Author: Honest Mwanitega

BALEKE AONGOZA MBIO ZA UFUNGAJI LIGI KUU YA NBC.

MBIO za kuwania kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/24 zimeendelea kupamba moto huku michezo mitano ikiwa imekamilika kwa kila timu.

Jean Baleke wa Simba ndiye kinara wa ufungaji akiwa na mabao matano huku akifanikiwa kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja (Hat-Trick) dhidi ya Coastal Union.

Feisal Salum wa Azam anashika nafasi ya pili akiwa na mabao manne huku akiwa amefunga mabao matatu katika mchezo mmoja dhidi ya Tabora United kwenye mchezo wa ufunguzi.

Pacome Zouzoua, Ki Aziz, Maxi Nzengeli wa Yanga na Matheo Anthony wa Mtibwa Sugar wanafuatia nafasi ya tatu wakiwa na mabao matatu kila mmoja.

SIMBA YAKAA KILELENI, SINGIDA IKITAMBA LIGI KUU NBC.

TIMU ya Simba imeshinda mchezo wa nne mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu na kukaa nafasi ya kwanza kwenye msimamo baada ya kuifunga Tanzania Prisons ya Mbeya mabao 3-1 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mabao ya Clatous Chama, John Bocco na Saidi Ntibazonkiza yameifanya Prisons iliyokuwa ya Kwanza kupata bao kupitia kwa Edwin Balua kupoteza mchezo wa tatu msimu huu unaowaweka nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Singida Big Stars imepata ushindi wa kwanza msimu huu ikicheza uwanja wa Manungu, Morogoro ugenini baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0.

Bao la Singida limefungwa na Elvis Rupia na kuifanya Singida kufikisha alama tano na kupanda mpaka nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo miwili kati ya Tabora United na Dodoma Jiji saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora huku mchezo wa pili ukiwa Coastal Union dhidi ya Azam Fc kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga saa 1:00 usiku.

WASHINDI TUZO ZA MWEZI SEPTEMBA LIGI KUU YA NBC.

KAMATI ya tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemtangaza mchezaji wa timu ya KMC ya Dar Waziri Junior kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya NBC kwa mwezi Septemba akiwashinda Jean Baleke wa Simba na John Nakibinge wa Tabora United.

Waziri ameifungia timu yake mabao mawili na kuisaidia kushinda michezo miwili ya mwezi Septemba dhidi ya JKT Tanzania na Geita Gold.

Kamati hiyo pia imemtangaza kocha wa KMC Abdihamid Moalin kuwa kocha bora wa mwezi baada ya kushinda michezo yote miwili KMC waliyocheza kwa mwezi Septemba.

Moalin amewashinda Roberto Oliveira wa Simba na Abdallah Mohamed wa Mashujaa baada ya kukusanya alama sita na kupanda kutoka nafasi ya 14 mpaka ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Aidha kamati imemtangaza meneja uwanja wa Azam Complex Amir Juma kuwa meneja bora wa uwanja kwa mwezi Septemba.

 

 

 

MBEYA KWANZA, MBUNI ZAPETA NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU za Mbeya Kwanza na Mbuni zimecheza michezo minne ya Ligi ya NBC Championship bila kupoteza baada ya kila moja kupata ushindi leo.

Mbeya Kwanza inayotumia uwanja wa Nangwanda Sijaona imeifunga Kengold ya Mbeya kwa bao moja kwenye mchezo uliochezwa mapema saa 8:00 mchana.

Mbuni imepata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Cosmopolitan kwenye uwanja wa Uhuru na kuifanya Cosmo iliyotwaa ubingwa wa First League msimu uliopita kucheza michezo minne bila kupata ushindi.

Mbeya Kwanza imepanda mpaka nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship ikifikisha alama 10 sawa na Mbuni huki Mbeya Kwanza akiongoza kwa tofauti ya mabao mawili.

Mchezo mwingine ulipigwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro na kushuhudiwa Ruvu Shooting ikifungwa bao moja na Mbeya City na kuifanya Ruvu kuwa timu pekee ambayo haijapata alama msimu huu ikifungwa michezo yote na kushika nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi hiyo.