Author: Honest Mwanitega

YANGA YATANGULIA FAINALI NGAO YA JAMII.

TIMU ya Yanga imefanikiwa kufuzu fainali ya Ngao ya Jamii baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Azam katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Azam iliyokuwa imejichimbia nchini Tunisia kwa maandalizi ya msimu mpya imeshindwa kutamba na kuruhusu mabao hayo mawili yaliyofungwa na Stephane Aziz Ki na Clement Mzize walioingia kipindi cha pili.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kusubiri timu itakayopoteza nusu fainali ya pili hapo kesho kati ya Simba na Singida Big Stars ili kucheza na kutafuta nafasi ya mshindi wa tatu.

Timu ya Yanga itasubiri mshindi kati ya Simba na Singida ili kucheza fainali itakayopigwa Agosti 13 kwenye uwanja wa Mkwakwani na kujaribu kutetea taji hilo baada ya kulitwaa kwa miaka miwili mfululizo iliyopita.

LIGI KUU RASMI AGOSTI 15.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imetangaza rasmi ratiba ya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 utakaoanza Agosti 15, na kutamatika Mei 29, 2024.

Michezo ya ufunguzi itaanza Agosti 15 ikiwakutanisha Ihefu na Geita Gold uwanja wa Highland Estate, Namungo na JKT Tanzania uwanja wa Majaliwa na Dodoma Jiji dhidi ya Coastal Union uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ligi hiyo itaendelea Agosti 16 kwa michezo miwili ambapo Mashujaa dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Lake Tanganyika na Azam FC dhidi ya Kitayosce uwanja wa Azam Complex huku Agosti 17 Mtibwa Sugar itawakaribisha Simba uwanja wa Manungu Complex wakati Agosti 22, Singida BS itacheza na Tanzania Prisons uwanja wa Liti na mchezo wa mwisho wa raundi hii utawakutanisha Yanga na KMC uwanja wa Azam Complex Agosti 31.

Mchezo wa watani wa jadi wa Kariakoo unaokutanisha Simba na Yanga utachezwa Novemba 5 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa saa 11 jioni.

Akizungumza na waandishi wa Habari Afisa Mtendaji mkuu wa Bodi hiyo Almasi Kasongo amesema ratiba imezingatia ushiriki wa timu za Yanga, Simba, Azam na Singida BS kwenye Michuano ya kimataifa.

“Ugumu wa upangaji wa ratiba msimu huu umetokana na uwepo wa michuano ya kimataifa kwa ngazi ya Klabu na timu za taifa hivyo kusababisha ratiba yetu kuchelewa” alisema Kasongo.

Aidha Kasongo amesisitiza juu ya ubora wa viwanja vitakavyotumika kwenye Ligi Kuu msimu huu akisema Bodi haitasita kufungia kiwanja chochote endapo kitashindwa kukidhi ubora unaohitajika kikanuni.

KASONGO AWAITA MADAKTARI VIWANJANI

AFISA Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Almasi Kasongo ameushauri uongozi wa Chama cha Madaktari wa Michezo nchini (TASMA) kutengeneza mazingira rafiki yatakayovutia madaktari wengi zaidi wanaofanya kazi katika Hospitali mbalimbali.

Amesema hayo alipokuwa akifungua Semina ya madaktari wa michezo inayofanyika Mkoani Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Tufungue milango ili tuwape nafasi madaktari wanaohudumu katika hospitali zetu ili waweze kuingia kwenye mpira wa miguu kupitia Chama hiki lengo ikiwa kuwapa nafasi ya kuhudumia wachezaji na mashabiki wanaohudhuria viwanjani” amesema Kasongo.

Aidha Kasongo amesisitiza klabu zinazoshiriki Ligi zote msimu ujao kusimamia vizuri eneo la tiba na afya kwani ni eneo muhimu katika utekelezaji wa masharti ya leseni za klabu.

“Ni muhimu klabu zote kuwa na wataalamu wa afya wenye ubobezi, utaalamu na uzoefu wa kutosha kazini ili michezo ichezwe katika hali ya usalama kwani hakuna timu itakayoshiriki mashindano ya msimu ujao bila kuwa na mtaalamu wa afya aliekidhi vigezo vyote” aliongeza Kasongo.

Mafunzo hayo ya ngazi ya juu kwa madaktari wa michezo yaliyoandaliwa na TASMA yatafanyika kwa siku saba lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo maradufu madaktari hao katika matibabu ya wachezaji na mashabiki viwanjani.

RATIBA ZA MASHINDANO ZATAMBULISHWA.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania imetangaza tarehe za matukio yote ya msimu mpya wa 2023/24 ikiwa ni pamoja na siku za kuanza kwa Ligi Kuu ya NBC, Championship na First League.

Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kuanza Agosti 15 ikitanguliwa na michezo ya Ngao ya Jamii itakayochezwa mkoani Tanga kuanzia Agosti 9 mpaka Agosti 13 .

Ligi ya Championship iliyopokea timu tatu ngeni za TMA Stars, Cosmopolitan na Stand United kutoka ligi ya First League inatarajiwa kuanza Septemba 2 ikiwa ni siku 17 baada ya kuanza kwa Ligi Kuu ya NBC.

Ligi ya First League inatarajiwa kuanza Oktoba 21 huku hatua ya Nane Bora ya ligi hiyo ikitarajiwa kuanza Aprili 10.

Michezo ya Ligi Kuu ya NBC itakua mbashara kupitia chaneli za Azam huku ikisikika kwa njia ya redio kupitia kituo cha TBC.

HAWA HAPA NYOTA WAPYA LIGI KUU YA NBC.

DIRISHA la usajili msimu mpya wa 2023/24 kwa klabu za Ligi Kuu ya NBC, Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake lilifunguliwa Julai Mosi ili kuruhusu timu kuhamisha wachezaji kutoka timu moja Kwenda nyingine.
 
Timu mbali mbali za Ligi Kuu zimeendelea kujiimarisha kwa kutangaza wachezaji na makocha watakaowasimamia katika michezo yao kuelekea msimu mpya.
 
Zifuatazo ni sajili mbalimbali zilizokwisha kutangazwa na  timu za Ligi Kuu ya NBC;
 
SIMBA-  Che Malone Fondoh (Beki)
               Esomba Onana (Mshambuliaji)
               Aubin Kramo (Winga)
                Mikael Igendia (Meneja wa timu)
               Corneille Hategekimana (Kocha wa viungo)
 
YANGA- Miguel Gamondi (Kocha mkuu)
               Nickson Kibabage (Beki)
 
AZAM- Djibril Sillah (Kiungo)
             Feisal Salum (Kiungo)
             Khalifa Ababakar Fall (Kocha wa makipa)
             Ibrahim Diop (Mchambuzi wa mechi kwa njia ya video)
             Allasane Diao (Mshambuliaji)
              Cheikh Sidibe (Beki)
             Bruno Ferry (Kocha msaidizi)
              Jean- Laurent Geronimi (Kocha wa viungo)
 
SINGIDA FOUNTAIN GATE – Yahya Mbegu (Beki)
 
NAMUNGO- Erasto Nyoni (Kiungo)

Timu nyingine 11 zilizosalia bado hazijatangaza usajili wowote huku dirisha likitarajiwa kufungwa Agosti 31.