wa ligi hiyo wakifuatiwa na Geita Gold na Mbeya City.

MBIO ZA UFUNGAJI BORA ZAPAMBA MOTO LIGI KUU YA NBC.

MZUNGUKO wa 16 umekamilika kwa timu zote za Ligi Kuu ya NBC huku vita ya kuwania ufungaji bora ikizidi kushika kasi na Elvis Rupia akiendelea kushikilia usukani wa kinyang’anyiro hicho.

Rupia anaongoza baada ya kupachika mabao nane hadi sasa na kuisaidia timu yake kufikisha alama 30 na kukaa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Clement Mzize wa Yanga, Jean Ahoua na Leonel Ateba wa Simba wanafuatia wakiwa na mabao saba kila mmoja huku Ateba akifunga penati nne na Ahoua akifunga tatu.

Selemani Mwalimu aliyekuwa Fountain Gate na kusajiliwa na ‘Miamba’ ya soka nchini Morocco Wydad Casablanca amefunga mabao sita sawa na Pacome Zouzoua wa Yanga.

Prince Dube wa Yanga, Edger William wa Fountain Gate na Peter Lwasa wa Kagera Sugar wanafunga msimamo huo wa vinara wa mabao wakiwa na mabao matano kila mmoja.

YANGA MGUU MMOJA NDANI ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu ya NBC timu ya Yanga imefanikiwa kupata ushindi wa bao moja ugenini dhidi ya AL Hilal na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Stephane Aziz Ki ndiye aliyepeleka furaha kwa ‘Wananchi’ baada ya kuipatia bao dakika ya saba kwa shuti kali la nje ya boksi na kuifanya Yanga kukusanya alama zote tatu kutoka nchini Mauritania na kurudi nazo nchini Tanzania.

Yanga inayoshika nafasi ya tatu inahitaji matokeo ya ushindi dhidi ya MC Algers inayoshikilia nafasi ya pili ikiizidi Yanga alama moja ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Yanga inasaka hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita ambapo iliondolewa kwenye hatua ya robo fainali na timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

VINARA WA LIGIKUU YA NBC WAFUZU ROBO FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA.

TIMU ya Simba inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupata sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya timu ya Bravos de Marquiz ya Angola.

Leonel Ateba ndiye alikuwa shujaa wa Simba baada ya kusawazisha bao dakika ya 69 lililoifanya timu yake kufikisha alama 10 ambazo haziwezi kufikiwa na Bravos waliopoteza mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Simba nchini Tanzania huku timu ya Sfaxien ikiburuza mkia bila alama .

Simba imefunga bao kwenye kila mchezo wa kombe la shirikisho msimu huu huku ikipoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya CS Constantine.

Vinara hao wa Ligi Kuu ya NBC wanatarajiwa kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya CS Constantine kwenye uwanja wa Mkapa, Dar na endapo watafanikiwa kushinda mchezo huo watafuzu hatua ya robo fainali kama vinara kwenye kundi lao.

 

FEISAL BINGWA WA KUPIKA MABAO LIGI KUU YA NBC.

KIUNGO wa Azam FC Feisal Salum ameendelea kuonyesha ubora aliokuwa nao msimu uliopita ambapo hadi sasa kiungo huyo anaongoza msimamo wa kutoa pasi nyingi zilizozaa mabao (9).

Feisal hadi sasa ameongeza pasi mbili za mabao zaidi ya alizimaliza nazo msimu uliopita ambapo alitoa pasi saba huku kinara akiibuka Kipre Junior aliyekuwa akicheza timu moja na Feisal.

Jean Ahoua wa Simba anamfuatia Feisal kwa karibu akiwa nazo tano sawa na winga wa Fountain Gate Salum Kihimbwa.

Ki Aziz, Pacome Zouzoua na Clement Mzize wa timu ya Yanga wanafuatia wakiwa na pasi nne kila mmoja sawa na Josephat Arthur Bada wa Singida Black Stars mwenye pasi nne pia.

Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kurejea Machi, 2025 kushuhudia namna vita hii ya kupika mabao itakavyokamilika ikipisha michuano ya CHAN inayoandaliwa Tanzania.